Serikali yasisitiza kila mmoja atunze mazingira, kupanda miti

NA DIRAMAKINI

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.Philip Isdori Mpango amesema,kila mwananchi anao wajibu wa kuhifadhi, kusimamia na kuyatunza mazingira nchini.

Hayo yamesemwa leo Januari 20, 2023 kupitia hotuba ya Makamu wa Rais iliyosomwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe.Angellah Kairuki (Mb) katika hafla ya kuufahamisha umma mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika Mkoa wa Dodoma.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango akipanda Januari 12, 2023 mti aina ya Msabuni katika shule ya msingi Msalato Jijini Dodoma wakati akiongoza zoezi la upandaji miti kusheherekea Maadhimisho ya Miaka 59 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

"Napenda pia nitumie fursa hii kusisitiza kuhusu suala la uhifadhi na usimamizi wa mazingira. Kazi ya kuhifadhi misitu,kulinda vyanzo vya maji, upandaji miti ya mbao, matunda, miti dawa, kivuli, kupendezesha miji yetu na kufanya usafi ni lazima iwe shirikishi na ya kudumu.

"Nawaomba wananchi wote kuendelea kupanda miti ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na kufaidika na fursa za Uchumi na kijamii.

"Nimesikia hapa kuwa Mkoa wa Dodoma mmeweka mipango ya kutekeleza maelekezo ya Mhe. Makamu wa Rais aliyoyatoa juu ya utunzaji mazingira,"amesema.

Waziri Kairuki kwa niaba ya Makamu wa Rais amesema, kila mmoja anapaswa kupanda miti ili nayo baadaye itutunze. "Na leo nitakwenda kuwakabidhi wadau wa mazingira 51 kwa niaba ya Mhe.Makamu wa Rais maeneo ya kupanda, kutunza miti na kuyapendezesha ili kuhakikisha ndoto ya Dodoma ya kijani inadhihirika.

"Hivyo niwatake kuhakikisha kuwa miti yote inayopandwa itunzwe na ikue. Hakikisheni mifugo inahifadhiwa na haizururi hovyo na kuharibu miti iliyopandwa uyatunze mazingira yetu Dodoma, ili yatutunze,"ameagiza.

Katika hatua nyingine amewashukuru na kuwapongeza Watanzania wote kwa maendeleo yaliyofikiwa katika Mkoa wa Dodoma na Tanzania kwa ujumla. "Uwajibikaji na Uongozi Bora; ndio chachu ya maendeleo yetu,"amesisitiza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news