Watumishi wa afya wasimamishwa kazi kwa mabishano machafu kazini

NA DIRAMAKINI

HALMASHAURI ya Wilaya ya Uyui mkoani Tabora amewasimamisha kazi watumishi wawili wa kada ya afya baada ya kutoleana lugha zisizofaa wakiwa kazini na kusambazwa katika mitandoa ya jamii jambo ambalo ni kinyume na sheria za utumishi wa umma.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake,Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui mkoani Tabora, Dkt.Kija Maige amesema kwamba tukio hilo lilitokea Januari 6, mwaka huu katika Zahanati ya Ishilimulwa Kata ya Bukumbi wilayani humo.

Amewataja watumishi hao kuwa ni Rose Shirima ambaye ni muuguzi mkunga na James Chuchu Mteknolojia wa maabara ambao walikuwa wakibishana na kutoleana lugha zisizofaa kazini hali iliyosababisha taaruki kwa umma.

Dkt.Maige amesema, watumishi hao watapumzishwa kutekeleza majukumu yao ya utoaji wa huduma za afya ili kupisha uchunguzi kwa mujibu wa kanuni 37 ya kanuni za utumishi wa umma ya mwaka 2003.

Amesema kwamba, uchunguzi huo utashirikisha mabaraza ya kitaaluma ambayo ni Baraza la Waunguzi Tanzania na Baraza la Wataalam wa Maabara Tanzania ambapo hatua zaidi zitafuata baada ya kukamilika kwa uchunguzi huo.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui, Dkt. Wendy Robert amesema kuwa, mabishano hayo yalionekana mtandaoni na kusababisha taaruki kubwa kwa wananchi na kusema tayari uchunguzi umeanza kufanyika ili kujua chanzo cha mabishano hayo.

Amesema, mabishano hayo yalitokana na mtaalam wa maabara kugomea kutumia kipimo cha malaria kwa ajili ya kinamama wajawazito kwa madai kilikuwa kimekwisha muda wake jambo ambalo si sahihi.

“Vitendanishi hivyo vinamalizika muda wake wa matumizi Aprili 14, mwaka huu jambo ambalo bado kipimo hicho kinafaa kwa ajili ya kupimia wajawazito kujua wingi wa wadudu wa malaria,”amesema Dkt.Wendy .

Amesema kwamba, kipimo hicho cha malaria chenye namba ya utambuzi iliyosajiwa ni 05EDG025B

Naye Mkuu wa Divisheni ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Wilaya ya Uyui, Hamis Mpume amesema kuwa, watumishi hao watasimama kazi kwa ajili ya kupisha uchunguzi wa tuhuma kwa kuzingatia kanuni na sheria.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news