Waziri Dkt.Mabula, Dkt.Kijazi, RC Makala wafunguka mambo mazito

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Dkt.Angeline Mabula amesema,ni jambo la kusikitisha pale ambapo viongozi wameidhinisha mambo mazuri kwa ajili ya kuendeleza miji, matokeo yake mambo yanaenda ndivyo sivyo.
Mheshimiwa Dkt.Mabula ameyasema hayo leo Januari 6, 2023 jijini Dar es Salaam baada ya kukutana na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kujadiliana kuhusu Mpango Kabambe wa Jiji la Dar es Salaam.

Sambamba na ukwamuaji wa zoezi la urasimishaji ambalo linakwenda kwa kusuasua ili kutoka na maazimio ya uwajibikaji wa kila mmoja wao katika kutekeleza matakwa ya kisheria kwa sababu kumekuwa na hali ya kutegeana.

"Wote ni mashahidi kwa Jiji la Dar es Salaam tunao mpango kabambe, lakini bado ujenzi holela unaendelea, lazima tujiulize wapi tunakwama, tumeuidhinisha wenyewe kwa mbwembwe, lakini bado tunakwama na halmashauri zote zilikuwepo."

Dkt.Mabula amesema, Mpango Kabambe wa Jiji la Dar es Salaam wa mwaka 2016 mpaka 2036 ulitayarishwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana mamlaka za Mkoa wa Dar es Salaam na fedha ambazo zililipwa na Serikali zilikuwa nyingi.

"Na mpango ule uliidhinishwa tarehe 28 Februari 2020, lakini ukatangazwa pia katika Gazeti la Serikali namba 466 la tarehe 16 Juni 2020...ukajadiliwa na ukazinduliwa rasmi katika Mkoa wa Dar es Salaam kwa mbwembwe nyingi tu Desemba 15, 2021 almost mwaka mmoja baada ya mpango kuwa umekamilika.
"Serikali ilitumia hela nyingi kuandaa mpango huu Msingi Mkuu wa utayarishaji wa mipango kabambe ya miji yetu ambayo iko kisheria ni sehemu ya pili kifungu cha (9) kifungu kidogo cha i-vii cha Sheria ya Mipango Miji namba (8) ya mwaka 2007 na kwa mujibu wa kifungu hicho miji yote inapaswa kuwa na mipango kabambe ili kutoa miongozo ya ukuaji wa miji na kutenga maeneo kwa ajili ya matumizi mbalimbali na kudhibiti uendelezaji holela wa miji yetu."

Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula ameongeza kuwa, kila mamlaka ya upangaji inao wajibu wa kisheria kuweka mkakati wa kuzuia uendelezaji usiofuata sheria, kanuni na taratibu akiongeza kuwa bila kufanya hivyo serikali itashindwa kutekeleza mipango iliyowekwa na hivyo kutumia fedha za wananchi vibaya.

Pia ameongeza kuwa Dira ya Mpango Kabambe ni kuwa na Jiji endelevu, lenye ushindani linalotumia rasilimali zake kiufanisi na kuhifadhi mazingira na unaolenga kukukuza utamaduni na kuhifadhi historia yake ya muda mrefu.

Waziri Mabula amewambia wajumbe wa mkutano huo kuwa mpango umeandaliwa kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya 2025 iliyofafanuliwa katika Mpango wa Maendeleo wa 2021-22 hadi 2025-26 na unatoa mwongozo katika utoaji wa maamuzi katika matumizi na maendelezo ya ardhi ili kuhakikisha uendelezaji wenye mpangilio katika ukuaji wa Jiji la Dar es Salaam hadi mwaka 2036.

"Mpango pia unatoa majibu ya changamoto zinazokabili Jiji la Dar es Salaam ikiwemo msongamano wa magari, ujenzi holela, uhaba wa huduma za jamii pamoja na miundombinu.

"Mapendekezo ya mpango kabambe huu yamezingatia uongezaji wa fursa za uwekezaji ambapo mwisho wa siku tutaongeza ajira kupitia miradi mbalimbali ambayo itatekelezwa na pia tunayo baadhi ya maeneo ambayo yamependekezwa katika mpango na mengine yapo kwenye kumbukumbu zetu la kwanza suala la ujenzi wa viwanda.

"Mpango umeeleza maeneo ya ujenzi wa viwanda tunayo Kisarawe 1 na Kimbiji haya yote yametengwa. Kisarewe 2 kulikuwa na viwanja squares mita milioni tatu, lakini square mita milioni mbili tayari tulishagawa kwa mwekezaji ambaye ameshachukua pale kwa hiyo bado tuna squares mita milioni moja.

"Kimbiji tuna squares mita milioni 3.5 ambapo huku pamepangwa, lakini tunazo barabara za mzunguko katika Manispaa ya Ilala na Ubungo ziko kwenye master plan utekelezaji bado, uboreshaji wa Mto Msimbazi katika hili tumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa sababu baada ya kuwa tumeweka kwenye mpango kabambe utekelezaji wake umeanza, makubaliano na Benki ya Dunia tayari yamekwishafikiwa, lakini uboreshaji wa mitaro tayari unaendelea na master plan imeandaliwa kwa ajili ya kuwa na daraja pale na lile bonde litakuwa historia nzuri,"amefafanua Mheshimiwa Dkt.Mabula.
Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula ameongeza kuwa, mpango huo unatoa majibu ya changamoto zinazolikabili jiji ikiwemo msongamano wa magari, ujenzi holela, uhaba wa huduma za jamii na miundombinu.

"Awamu ya Sita chini ya Rais Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeelekeza msukumo mkubwa katika Sekta ya Uwekezaji kwenye sekta ya viwanda na ujenzi wa miundombinu.

"Ukamilishaji wa mpango kabambe ni hatua muhimu sana kupitia azimio hilo katika kupanua miji yetu. Aidha, wizara yangu imekuwa ikisisitiza kila mamlaka za upangaji kuandaa mpango kabambe wa eneo lake ikiwa ni pamoja na kuandaa mipango ili kwenda na kasi hiyo kupitia uwekezaji wote tunajua Mheshimiwa Rais amefungua milango ya uwekezaji...

"Uwekezaji unatakiwa kufanyika hapa nchini, maeneo tumeyatenga ndani ya master plan yetu, lakini je? Tumeshakamilisha mchakato mzima wa kuyapima? Tumeshakamilisha suala la utoaji hati? Tumeshakamilisha suala la utoaji fidia? Au tunangoja mwekezaji akifika tuanze kufukuzana na wananchi?."

"Hilo ni suala lenu kamati za mipango miji, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa (CPA Amos Makala), mpango kabambe uliopo katika Jiji la Dar es Salaam uliandaliwa mwaka 1979 na ukadumu miaka 20 mpaka mwaka 1999 ambao sasa baadaye tulikuja kuhuisha 2016 kutokana na ukuaji kwa kasi wa Jiji la Dar es Salaam, kipindi ambacho hapakuwa na mpango changamoto nyingi zilijitokeza hasa za kijamii, kiuchumi na kimazingira,"amefafanua Mheshimiwa Dkt.Mabula.

Waziri Dkt.Mabula ametaja baadhi ya miradi iliyopendekezwa kuwa ni ujenzi wa viwanda maeneo ya Pugu, Pembamnazi, Kisarawe 2 na Kimbiji, ujenzi wa barabara ya mzunguko katika Manispaa za Ilala na Ubungo, Uboreshaji na uendelezaji wa Bonde la Mto Msimbazi.

Aidha,miradi mingine ni uhifadhi wa maeneo ya kihistoria katikati ya Jiji, mradi wa maji safi katika eneo la Kimbiji, ujenzi wa madampo ya kisasa katika maeneo ya Kisopwa na Lingato,ujenzi wa viwanda vidogo vidogo katika baadhi ya maeneo yaliyofanyiwa urasimishaji.

"Mpango kabambe unalenga kukuza utamaduni na kuhifadhi historia ya muda mrefu tuliyokuwa nayo mpango umeandaliwa kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya mwaka 2025 uliofafanuliwa katika Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano 2021/2022 mpaka 2025 /2026 .

"Mpango huu unatoa mwongozo katika utoaji wa maamuzi katika matumizi ya maendeleo ya ardhi na kuhakikisha uendelezaji wake na mpangilio wa Jiji la Dar es Salaam mpaka 2036 ambapo tutakuwa tumemaliza kipindi hicho sasa na tutakuwa tunafikiria kuuboresha tena kutokana na hali halisi itakavyokuwa kwa wale ambao Mwenyezi Mungu atawajalia kuwepo.

‘’Hadi sasa urasimishaji makazi nchini umefanyika katika mitaa 1961 katika halmashauri 164 za mikoa yote 26. Katika mitaa hiyo jumla ya viwanja 2,338,926 vimebuniwa kupitia michoro ya mipangomiji 7,051,"alifafanua Waziri Dkt. Mabula.

Wakati huo huo, Waziri Dkt.Mabula pia ameongeza kuwa suala la upimaji nalo limefanyika kwa kiasi kikubwa ambapo jumla ya viwanja 1,170,639 vimepimwa na kuidhinishwa ambavyo ni sawa na asilimia 50.4 ya viwanja vyote vilivyopangwa.

Katika hatua nyingine, Waziri Dkt.Mabula amewataka viongozi hao kutambua kuwa,maelekezo mahususi yaliyotolewa na Rais Dkt.Samia wakati akitoa salamu za kufunga mwaka yanapaswa kuzingatiwa na kutekelezwa kikamilifu.

"Ndugu zangu pamoja na salamu za Mheshimiwa Rais alizozitoa kwa Watanzania wote wakati akifunga mwaka na mimi narudia alituambia tuangalie tulikotoka na tunakokwenda, akatuambia mwaka huu ni mwaka wa kazi na anataka kasi iwe kubwa zaidi na pia anasisitiza suala la kuzingatia sheria,taratibu na kanuni.

"Hatuwezi kuwa na mwendelezo wa kazi bila kuzingatia maelekezo ambayo Mheshimwa Rais ameyatoa. Kikao hiki tulikiita kwa lengo la kujadili masuala muhimu yanayogusa sekta ya ardhi ili tuwe na uelewa wa pamoja. Tunayo mengi leo hapa tutayapata kati yenu na sisi.

Katibu Mkuu

Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Allan Kijazi amesema, wizara hiyo iliandaa Sera ya Maendeleo ya Makazi ambayo imeweka mikakati mbalimbali ya kukabiliana na changamoto za ujenzi wa makazi holela.

Dkt.Kijazi amesema, baadhi ya mikakati ambayo imewekwa kwenye sera hiyo ni msingi wa majadiliano ya kikao hicho.

"Mkakati wa kwanza ni kuwezesha wananchi kuunda asasi za kijamii au asasi zisizo za serikali kwa lengo la kuboresha makazi. Mkakati wa pili ni kuandaa mpango maalumu wa kupata fedha kwa ajili ya upangaji,upimaji kwa kuchangia gharama kwa ajili ya upimaji.

"Mkakati wa tatu ni kuhakikisha kwamba upangaji, na upimaji na utoaji wa hati milki za ardhi zinalindwa kwa uendelezaji wa maeneo ya pembezoni inafanyika kikamilifu ili kuzuia ujenzi holela. Mkakati wa nne ni kutenga maeneo maalum kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za gharama nafuu na kuweka katika kiwango cha chini cha huduma ambacho wananchi wanaweza kukimudu kwa kuzingatia hali yao ya kiuchumi.

"Mkakati wa tano ni kuhakikisha kwamba upangaji na utaoji ardhi unazingatia matakwa ya Sheria ya Ardhi sura ya 113 Sheria ya Ardhi ya Vijiji sura 114 na Sheria ya Umiliki wa Ardhi sura 118, hizi ndizo sheria kubwa ambazo zinazingatiwa katika kuhakikisha upangaji na utoaji wa ardhi katika maeneo yetu.

"Mheshimiwa Waziri kwa kuzingatia matakwa ya kisera na sheria, wizara iliandaa programu ya kurasimisha makazi yasiyopangwa ya mwaka 2013 na 2023.

"Lengo mahususi la programu hii ilikuwa ni kuzuia makazi yasiyopangwa yasiongezeke na hili litawezekana tu kwa kutekeleza shughuli mbalimbali za upangaji wa miji kudhibiti ujenzi, upimaji wa maeneo yaliyopangwa, uendelezaji wa maeneo, ushirikishaji wa sekta binafsi na ushirikishaji wa jamii ili kuweza kuboresha makazi yao kwa njia shirikishi.

"Lengo ni kwamba chochote kinachofanyika basi kifanyike kwa njia shirikishi na ndio sababu kubwa tumeona leo tuwashirikishe kujadiliana mambo mambo mbalimbali.

"Mheshimiwa Waziri mwaka 2022 kikao kilifanyika na changamoto mbalimbali ziliibuka, baada ya kikao hicho na wizara iliunda timu ya wataalam kwa ajili ya kupitia changamoto zilizobainishwa na baada ya kupitia changamoto hizo mkakati uliandaliwa utakaobainisha chanzo cha changamoto nini kifanyike ili kuweza kukabiliana na hizo changamoto na tutatumia vigezo gani kuona kwamba programu hii inaleta ufanisi na kuleta matokeo yanayotakiwa katika kuboresha makazi.

"Mheshimiwa Waziri mapendekezo ambayo yameandaliwa na kikosi kazi hicho yatakayowasilishwa katika kikao hiki yataboreshwa ili kuweza kuleta tija pamoja na umuhimu wa kikao hiki kuwa katika mikoa yote.

"Mkoa wa Dar es Salaam una umuhimu wa kipekee kutokana na ukweli kwamba unabeba zaidi ya asilimia 8.5 hadi asilimia 10 kwa Watanzania wote, lakini pia changamoto iliyopo pamoja na kuwa na idadi kubwa ya watu na mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa, lakini ni asilimia 23.5 tu ya makazi yote ambayo yamerasimishwa Dar es Salaam.

"Pamoja na kuwa na kiwango kikubwa cha urasimishaji makazi kiwango cha upimaji wa viwanja katika Jiji la Dar es Salaam ni asilimia 20 pekee, ambapo tunayo asilimia 80 ambayo hatujaifanyia kazi. Jambo hili halileti taswira njema kwa mkoa wetu wa Dar es Salaam.

"Aidha, ilitegemewa kwamba kwenye programu yetu hii ya urasimishaji wananchi wangeweza kuchangia shilingi bilioni 91.6 ili kuweza kuhakikisha kwamba programu hii inafanikiwa, lakini kwa mwamko mdogo wananchi wameweza kuchangia shilingi bilioni 24.6 pekee, hii ni chini kidogo na matarajio.

"Katika kikao cha leo tunaimani kwamba wadau wetu tutaweza kujadiliana na kuweza kuboresha programu hii kwa hapa Dar es laam kwa kutoa mawazo, kwani asilimia 80 bado makazi hayajarasimishwa na bado michango iliyotolewa ni kama robo tu, kwa hiyo tuna haja ya kuweka nguvu ya pamoja kuweza kubooresha,"amefafanua kwa kina Katibu Mkuu Dkt.Allan Kijazi.

RC Makala

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Amos Makala amesema, ofisi yake inafarijika kwa namna ambavyo Waziri Dkt.Mabula anafanya kazi nao bega kwa bega ili kupata matokeo bora.

"Tunapenda kukushukuru Mheshimiwa Waziri kwa namna unavyofanya kazi na ofisi yako ya Mkoa wa Dar es Salaam. Nilipoingia hapa nilikabidhiwa migogoro iliyoshindikana mikubwa mikubwa, Lukuvi (Mkuu wa Mkoa mstaafu Mheshimiwa William Lukuvi) aliita mafupa nataka kukuhakikishia Mheshimiwa Waziri tumeshughulika na migogoro mingi kwa sasa ni kama tunaelekea kuimaliza.

"Tulikutana na migogoro mikubwa, yote hiyo tumeishughulikia vizuri na kila tulichokuwa tunakifanya tulikujulisha Mheshimiwa Waziri, kwa hiyo kama tungekosa sapoti yako ndiyo ile ingekuwa DC anafanya hivi, RC anafanya hivi, Waziri anakuja kurekebisha, lakini nasema migogoro yote tumeishughulikia kama ambavyo ofisi yako inataka.

"Nataka nikuhakikishie naweza kusema kwamba tuna maafisa ardhi waliotusaidia, wapo wanasiasa walitaka kuingilia lakini tulisimama kidete na kikao hiki kimekuja muda mwafaka.

"Kwa hiyo maelekezo ni yale yale unatatua mgogoro unarasimisha, yapo maeneo upande wa wanasiasa waliingilia, lakini tulisimama kwa ajili ya utatuzi kwa haki. Na yapo maeneo wapo wapotoshaji na mimi nasema wasikilize mkuu wa Wilaya na Mkoa anasema nini na sio vinginevyo, sisi ndio tunawapenda zaidi wananchi kuliko hawa wanaowadanganya wananchi.

"Tunapoamua kwamba umevamia eneo tunataka lipimwe, lirasimishwe sisi ndio wenye nia nzuri, akija mtu anakwambia usitoe pesa wala usipimiwe kwa kukuhadaa kwa maneno ya uongo ukakosa hati, mwema ni yule anayesema kaa hapa pimiwa na tukupe hati? Na hilo ndilo tamko letu Serikali tuna nia nzuri zaidi na wananchi tunapowaambia tunarasimisha sisi kama Mkoa wa Dar es Salaam baada ya kujua chanzo cha mgogoro ni nini.
"Wananchi wamepata kujua kupitia mikutano ya hadhara, mimi mkuu wa mkoa nimepita na wakuu wa wilaya wameweka utaratibu katika maeneo yao kukutana na wananchi kwa kiasi kikubwa. Wananchi wamepata kueleza na kushughulikiwa kero zao nataka niseme tu kwamba.

"Tulikopita tulikutana na changamoto kwa sababu unachukua hela za watu huonekeni na hupokei simu, kwa hiyo kikao hiki kimekuja muda mwafaka ili kuhakikisha kwamba wananchi ambao walitoa pesa zao waweze kupata huduma hii,"amefafanua RC Makala.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news