Wizara ya Ardhi yakusanya bilioni 90.91/- nusu mwaka

NA DIRAMAKINI

WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imekusanya jumla ya shilingi bilioni 90,907,939,421 sawa na asilimia 75 ya malengo ya nusu mwaka kutokana malimbikizo waliokuwa wanadaiwa wananchi ambao walisamehewa riba za malimbikizo ya kodi za majengo na ardhi.
Waziri Mhe. Dkt.Angeline Mabula ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema kuwa, hadi kufikia Novemba, 2022 wananchi 2,819 wamenufaika na msamaha wa riba ya malimbikizo ya kodi ya pango la ardhi yenye jumla ya shilingi 6,946,930,272. Idadi hiyo haijumuishi wananchi waliojitokeza ambao wamehudumiwa kuanzia tarehe 1 hadi Desemba 31, 2022.

Amesema kuwa, anawapongeza wamiliki wa ardhi waliojitokeza kunufaika na msamaha uliotolewa na Mhe. Rais na kubainisha kuwa, katika mwezi Desemba, 2022 Wizara ya Ardhi imeshuhudia idadi kubwa ya wamiliki waliojitokeza kulipa na kiasi cha shilingi bilioni 22.6 kimekusanywa katika mwezi Desemba pekee.

Dkt.Mabula amesema kuwa, katika kutatua migogoro ya ardhi, Mamlaka za Serikali za Mitaa zinapaswa kusimamia kikamilifu mipango ya jumla, mipango ya kina na mipango ya matumizi ya ardhi vijijini kupitia kamati za ardhi za vijiji ili kudhibiti ujenzi holela usiozingatia mipango iliyoandaliwa na kuidhinishwa kupitia Kamati za Mipango miji.

“Wizara imekuwa ikipokea taarifa na malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu ukiukwaji wa taratibu mbalimbali zinazohusu usimamizi wa ardhi mijini na vijijini.

"Miongoni mwa malalamiko ni baadhi ya viongozi wa vijiji na mitaa kuuza ardhi kinyume na utaratibu, kukosekana kwa udhibiti wa uendelezaji ardhi katika maeneo ya vijiji na miji. Hali hiyo imesabisha kuongezeka kwa migogoro ya ardhi na uendelezaji ardhi kinyume na mipango iliyoandaliwa na kuidhinishwa,"amesema Dkt.Mabula.

Dkt.Mabula amesema,wizara inaandaa programu maalum ya kufanya ukaguzi wa uzingatiaji wa mipango ya matumizi ya ardhi kwa Mamlaka za Upangaji. "Taarifa hizo zitatolewa kwa umma kama sehemu ya uwajibikaji wa mamlaka zetu kwa wananchi,"amesema.

Kuhusu ujenzi wa vituo vya mafuta, Dkt.Mabuka amesema hadi kufikia tarehe 31 Disemba, 2022 wizara imepokea taarifa ya uendelezaji wa vituo vya mafuta kutoka halmashauri 129 kati ya 184 zilizopo nchini sawa na asilimia 70.1.

Amesema, uchambuzi uliofanywa na Wizara ya Ardhi umebaini katika Halmashauri 129, kuna vituo 2,063 ambapo kati ya hivyo vituo vya mafuta ni 1269 (asilimia 61.6) na vituo vidogo vya mafuta ni 794 (asimilia 38.5) huku vituo 1,868 vimejengwa katika umbali wa zaidi ya mita 200 kutoka kituo kimoja na kingine sawa na asilimia 90.5 kama inavyoelekezwa na kanuni ya viwango vya umbali.

Aidha, Dkt.Mabula amesema kuwa, vituo 195 vimejengwa umbali wa chini ya mita 200 sawa na asilimia 9.5. "Wizara inaendelea kufanya uchambuzi zaidi ili kubainisha vituo ambavyo vimejengwa kabla au baada ya kanuni za mwaka 2018 zinazoendelea kutumika ili hatua stahili ziweze kuchukuliwa,"alisema.

Pia Waziri wa Ardhi alizungumzia suala la programu ya miaka 10 ya urasimishaji makazi holela ambapo Wizara inayo Programu ya Urasimishaji Makazi iliyoanza kutekelezwa mwaka 2013. Programu hiyo mwisho wake ni mwaka huu 2023 na imekuwa ikitekelezwa katika Mitaa 3,397 kwenye Mikoa yote 26.

Dkt.Mabula amesema, mitaa 1,961 imerasimishwa sawa na asilimia 57.7 na mitaa 1,436 haijarasimishwa sawa na asilimia 42.3 na kubainisha kuwa prrogramu hiyo imewezesha upangaji wa viwanja 2,338,926 na kati ya hivyo, viwanja 1,170,638 upimaji wake umekamilika. Aidha, jumla ya milki 177,330 zimeandaliwa na kutolewa kwa wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news