DODOMA INAKALIKA, DODOMA INAPANUKA

NA LWAGA MWAMBANDE

JANUARI 31, 2023 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax ameupongeza Ubalozi wa Ufaransa nchini kwa kufungua Ofisi Ndogo ya Uwakilishi jijini Dodoma na kuzihamasisha balozi nyingine kuendelea kuitikia wito wa kuhamia makao makuu ya nchi.

Akizungumza katika ufunguzi wa ofisi hiyo, Mhe.Dkt.Tax alisema, anaupongeza ubalozi huo kwa kuitikia wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan alioutoa mwanzoni mwa mwaka 2023 wa kuwasihi mabalozi kuhamia makao makuu ya Serikali jijini Dodoma.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema kuwa, uamuzi uliofikiwa na Wafaransa kuweka ofisi zao Dodoma ni ishara na hatua njema ambayo inafaa kuungwa mkono na kila mmoja. Endelea;


1.Hawaji hawaji waja, karibu sana Dodoma,
Ufaransa wamekuja, ubalozi wasimama,
Kwetu sisi ni wateja, watazipata huduma,
Dodoma inakalika, Dodoma inapanuka.

2.Waongezeka wakuja, jiji halijasimama,
Na huduma nyingi zaja, ukizidi usalama,
Na hata wewe ukija, tapata mahali pema,
Dodoma inakalika, Dodoma inapanuka.

3.Ufaransa ni daraja, waliokuwa na homa,
Imekwishajenga hoja, mji mkuu ni mwema,
Tushahamia kimoja, haturudi Dasalama,
Dodoma inakalika, Dodoma inapanuka.

4.Vyuo vikuu ukija, ni vingi vinasimama,
Endapo unayo haja, uje mzimamzima,
Tunahitaji wateja, Chuo Kikuu Dodoma,
Dodoma inakalika, Dodoma inapanuka,

5.Afya hakuna vioja, sipitali ni mlima,
Jenero tunayo moja, ya rufaa yasimama,
Ya Ben Mkapa moja, kubwa sana kwa huduma,
Dodoma inakalika, Dodoma inapanuka.

6.Barabara siyo moja, zinajengeka Dodoma,
Ring Road si viroja, usafiri wawa Mwema,
Endapo wewe ukija, utaipenda Dodoma,
Dodoma inakalika, Dodoma inapanuka.

7.Na kwa vilaji wateja, hapa hakuna kukwama,
Chaguzi zako mteja, ukitaka nyama choma,
Jumla na rejareja, inapatikana nyama,
Dodoma inakalika, Dodoma inapanuka.

8.Reli ndege kwa pamoja, usafiri wawa mwema,
Reli mpya iko moja, kutokea Dasalama,
Kiwanja ndege kimoja, Msalato wimawima,
Dodoma inakalika, Dodoma inapanuka.

9.Ni balozi mojamoja, zitazokuja Dodoma,
Na viwanja si kimoja, vimeshatengwa Dodoma,
Mje kwetu ni wateja, mtazipata huduma,
Dodoma inakalika, Dodoma inapanuka.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news