Jambo letu ni Bunge la Aprili-Msigwa

NA DIRAMAKINI

MSEMAJI Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema, Serikali imesogeze mbele uwasilishaji wa Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari ambao ulipangwa kuwasilishwa katika Bunge linaloendelea ikiwa ni sehemu ya miswada ya mabadiliko ya sheria mbalimbali.

Kwa taarifa hiyo, muswada huo sasa utawasilishwa katika Bunge la Bajeti linalotarajiwa kuanza mwezi Aprili, mwaka huu.

Msigwa ameyasema hayo Februari 7, 2023 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema muswada huo unatarajiwa kufanyia mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari namba 12 ya mwaka 2016.

“Jambo letu tulikuwa tumepanga tuliwasilishe, lakini ndugu zangu imetokea kwamba ratiba ya Bunge imebana sana, hakukupatikana nafasi, kwahiyo tumeshindwa kuwasilisha muswada wa mabadiliko ya sheria hii ya habari.

“Serikali baada ya kusikiliza maoni mbalimbali kutoka kwa wadau wa habari walitaka Sheria ya Huduma za Habari kufanyiwa marekebisho na kweli,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan aliona ni jambo jema ili kila mmoja aweze kufurahi na huduma hiyo.

“Kweli, Serikali imekusanya maoni na hata wanahabari walitoa maoni yao, kwa hiyo kutokana na kupatikana kwa maoni Serikali ilikuwa imekusudia kupeleka marekebisho hayo bungeni ili wabunge waweze kujadili mswada huo.

“Lakini kama mnavyojua kwa sasa bunge hili linaloendelea ni kwa ajili ya kujadili taarifa za kamati za bunge na kwa maana hiyo muda haukuweza kutosha kuweza kujadili mswada huu kwa maana hiyo basi mswada huo mahususi kama JAMBO LETU hautaweza kupeleka bungeni, lakini tunauhakika kwamba Bunge lijalo la mwezi wa nne mswada huo utapelekwa bungeni na utajadiliwa, kwani huko vizuri na umeandaliwa vizuri,”amesema Msigwa.

Pia amesema, maoni yote ya wadau yamezingatiwa na yamefanyiwa kazi kwani wanataka mswada huo uweze kuwafurahisha watanzania wote ili kila mdau wa habari aweze kuwa na uhuru wa sheria hiyo na hiyo ndiyo makusudi njema ya serikali.

Hii ni miongoni mwa hatua nzuri kwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan ambayo imeonesha kuijali Sekta ya Habari kama injini ya kusaidia kusukuma mbele taarifa chanya kwa ustawi bora wa maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.

Pia ishara hii inatoa mwanga kuwa, huenda sheria nyingine zinazolalamikiwa ikiwemo Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Huduma za Posta (EPOCA, 2010), Sheria ya Makosa Mtandaoni (2015), Sheria ya Haki ya Kupata Habari (2016) na Kanuni za Maudhui Mtandao (2018) kama zilivyorekebishwa mara kadhaa huenda nazo zikafanyiwa marekebisho.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news