Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) yatoa ufafanuzi kuhusu kimbunga Freddy

NA DIRAMAKINI

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inapenda kutoa ufafanuzi juu ya taarifa za uwepo wa kimbunga “Freddy” zinazosambaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii na kuzua taharuki kwa jamii.

Picha na weather.com

Kupitia Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na. 2 ya mwaka 2019, Mamlaka imepewa jukumu kisheria kufuatilia na kutoa tahadhari za hali mbaya ya hewa kwa jamii. Taarifa hizi za hali mbaya ya hewa hutolewa kwa jamii pale tu zinapokuwa zimekidhi viwango na miongozo ya utendaji kazi.

Kwa takribani wiki sasa Mamlaka imekuwa ikifuatilia mwenendo wa kimbunga “Freddy” kilichopo Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi karibu na Pwani ya Madagascar na kujiridhisha kutokuwa na madhara ya moja kwa moja kwa sasa kwa maeneo yaliyoko nchini kwetu.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, inaendelea kufuatilia kwa kina mwenendo wa kimbunga hiki na itatoa taarifa punde tu kutakapokuwa na haja ya kufanya hivyo.

Aidha, mamlaka inapenda kuikumbusha jamii na umma kwa ujumla kuwa kwa mujibu wa sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na. 2 ya 2019, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ndiyo pekee yenye mamlaka ya kutoa taarifa za tahadhari za matukio ya hali mbaya ya hewa na ni kosa kisheria mtu mwingine kufanya hivyo.

Kwa taarifa hii wananchi wanashauriwa kuendelea kuzingatia taarifa na tahadhari za hali mbaya ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania sambamba na kutafuta, kupata na kufuata ushauri wa wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazotokana na hali mbaya ya hewa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news