Manusura ‘wakiomba miujiza’ huku Uturuki ikiongeza juhudi za uokoaji

ANKARA-Waturuki wanaomba miujiza huku zoezi la uokoaji likiendelea kuwatafuta manusura wa tetemeko kubwa la ardhi lililoharibu maeneo ya Kusini mwa nchi.
Mesut Hanser akiwa amemshika mkono binti yake Irmak mwenye umri wa miaka 15, ambaye alifariki katika tetemeko la ardhi huko Kahramanmaras. (Picha na AFP).

Mvua kubwa na theluji vinatatiza juhudi za kuokoa maelfu ya watu waliokwama chini ya vifusi huku idadi ya vifo ikiendelea kuongezeka.

Zaidi ya watu 5,000 wamefariki na 15,000 kujeruhiwa huko Uturuki na nchi jirani ya Syria wakati tetemeko kubwa la ardhi ambalo linakadiriwa kuwa na vipimo vya Richter 7.8 kupiga huku likifuatiwa na mfululizo wa mitetemeko iliyofuata mapema Jumatatu.

Kutokana na hali hiyo,Rais wa Uturuki, Mheshimiwa Recep Tayyip Erdogan ametangaza hali ya hatari kwa muda wa miezi mitatu katika maeneo yaliyoathiriwa na tetemeko la ardhi ambalo ni baya zaidi kuwahi kutokea nchini humo kwa miaka 80.

Idadi ya waliofariki katika maafa hayo nchini Uturuki inafikia 3,500, huku zaidi ya 22,000 wakijeruhiwa na majengo 6,000 kuharibiwa. Zaidi ya watu 8,000 walionusurika wamechukuliwa kutoka kwenye magofu ya majengo yaliyoporomoka.

Mamlaka zinaonya kwamba, idadi ya waliofariki itaendelea kuongezeka.Aidha, Serikali ya Uturuki imetangaza wiki moja ya maombolezo ya kitaifa na kutenga dola bilioni 5.3 za msaada wa dharura, huku Shirika la Ndege la Uturuki likiwa limebeba wafanyakazi wa kujitolea zaidi ya 11,000 kwenye eneo la tetemeko hilo.

Makumi kwa maelfu ya wafanyakazi wa misaada na wafanyakazi wa dharura wametumwa katika eneo lililoathiriwa kama sehemu ya misaada ya kibinadamu ya kitaifa na kimataifa, huku mataifa zaidi ya 70 yakitoa msaada.

Firat Gerger, mwanasheria katika Jimbo la Kusini-Mashariki la Sanliurfa, alimwamuru mkewe na watoto kurejea nyumbani kwao baada ya kunusurika kwenye tetemeko hilo kabla ya kurejea katikati mwa jiji kujiunga na juhudi za uokoaji.

“Nilianza kuwahamisha wageni kutoka hoteli ninayomiliki katika wilaya ya Haliliye ya Urfa. Kisha tuliona kwamba nguzo za jengo karibu na hoteli yangu zilikuwa zikipasuka. Jengo liliinama upande mmoja. Kwa haraka tulizingira jengo hilo kwa kamba na kusogeza magari yaliyokuwa karibu,”aliambia Arab News.

Gerger na timu yake walipanda kupitia dirishani kwenye ghorofa ya kwanza ya jengo ili kuokoa wanyama waliokwama ndani.

Hata hivyo, majaribio yao ya kutaka familia ya wakimbizi kuondoka katika jengo lao la ghorofa ya tatu yaliishia kuwa msiba wakati jengo hilo lilipoporomoka muda mfupi baadaye.

"Tulirushia jiwe kwenye dirisha lao ili kuvutia umakini wao," alisema. "Jengo la zamani liliporomoka kwa sekunde chini, ilionekana kama sinema ya kutisha,"alisema.

Wakimbizi walikuwa watu pekee waliosalia katika jengo hilo baada ya wito wa kuhamishwa. Miili ya watu watano wa familia hiyo ilipatikana kufuatia shughuli ya uokoaji.Mamilioni ya wakimbizi wa Syria waliokimbia vita nchini mwao sasa wanaishi katika eneo hilo.

Watu wa eneo hilo wanasema kuwa, majengo mengi hayakujengwa kwa viwango vinavyohitajika ili kustahimili matetemeko ya ardhi, na hayajawahi kukaguliwa ipasavyo.

Majengo mapya, hata yale yaliyojengwa miezi michache iliyopita, yaliporomoka katika tetemeko hilo. Serdar Ozsoy, mwandishi wa habari aliyefika katika mji wa bandari wa Iskenderun jana, alikuwa katika wilaya iliyoathirika sana ya Kirikhan katika jimbo la Hatay baada ya tetemeko hilo kutokea.

"Ni moja ya kanda zilizoathiriwa zaidi. Uharibifu huo umeenea sana, timu za uokoaji haziwezi kupangwa ipasavyo. Leo msaada wa kibinadamu unaonekana bora zaidi kuliko jana. Niliona mahema mengi sana yakiwasili kwa ajili ya walionusurika. Lakini mvua inaendelea kunyesha na kutatiza juhudi za uokoaji,” alisema.

"Siku ya kwanza ilikuwa muhimu kupata manusura chini ya majengo yaliyoporomoka. Lakini sasa nafasi za kuokoa watu zinapungua."

Ozsoy alisema kuwa, alikuwa amezungumza na mtu aliyenusurika ambaye nyumbani kwake watu walivamia na kuiba alipokuwa makaburini akimzika mama yake."Wezi walipata fursa nzuri ya kuingia ndani ya nyumba yake na kuiba chochote cha thamani," alisema.

Vikosi vya uokoaji kutoka Uzbekistan vilifika wilayani Kirikhan mapema Jumanne, huku waokoaji wengine wa kimataifa, wakiwemo kutoka nchi za Umoja wa Ulaya, wakifanya kazi katika eneo lote.Red Crescent ya Uturuki pia inatoa mahema na blanketi yakiwemo mahitaji mengine..

Huko Hatay, maelfu ya watu walionusurika wamejificha kwenye magari yao huku kukiwa na hofu ya kutokea matetemeko zaidi."Kuna hitaji la dharura la pesa taslimu kwa sababu hakuna umeme na hakuna ATM ya kutoa pesa," Ozsoy alisema.

Katika miji mingine, kama vile Kusini Mashariki mwa Gaziantep, hifadhi ya vitu muhimu inapungua. Ugur Poyraz, katibu mkuu wa Chama cha IYI alisema, hakuna mkate kwa sababu usambazaji wa gesi asilia kwa jiji ulikumbwa na tetemeko hilo.

"Baadhi ya watu wa eneo hilo wanajaribu kusambaza supu kwa manusura na vifaa vyao," alisema. Huko Hatay, mchezaji wa soka wa Ghana, Christian Atsu, ambaye alicheza mechi 107 katika klabu ya Newcastle inayoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza na sasa anachezea klabu ya Uturuki ya Hatayspor, aliokolewa kutoka katika jengo lililoporomoka.

Barabara zilizoharibika, moto uliozuka katika bandari ya Iskenderun na njia ya ndege iliyofungwa kwenye uwanja wa ndege umefanya njia ya kufikia jimbo la Hatay kuwa ngumu zaidi.

Duygu Duman aliiambia Arab News kwamba, jamaa zake waliweza kusikia sauti chini ya vifusi vya jengo lililoporomoka katikati mwa Hatay, ambapo bibi na shangazi yake walikuwa wamenaswa.

"Bibi yangu ni mzee sana, hawezi kusubiri kwa muda mrefu," Duman alisema. Mtu mwingine aliyenusurika, Ismail Keser, alimuokoa shemeji yake kutoka kwenye magofu ya jengo la ghorofa tano huko Antakya.

"Hatuwezi kuingia ndani ya nyumba kwa sababu ya mitetemeko ya baadaye," alisema. "Bado ninashiriki katika juhudi za uokoaji, lakini tunaishiwa na matumaini. Kuna fujo hapa,”aliambia Arab News. (DIRAMAKINI/Arab News)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news