Rais Dkt.Mwinyi aahidi ushirikiano zaidi kwa ofisi ya haki za binadamu

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameahidi kushirikiana na ofisi ya haki za binadamu katika kuendeleza ushirikiano wao.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiagana na Mwakilishi na Mkurugenzi wa Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu katika Kanda ya Afrika Mashariki na Umoja wa Afrika, Bw.Marcel Akpovo, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika Februari 10, 2023 katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar. (Picha na Ikulu).

Amesema, Zanzibar inafurahia ushirikiano uliopo baina yao na kuendeleza masuala mbalimbali ya sheria na haki za binadamu ili kujenga uelewa mpana kwa jamii.

Dkt.Mwinyi ameyasema hayo Ikulu jijini Zanzibar alipozungumza na Mwakilishi na Mkurugenzi wa Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu Kanda ya Afrika Mashariki na Umoja wa Afrika, Bw.Marcel Akpovo aliyemtembelea.

Amesema Zanzibar, kama sehemu ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ina maeneo mengi inayofanya kazi na kutelekeza haki za binadamu ikiwemo, mahakama, ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Jeshi la Polisi na taasisi nyingine za sheria.

Pia amesema, ushirikiano baina Serikali na ofisi hiyo ya kimataifa unasadifu azima ya taasisi za sheria zilizopo nchini.

Aidha, Rais Dkt.Mwinyi ameiomba taasisi hiyo kuangalia uwezekano wa kuzisaidia taasisi za Serikali zinazofanya kazi na kutekeleza masuala ya sheria kwa kuwajengea uwezo kwenye maeneo wanayoyatumikia ikiwemo mafunzo ya muda mfupi na mrefu, warsha na masuala yatakayowajengea ufanisi na kuwaongezea weledi kwenye majukumu yao ya kila siku.

Ameeleza Zanzibar inafanya kazi chini ya mwamvuli wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania licha ya baadhi ya taasisi hizo za sheria kila moja ikijitegemea kwa mujibu wa maumbile ya upande inakotokea, lakini pande zote mbili za Muungano zinashirikiana moja kwa moja kufanikisha wajibu wao wa kuwatumikia Watanzania wote.

Hata hivyo, Dkt.Mwinyi ametumia fursa hiyo kumtaka mwakilishi huyo kuitumia vyema Zanzibar sio kwa utalii pekee bali kuichagua hata kwa mikutano na makongamano yao ya kimataifa kwani Zanzibar ina kumbi kubwa za mikutano ya kimataifa na vitutio vizuri kwa wageni.

Kwa upande wake, Marcel Akpovo amemuambia Rais Dkt.Mwinyi kwamba ofisi yao inaunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuwatumikia watu wake na kuwaletea maendeleo makubwa.

Amesema, ofisi yao pia ina imani kubwa na Serikali na kwamba ushirikiano wao utaleta mafanikio zaidi kwa watu wa pande zote anazoziwakilisha na kuongeza kuwa, ujio wake kwa Zanzibar mbali na kuonana na Serikali ya Awamu ya Nane, lakini kuimarisha ushirikiano wao.

Marcel ambaye ni raia wa Benin huko Afrika Magharibi, alimuahidi Dkt.Mwinyi kwamba taasisi yao watafanya kazi bega kwa bega katika kuiunga mkono Serikali pamoja na kushirikiana kwenye masuala ya sheria na taasisi za sheria zilizopo nchini.

Alieleza taasisi yake itashirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kutoa mafunzo kwa Makahimu, Majaji, Mawakili, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka na taasisi za sheria zilizopo Zanzibar.

Alisema, moja ya majukumu ya ofisi yao ni kuitangaza na kuunga mkono kampeni ya kimataifa ya “Haki za wanawake na masuala ya jinsia” kwa kutekeleza wajibu wa haki za kila mtu kwenye jamii na kuendelea kuhamasisha.

Alisema, Tanzania ni nchi ambayo wameendeleza zaidi urafiki na kueleza kwamba wanaufurahia uhusiano mzuri uliopo baina ya taasisi yao na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ambao aliusifu ni Muungano wenye baraka na kuimarisha amani, upendo na mafanikio makubwa ya watu wa pande mbili hizo.

“Uhusiano wetu tulionao unaakisi maumbile halisi ya Muungano wa watu wa pande mbili za taifa hili la Tanzania,” alisifu mgeni huyo.

Alisema, lengo la ujio wao kwa Zaznzibar ni kuona kwa kiasi gani wataunga moko kwenye masuala ya upatikanaji wa haki kwa Zanzibar na maeneo yanayohusiana na hayo.

Bw. Marcel Akpovo anatekeleza wajibu wake kwa mataifa ya Djibuti, Erictria, Ethiopia, Kenya, Sudan, Somalia, Sudan Kusini,Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Uganda.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news