Rais Dkt.Mwinyi atoa maagizo kwa wadau wa utalii

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewataka wadau kwenye sekta ya utalii kuboresha huduma ziendane na mazingira ya wakati uliopo ili kukidhi haja na mahitaji ya wageni wanaoitembelea Tanzania.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akihutubia na kuufungua Mkutano Mkuu wa Kimataifa wa Wadau mbalimbali katika Sekta ya Utalii “The Z Summit” , uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Kiembesamaki, Wilaya ya Magharibi “B” Unguja jijini Zanzibar leo Februari 23,2023. (Picha na Ikulu).

Dkt. Mwinyi alieleza hayo alipofungua Mkutano wa Kimataifa wa Biashara na Utalii “The Z- Summit” katika Ukumbi wa Golden Tulip, Uwanja wa Ndege Wilaya ya Mjini.

Amesema, sekta ya utalii Zanzibar ambayo inajumuisha vivutio vingi ni sekta muhimu inayochangia asilimia 30 ya pato la taifa.

Dkt.Mwinyi amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanazibar imechukua jitihada mbalimbali kuimarisha sekta hiyo yenye lengo la kuongeza watalii kufikia 850, 000 ifikapo mwaka 2025 ambapo tayari imeimarisha miundombinu ikiwepo kutanua barabara za kisasa, kuboresha uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume ambapo alieleza kwa sasa unatoa huduma za kimataifa zenye kukidhi haja ya mahitaji ya wageni chini ya uongozi wa Taasisi ya Kimataifa ya DNATA inayotoa huduma za kimataifa za viwanja vya ndege.
Amesema, ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Pemba unaotarajiwa kuifungua Pemba kiutalii ni miongoni mwa juhudi za serikali kwenye kukuza sekta ya utalii nchini.

Amesema, Zanzibar ni kituo cha wageni wengi kutoka mataifa mbalimbali duniani,kama kilivyopambwa na magofu yaliyohifadhi historia pamoja na mji mkongwe uliopo kwenye hifadhi ya UNESCO hivyo inawavutia wageni wengi kupitia fukwe angafu, ubuluu wa bahari pamoja na ukijani wa visiwa vyake vilinavyopambwa na michezo ya baharini

Alieleza milango ya serikali ipo wazi kuwakaribisha wawekezaji kuwekeza kwenye michezo ya baharini ikiwemo michezo ya fukwe.
Akizungumzia Sera ya Uchumi wa Buluu na Utalii, Rais Dkt.Mwinyi alieleza Serikali imechukua jitihada kubwa kuitekeleza sera hiyo kwa vitendo ikiwa ni pamoja na kutilia mkazo suala la endelevu kupitia sera yake ya Utalii kwa Wote.

Ameahidi kuwa serikali itaendelea kuwawekea mazingira mazuri wadau wote wa utalii na kuwaomba mkutano huo uwe chachu ya kutoa firsa nyingi kwa watalii na wadau wake.

Hivyo amesema ni imani kwamba mkusanyiko huo ulioshirikisha wadau mbalimbali wa sekta utatoa mafanikio mazuri katika kuikuza sekta nchini.

“Sote kwa pamoja tuungane kubadilishana uzoefu, kufanya kazi pamoja tutachangia kuikuza sekta ya utalii Tanzania,"amesema.

Akizungumzia suala la kutunza mazingira endelevu, Rais Dkt.Mwinyi amesema utalii ni chachu ya uchafuzi wa mazingira, hivyo aliitaka jamii, wadau wa utalii pamoja na wawekezaji kwenye sekta hiyo, kutunza mazingira na viumbe vya bahari, kuepuka ujaribifu wa ikolojia, uharibifu wa ardhi, uchafuzi wa hewa na maji kwa kuweka mazingira na utalii endelevu.
Mapema Waziri wa Utalii na Maliasili wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Muhamed Omary Mchengerwa alieleza hali ya utalii ilivyo duniani, huku akisema Tanzania ina kazi kubwa ya kuitangaza nchi kimataifa kupitia sekta ya utalii.

Amesema kwa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wana lengo la kuongeza watalii wengi kutoka mataifa makubwa duniani ikiwemo Bara la Ulaya, Asia, Mashariki ya Mbali na Amerika.

Aidha, alieleza serikali pia zina nia ya kuliteka soko la utalii kutoka China ambao wanaongoza Dunia kutoa watalii wengi hadi kufikia milioni moja na nusu.

Naye Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Simai Muhammed Said alisema wakati umefika kwa Zanzibar kubadili mtazamo kupitia misimu ya utalii kuondokana na dhana msimu mdogo na mkubwa badala yake wawe tayari kuutangaza utalii misimu yote iwanufaishe wao na taifa kwa ujumla.

Mwenyekiti wa ZATI ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamisheni ya Utalii, Rahim Baloo alisema mkutano huo umelenga kuitambulisha Dunia na kuitangaza Zanzibar kiutalii na kiutamaduni pamoja na kuwakaribisha wawekezaji zaidi.

Aidha, aliipongeza Serikali Awamu na Nane na wizara kwa ujumla kwa kuziunga mkono sekta binafsi kwa mchango mkubwa wanaoutoa kwa uchumi wa Zanzibar.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news