Rais Dkt.Mwinyi atoa maelekezo kwa mahakama kuu nchini

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amezitaka Mahakama Kuu ya Tanzania na Zanzibar kutengeneza mfumo endelevu wa kuboresha mageuzi ya kiutendaji yaliyofanyika kwa lengo la kudumisha juhudi za mahakama hizo kuwa endelevu katika kuwatumikia watu.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe.Prof.Ibrahim Juma (kulia kwa Rais) na Ujumbe wake walipofika Ikulu jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Ikulu leo Februari 11,2023 na (kushoto kwa Rais) ni Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdallah.(Picha na Ikulu).

Dkt.Mwinyi ameyasema hayo leo Ikulu jijini Zanzibar alipozungumza na Majaji na watendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mahakama Kuu ya Zanzibar.

Amesifu ushirikiano wa kiutendaji uliopo baina ya Mahakama hizo baada ya mabadiliko makubwa waliyoyafanya baina yao ambayo alieleza yameongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu yao, pia alizishauri taasisi mbili hizo za sheria kuendeleza ushirikiano wao katika kufanikisha malengo yao.

“Nataka niseme, kama kuna sekta katika Muungano wetu zenye ushirikiano wa karibu ni Mahakama kuliko sekta nyingine na nawashukuru Mahakama Kuu Zanzibar kwa kulichukulia hilo kwa uzito wake, wamenitaarifu kwamba wako kwenye mabadiliko makubwa ya kubadili ufanisi wa utendaji wao,”ameeleza Rais Dkt.Mwinyi.

Amemuagiza Jaji Mkuu wa Mahakama Kuu ya Zanzibar kufuata mfumo wa Mahakama Kuu ya Tanzaia kwa sehemu kubwa ya mabadiliko iliyoyafanya kwenye utendaji wao ili na Zanzibar ipige hatua kubwa kiutendaji kama walivyofanikiwa Tanzania Bara.

Amesema, Zanzibar ina mengi ya kujifunza kwa Mahakama Kuu ya Tanzania, hivyo aliwataka watendaji wa Mahakama kuu Zanzibar kujitahidi kuisarifu teknolojia ili kuendana sambamba na mifumo yakisasa iliyopo katika kuwawepesishia kazi zao ili wananchi wapate huduma kwa haraka zaidi kwa lengo la kurejesha imani zao kwa mahakama.

Akizungumzia thamani ya mahakama kwenye ukuaji uchumi wa nchi, Dkt.Mwinyi ameeleza ukuaji uchumi unategemeana na mihimili yote ya Serikali kufanya kazi kwa ushirikiano na alieleza mabadiko makubwa ya kiufanisi yaliyofanywa kwenye mahakama hizo anaamini yatarejesha hadhi ya utendaji na kuitaka mihimili mingine ya Serikali kufanya mabadikilo kama walivyofanikiwa Mahakama ili kurejesha imani za wananchi.

“Ikifika sehemu wananchi wakaanza kusema hatuna imani na mahakama anajua akienda mahakamani atachukua muda mwingi kupata haki yake, au uwezo wa kulipia hadi apate haki yake hana, basi ile kukata tamaa tu inatufanya kama serikali lazima tuone jinsi gani hii mihimili inasaidia watu kurejesha imani zao,” Alisihi Rais Dkt. Mwinyi.

Rais Dkt. Mwinyi, aliishukuru Mahakama Kuu Tanzania kwa msaada wao wa kujenga kituo jumuishi Pemba na kueleza kwamba juhudi hiyo ni msaada mkubwa kwa Serikali.

“Nishukuru sana kwa utayari wenu wa kusaidia Serikali kujenga kituo hiki jumuishi Pemba, ni dhamira njema kwa nchi yenu, tunashukuru sana na hayo yaliyobaki tutayafanyia kazi sisi wenyewe,”alishukuru Rais Dkt.Mwinyi.

Naye, Jaji Mkuu wa Mahakama Kuu Tanzania, Prof. Ibrahim Juma amesema Mahakama imejipanga vizuri kuhakikisha kila mwananchi anapatiwa haki yake licha ya ukubwa wa nchi na wingi wa watu wake, mgawanyiko wa idadi ya mikoa yake, wilaya, vijiji na vitongoji kila mmoja mahakama imelenda kumfikia, hivyo alieleza lazima mahakama zijipange hukakikisha zinawafika watu wote na kila mmoja anapatiwa haki yake.

Amesema, Mahakama ya Tanzania imefanikiwa sana kutokana na maboresho yake ambayo yalianza mara tu baada ya nchi kupata uhuru wake.

Amesema maboresho zaidi ambayo Mahakama imekuwa ikiyafanyia kazi ni yale yaliyofanywa na Tume ya Jaji Bomani mwaka 1993 ambapo Mahakama imeangalia matatizo nane na imeanza kuyatekeleza kwa vitendo.

Alieleza matatizo hayo ni ucheleweshwaji wa kutatua migogoro inayofikishwa mahakamani ambayo alieleza yanaendelea kufanyikwa kazi kwa kutumia mifumo wa kisasa ya kiteknolojia.

Alieleza eneo lingine ni wananchi kuwa na fursa ya kupata haki zao kwa kwenda kwenye majengo ya mahakama kufuata taratibu za kisheria na kupata taaluma juu ya haki zao.

Aidha, kudhibiti rushwa na utovu wa maadili kwenye mahakama jambo alilolieleza bado ni vita endelevu, tatizo jingine walilojielekeza ni sheria kutokuwa na uharaka wa kutoa maamuzi kwa vile ni za zamani kwa hiyo, alieleza mahakama sasa zinafanya mabadiliko makubwa kwenye eneo hilo kwa msaada wa teknolojia, aidha, kurejesha imani ya wananchi kwenye vyombo vya sheria katika kuwapatia haki zao.

Eneo jingine wanaloliangalia alieleza ni uwezo wa majaji, mahakimu na mawakili kulingana na taaluma zao pamoja na uchache wa watoa kuduma kulingana na mahitaji ya wananchi, Jaji Ibrahim alisema pamoja na miundombinu ya majengo ya mahakama lakini zaidi kwenye kupata huduma bora.

“Sisi mahakama baada ya kuona matatizo kwenye vituo vya sheria ni makubwa sana, tumekuwa tukitegemea zaidi Wizara ya Katiba na sheria ziongoze, tumeona bora tubadili mwelekeleo, sasa sisi Mahakama ndio tuwe kiini cha maboresho hayo,” amefafanua Jaji Ibrahim.

Naye Jaji Mkuu wa Zanzibar, Khamis Ramadhan Abdalla, aliishukuru Mahakama ya Tanzania kwa ushirikiano inayoendeelea kutoka kwa Mahakama ya Kuu ya Zanzibar tokea alipoteuliwa kushika wadhifa huo. Pia aliahidi kwenda sambamba na kasi ya Mahakama ili kuleta mabadiliko makubwa Zanzibar.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel alieleza sehemu kubwa ya maboresho iliyofanya mahakama hiyo ni matumizi ya mifumo kwa majengo yote kuunganishwa na mtandao na utendaji mzima wa Mahakama, ikiwemo matumizi ya TEHAMA na teknolojia ya kisasa katika uendeshaji kesi ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya kitelektroniki na na kidijitali.

Aliongeza mifumo hiyo imeweka miundombinu yote ya mahakamama kwa kuweka kipaumbele cha matumizi ya teknolojia wakati wa kusikiliza kesi hali iliyorahisisha kesi nyingi kusikilizwa kwa wakati mfupi, matumizi ya mifumo ya simu imeleta mabadiliko makubwa.

Alieleza matumizi ya mifumo hiyo imeongaza ufanisi kwa utendaji wa mahakama ambayo imerahisisha kazi, pia alisema teknolojia imesaidia kuziunganisha mahakama zote Tanzania kwenye mfumo mmoja wa kidijitali ambao umerahisisha utendaji wao kutoka mahakama ya mwanzo hadi Mahakama Kuu.

Alisema katika kurahisisha utendaji wao mifumo imefanikiwa kuunganisha Mahakama na wadau wengine wote wa taasisi za Mahakama ili kurahisisha kazi na kuokoa muda wa kiuendashaji kwa kutumia teknolojia hiyo.

Amesema mifimo pia imezisaidia mahakama kupata taarifa nyingi zaidi wakati wa kusikiliza mashauri, kutokana na ushikiano baina ya mahakama na taasisi zake.

Hata hivyo, alieleza mifumo hiyo pia imechangia kuanzisha kituo cha kuratibu, kusimamia na kufuatilia mwenendo wa mahakama zote Tanzania kwa njia ya mtandao kwa kusaidiwa na wataaalmu wa ndani ambao hudhibiti hitilafu wakati mahakama zikiendelea jambo alilolieleza kwamba wataalamu hao wana uwezo wa kuimiliki wenyewe na kuisawazisha wakati wa hitilafu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news