Rais Dkt.Samia aomboleza ajali iliyoua watu 17 mkoani Tanga

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameeleza kusikitishwa na ajali iliyoua watu 17 mkoani Tanga.
Hayo ameyabainisha leo Februari 4,2023 kupitia taarifa fupi aliyoitoa katika kurasa zake rasmi za mitandao ya kijamii.

"Nimesikitishwa na vifo vya watu 17 vilivyosababishwa na ajali iliyotokea jana saa 4:30 usiku eneo la Magila Gereza, Wilaya ya Korogwe, Mkoa wa Tanga.

"Nawapa pole wafiwa na wote walioguswa na vifo hivi. Nawaombea ndugu zetu hawa wapumzike mahali pema na majeruhi wapone haraka,"amesisitiza Rais Dkt.Samia.
Awali katika taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Omary Mgumba imeeleza kuwa ajali hiyo imehusisha magari mawili na kusababisha vifo vya watu 17 na majeruhi 12.

"Ajali hii imesababisha vifo 17 na majeruhi 12 ambao majina yao wote hayajafahamika, miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali yetu ya Wilaya ya Korogwe na majeruhi 10 wamehamishiwa Hospitali ya Mkoa wa Tanga, Bombo na majeruhi wawili wamebaki Hospitali ya Korogwe kwa matibabu.

“Ajali hii imehusisha gari aina ya Mitsubishi Fuso na Coaster iliyokuwa imebeba mwili wa marehemu na abiria 26 ikitokea Dar kwenda Moshi kwenye mazishi,”ameeleza.

Kwa nini ajali?

Hivi karibuni VOA iliripoti kuwa,takwimu mbalimbali zinaonesha ajali nyingi za barabarani, katika ukanda wa Afrika Mashariki, zinatokana na kutofuatwa kwa sheria za barabarani,

Kwa mujibu wa taarifa hizo madereva wasio na weledi na kitendo cha kutozingatiwa masuala ya kiusalama kwa vyombo vya usafirishaji ndio vyanzo vikuu vya ajali hizo.

Karibu kila nchi ya Afrika Mashariki ina sheria nzuri za vyombo vya usafirishaji, lakini rushwa hufunika sheria.

Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) inabainisha kwamba nchi nyingi zimeboresha sheria kama vile kuzuia mwendo kasi, ulevi na matumizi ya vifaa vya usalama kama matumizi ya mikanda, kofia za bodaboda yaani Helmet na hata viti maalumu kwa watoto.

“Sababu za ajali zipo nyingi lakini kwa uchache ni ufinyu wa barabara, mwendo kasi na uzembe wenyewe wa madereva hasa ikizingatiwe wengi wao hawana elimu ya kutosha ya udereva.”

Pamoja na barabara nyingi za Afrika Mashariki kuelezwa kuwa ni nyembaba na mbovu zisizotoa mwanya wa makosa kwa madereva, WHO ilipendekeza mwendo kasi wa kutumika barani Afrika. 

Imependekeza mwendo kasi wa juu usiozidi kilometa 50 kwa saa, lakini inadaiwa nchi 47, zinazowakilisha watu milioni 950, zinaheshimu mapendekezo hayo.

Uganda ni kinara wa ajali za barabarani kwa ukanda wa Afrika Mashariki. Inadaiwa mwendo kasi uliopitiliza, barabara mbovu na ulevi ndivyo vyanzo vikuu vya ajali za barabarani kama anayoeleza Akor Amazima mchambuzi wa masuala ya kijamii nchini Uganda.

“Vyanzo vya ajali za barabarani nchini Uganda vipo vingi sana, lakini tatizo la ushirikina, barabara kuwa mbovu, barabara kuwa nyembamba sana, vilevile madereva wanaendesha bila kujali maisha ya watu, na magari mabovu, ikijumuisha usimamizi mbaya, lakini pia watembea kwa miguu nao wanachangia ajali za barabarani.”

Nchi za Afrika Mashariki zina sheria za barabarani ambazo katika maandishi huonekana nzuri, japo wadau wa usafirishaji wakisema sio kali kama ilivyo katika nchi nyingine. 

“Zipo nchi zenye sheria kali kidogo hasa kwa madereva wa mabasi, mfano niliwahi kwenda Angola, nikakuta masharti ni magumu, hata Rwanda pia ni magumu na ndio maana uzembe kwa madereva kule ni mdogo kuliko kwetu.”

Taarifa rasmi za idara za usalama barabarani za Afrika Mashariki, zinaeleza vyanzo vya ajali vinavyo shabihiana ni makosa ya kibinadamu, hasa uzembe wa madereva, kutotii sheria na kanuni za barabarani, mwendo kasi, matumizi ya vileo, ubovu wa barabara na ubovu wa vyombo vya usafiri vyenyewe.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news