Serikali ya Awamu ya Nane chini ya Rais Dkt.Mwinyi yazidi kuwafungulia vijana njia

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amewataka vijana kuzitumia fursa zilizopo na zitakazoletwa na Serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo kwa ajili ya Maendeleo na Ustawi wao na Taifa kwa ujumla.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akikabidhiwa zawadi maalum Februari 22, 2023 na Mkurugenzi Mkaazi wa USAID nchini Tanzania, Bi. Kate Somvongsiri na kushoto kwake ni Naibu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Taasisi ya T-Marc, Bw.Alex Mgongolwa, wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Mradi wa Kijana Nahodha Tanzania, uliozinduliwa viwanja vya mpira Maisara Suleiman Wilaya ya Mjini Unguja.(Picha na Ikulu).

Amesema, vijana ni nguvu kazi kwa taifa lolote duniani, ambayo inahitaji kuandaliwa vema kwa faida za baadae.

Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo huko Maisara Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi alipozungumza na vijana wa makundi tofauti kwenye uzinduzi wa mradi wa “Kijana Nahodha” unaofadhiliwa na Shirika la USAID la Marekani.

Amesema, mradi huo unaunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hasa kwenye utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya kitaifa ikiwemo dira ya 2050, mpango wa taifa wa maendeleo 2026 na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025.

Alisema, kundi kubwa la vijana duniani kote limekuwa likikabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ukosefu wa ajira, matumizi ya dawa za kulevya, mimba na ndoa za umri mdogo, UKIMWI, Afya ya Akili, ukatili na udhalilishaji wa kijinsia pamoja na matumizi mabaya ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Dkt.Mwinyi amezitaka wizara zote zinazoguswa na mradi huo kushiriki na kufuatilia kwa karibu utekelezaji wake ili kufikia malengo yaliyokusudiwa kwa kuwaandaa na kuwasimamia vijana kuhakikisha shughuli watakazozianzisha zinakua endelevu hata baada ya kukamilika mradi.

Akizungumzia mabaraza ya vijana, Dkt.Mwinyi amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inasimamia uendeshaji wa Baraza la Vijana la Zanzibar kuanzia ngazi ya Shehia hadi taifa pia alisema baraza hili ni chombo kinachowaunganisha vijana nchini ili kupaza sauti zao kwenye masuala mbalimbali yanayohusu maslahi yao pamoja na kuchochea maendeleo ya jamii.

Alieleza mabaraza hayo yamechangia kuanzishwa vituo vya mafunzo ya vijana maeneo ya Bweleo na Pangeni kwa Unguja na Weni na Mjini Ole kwa Pemba kwa kuwaandaa vijana kupata maarifa na umahiri wa kukabiliana na changamoto kwenye makuzi yao.

Akizungumzia fedha za ahueni ya Uviko isiyo na riba, Rais Dkt.Mwinyi alieleza Serikali ilitoa fedha hiyo kwa ajili ya mikopo ya kuwawezesha wananchi kiuchumi, kujenga vituo maalumu vya wajasiriamali kwa kila wilaya pamoja na kuwapatia wananchi vifaa vya uvuvi zikiwemo boti na vifaa vyengine vya uvuvi wa kisasa, vifaa kwa wakulima wa mwani kwa vijana na kinamama.

Alisema, Serikali imeongeza uwekezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ya binafsi, uimarishaji wa shughuli za uchumi wa buluu ikiwemo kuendeleza sekta ya utalii, kukuza uchumi wa nchi na kuongeza fursa za ajira ambazo vijana ni miongoni mwa walengwa wakuu.
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita aliwaomba wadau wa maendeleo kuendelea kuiungamkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwekeza zaidi kwenye miradi inayowahusisha vijana ili kuwakomboa na changamoto zinazowakabili ikiwemo ukosefu wa ajira wapate kujitegemea.

Naye Mkuu wa Mradi wa Kijana Nahodha, Dkt.Tuhuma Tuli alieleza mradi ni sekta mtambuka amabao utahusisha ajira kwenye sekta za elimu, kilimo, utawala bora na afya kwa unalengo la kuwajengea uwezo vijana wenye umri kati ya miaka 15-25.

Alisema mradi pia imelenga kuwajengea uwezo vijana, kuwasaidia upatikanaji ubora wa stadi mbalimbali ikiwemo mafunzo ya ufundi, kuboresha uelewa wa afya ya akili kupitia zana za elimu ya kidijitali zinazoongozwa na watu binafsi na kuimarisha njia za wazi za mawasiliano kati ya vijana na serikali ili kuinua sauti za vijana katika maisha ya kiraia, siasa, na utungaji sera.

USAID Kijana Nahodha ni mradi wa sekta mtambuka unaofanya kazi katika sekta ya ajira, elimu, kilimo, utawala bora na afya, na unalenga kujenga uwezo wa vijana wenye umri kati ya miaka 15-25. Kujenga uwezo huu ni pamoja na kuongeza upatikanaji na ubora wa stadi mbalimbali; mafunzo ya ufundi; kuboresha uelewa wa afya ya akili kupitia zana za elimu ya kidijitali zinazoongozwa na watu binafsi; na kuimarisha njia za wazi za mawasiliano kati ya vijana na serikali za mitaa ili kuinua sauti za vijana katika maisha ya kiraia, siasa, na utungaji sera.

Akizungumza katika hafla hii, Mkrurgenzi Mkazi wa USAID V. Kate Somvongsiri alisema, “ Kupitia Kijana Nahodha, tunalenga kuwawezesha vijana kupitia ujuzi mbalimbali; maarifa sahihi ya kuendesha biashara; msaada kutoka kwa familia zao, jamii, na serikali; ili wapate fursa kupitia elimu na ujuzi.”

Mradi wa Kijana Nahodha unatarajia kuwawezesha vijana zaidi ya 45,000 – takribani 10,000 kutoka Zanzibar na 35,000 katika mikoa miwili iliolengwa ya Bara.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news