Serikali ya Awamu ya Nane Zanzibar kuja na neema nyingine ya Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Teknolojia

NA DIRAMAKINI

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imeeleza dhamira yake ya kuanzisha chuo cha teknolojia chenye nia ya kuleta mageuzi makubwa ya mifumo itakayosaidia kwenye mabadiliko ya kiutendaji kwa taasisi za umma na binafsi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akiagana na Balozi wa India katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Binaya Srikanta Pradhan,mara baada ya mazungumzo na Ujumbe wa Taasisi ya Teknolojia ya Madrasa (Insititute of Technology IITM) ya India,ulipofika Ikulu jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu).

Chuo hicho, kinatarajiwa kujengwa Zanzibar kwa ushirikiano wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya India ikiwa ni jitihada zao za kuimarisha uhusiano wa Diplomasia baina yao.

Akizungumza Februari 14, 2023 Ikulu jijini Zanzibar na Balozi wa India nchini Tanzania, Mhe. Binaya Pradhan, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt.Hussein Ali Mwinyi alisema, Zanzibar kuanzisha Chuo Kikuu cha Teknolojia cha IIT, ni kujijengea sifa na kujitangaza kimataifa kwa fursa ya taaluma itakayotoa.
Rais Dkt.Mwinyi ameihakikishia Serikali ya India kwamba, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatoa ushirikiano wa kutosha katika kufanikisha ujenzi wa chuo hicho.

Alisema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeridhishwa na kasi ya uanzishwaji wa taasisi hiyo ambayo inatarajiwa kuanza mwezi Oktoba, mwaka huu kwa ushirikiano wa pande mbili hizo na wadau wengine wa Serikali na kueleza kuwa wanaunga mkono hatua hiyo itakayoleta mageuzi makubwa kwenye sekta ya elimu, Zanzibar.

Alieleza taasisi hiyo ya Teknolojia kwa Zanzibar ni fursa adhimu kwa vijana kuongeza utaalamu na uwezo wa kujiajiri ili kuondokana na utegemezi na kuziba mianya ya changamoto za ajira.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Balozi Pradhan alisema kuanzishwa kwa chuo hicho nje ya India ni mafanikio makubwa kwa Zanzibar kwani ni mfano pekee kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Afrika kwa jumla.

Balozi Pradha, alieleza kuna mataifa nane kutoka Afrika ambayo awali waliwania nafasi ya kujengewa chuo hicho na Serikali ya India, lakini bahati imekwenda kwa Tanzania kutokana ushirikiano mzuri wa kidiplomasia uliopo baina yao.

Alisema, Chuo Kikuu cha Teknolojia cha IIT kitakachojengwa Zanzibar kitaunganishwa kitaaluma na taasisi ya Teknolojia ya India ya “India Institute of Technology (IIT)” ambayo ina hadhi ya juu kabisa sawa na taasisi ya teknolojia ya Marekani ya “Massachusetts Institute of Technology (MIT).

Alisema nchi ya Tanzania inaongoza kwa kupata msaada wa nafasi nyingi za udhamini wa masomo nchini India kuliko nchi nyinyine yoyote barani Afrika kutokana na ushirikiano mzuri uliopo baina ya mataifa mawili hayo.
Chuo Kikuu cha Teknolojia cha IIT kinachotarajiwa kujengwa Zanzibar hivi karibuni, kinatarajiwa kufundisha fani nyingine ambapo wanafunzi kutoka mataifa mbalimbali wataruhusiwa kujiunga na chuo hicho.

Uhusiano wa diplomasia baina ya Tanzania na India ni wa kihistoria ambapo India ilifungua Ubalozi wake Dar es Salaam mwezi Novemba mwaka 1962 na mwaka 1974 ikafungua ubalozi mdogo Zanzibar.

Uhusiano baina mataifa mawili hayo umeendelea kuimarika kwa fursa nyingi za maendeleo kupatikana kwa pande mbili hizo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news