Serikali yatoa maagizo kwa taasisi za umma

NA JAMES MWANAMYOTO

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amezielekeza taasisi zote za umma nchini kutumia mifumo shirikishi ya TEHAMA iliyoandaliwa na Serikali kupitia Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) badala ya kutumia mifumo yao ambayo inajitegemea kiutendaji.
Washiriki wa kikao kazi cha tatu cha serikali mtandao wakisikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista (hayupo pichani) wakati akifunga kikao kazi hicho jijini Arusha kilichoandaliwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA).

Mhe. Jenista ametoa maelekezo hayo jijini Arusha wakati akifunga Kikao kazi cha tatu cha serikali mtandao kilichowashirikisha wadau zaidi ya 1500 wa serikali mtandao nchini.Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na washiriki wa kikao kazi cha tatu cha serikali mtandao wakati akifunga kikao kazi hicho jijini Arusha kilichoandaliwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA).

“Tumekubaliana mifumo yote ya TEHAMA iliyojengwa na itakayojengwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao ni lazima iwe endelevu ili iwe na tija kiutendaji hivyo taasisi zote za umma hazina budi kutumia mifumo hiyo shirikishi ya TEHAMA,” Mhe. Jenista amesisitiza.
Mkurugenzi wa TEHAMA Serikalini Bw. Priscus Kiwango akieleza maazimio ya washiriki wa kikao kazi cha tatu cha serikali mtandao kabla ya kikao kazi hicho kufungwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama jijini Arusha.

Mhe. Jenista ameongeza kuwa ni lazima kwa kila taasisi ya umma kuhakikisha sheria na miongozo ya serikali mtandao inazingatiwa wakati wa kusanifu mifumo ya TEHAMA, ikiwa ni pamoja na kuomba kibali Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) ili kupata idhini ya kutengeneza mifumo.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Xavier Daudi akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kufunga kikao kazi cha tatu cha serikali mtandao jijini Arusha.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi amesema ofisi yake imejipanga kuhakikisha eGA inasimamia vema matumizi ya TEHAMA katika taasisi za umma na inajenga mifumo jumuishi inayowasiliana ili kurahisisha utendaji kazi katika utumishi wa Umma ikiwa ni pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji wa Serikali.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) Mhandisi Benedict Ndomba akieleza lengo la kikao kazi cha tatu cha serikali mtandao kabla ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kukifunga kikao hicho jijini Arusha.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) Mhandisi Benedict Ndomba amesema kuwa, washiriki wa kikao kazi hicho wametoa maoni na mapendekezo ya namna ya kuimarisha serikali mtandao na kushauri uboreshaji wa baadhi ya mifumo inayotoa huduma kwa umma pamoja ili kupanua wigo wa utoaji wa huduma mtandao, hivyo mamlaka yake itahakikisha inayafanyia ushauri, maoni na mapendekezo yaliyotolewa kwa lengo la kuboresha matumizi ya serikali mtandao nchini.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Serikali Mtandao, Dkt. Jasmine Tiisekwa akitoa neno la shukrani kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama mara baada ya waziri huyo kufunga kikao kazi cha tatu cha serikali mtandao jijini Arusha kilichoandaliwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA).

Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Serikali Mtandao, Dkt. Jasmine Tiisekwa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa agizo lake la kuimarisha Serikali Mtandao nchini ikiwa ni pamoja na utashi wake wa kisiasa wa kuijenga Tanzania kuwa ya kidijitali.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwa katika picha ya pamoja na kamati ya maandalizi ya Kikao kazi cha tatu cha serikali mtandao (waliosimama) na viongozi mara baada ya kukifunga rasmi kikao kazi hicho jijini Arusha.

Kaulimbiu ya kikao kazi hicho cha tatu cha Serikali Mtandao ni ‘Mifumo Jumuishi ya TEHAMA kwa Utoaji Bora wa Huduma za Umma’.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news