Yaliyowakuta Simba, Yanga SC yawaacha hoi mashabiki

NA GODFREY NNKO

BAADA ya Klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam kumaliza mchezo wao wa kwanza wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Horoya uliopigwa Uwanja wa Jenerali Lansana Conte nchini Guinea kwa kupoteza, watani zao Yanga SC ya jijini Dar es Salaam wamechapwa na US Monastir ya nchini Tunisia pia.

Kwa Simba SC walikuwa na nafuu ya kufungwa bao moja kwa sufuri huku Yanga SC wakizidishiwa bao moja, hivyo kuondoka wakiwa wameinamisha vichwa chini kwa kuchapwa mabao mawili kwa sifuri.

Yanga kwenye mchezo huo wa hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho barani Afrika wamemenyana leo Februari 12, 2023 na US Monastir katika dimba la Olympic Rades.

Wanajangwani hao wameonekana wakishindwa kumiliki mpira kwa muda mrefu, hivyo kuwapa nafasi US Monastir kucheza mpira kwa uhuru na kuweza kupata mabao mawili ya haraka katika kipindi cha kwanza cha mchezo.

Aidha, Yanga SC ilirudi kipindi cha pili kutafuta mabao bila mafanikio licha ya kuwapumzisha baadhi ya wacheaji na kuingiza igizo jipya.

Mabao ya US Monastir yamefungwa na nyota wao Mohamed Saghraoui dakika ya 10 ya mchezo na bao la pili likifungwa na Boubacar Traore dakika ya 16 na kufanya matokeo kuwa 2-0.

Februari 11, 2023 wenyeji Horoya dhidi ya Simba SC walipata bao dakika ya 18 kupitia kwa Pape Ndiaye kwa kichwa akimalizia mpira wa kona uliopigwa na Mohamed Wonkoye.

Baada ya bao hilo, Simba SC hawakupaniki bali walicheza kwa kutulia na kupiga pasi ndefu na mipira ya juu huku kasi yao ikiwa ya kawaida kipindi cha kwanza.

Mlinda mlango Aishi Manula alicheza mkwaju wa penati dakika ya 72 uliopigwa na Ndiaye baada ya mlinzi Joash Onyango kuunawa mpira ndani ya 18.

Dakika ya 79 nahodha John Bocco almanusura awapatie Simba SC bao la kusawazisha kufuatia mpira wake kutoka nje kidogo ya lango la Horoya baada ya kupokea pasi ya Kibu Denis.

Mchezo wa Simba SC unaofuata utakuwa Februari 18, 2023 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa dhidi ya Raja Casablanca ya Morocco.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news