Simba SC yagonga mwamba kwa Azam FC

NA DIRAMAKINI

SIMBA SC ya jijini Dar es Salaam imetoka sare ya bao 1-1 na Azam FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.

Ni kupitia mtanage uliopigwa jioni ya Februari 21, 2023 katika Dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Mshambuliaji hatari wa Azam FC, Prince Dube alifunga bao ambalo huenda ndilo la kasi zaidi msimu huu ndani ya sekunde 16 tu baada ya mchezo huo kuanza.

Hata hivyo, wenyeji walisimama kidete hadi dakika ya 90 ilipomalizika kwa bao la kujifunga la beki wa Azam, Abdallah Kheri ambalo lilitinga nyavuni kwake.

Kheri alikuwa akijaribu kuuwahi mpira wa hatari uliowekwa kwenye eneo la hatari na mchezaji wa akiba, Kibu Denis ambaye kuingia kwake kuliwapa nguvu Simba SC.

Kwa matokeo hayo, Simba sasa imefikisha alama 54 baada ya kucheza mechi 23 na kuwa nyuma kwa alama tano kwaYoung Africans.

Kwa upande wa Azam FC, wamerejea nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi wakiwa na alama 44 sawa na Singida Big Stars.

Wakati huo huo, ligi hiyo inaendelea Jumatano kwa mechi moja huku KMC wakiwakaribisha mabingwa watetezi Yanga SC kwenye Dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Katika hatua nyingine, Kocha Mkuu wa Simba Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amewapongeza wachezaji wake kwa kupambana kutafuta alama tatu ingawa hawakufanikiwa.

Robertinho amesema, wamecheza vizuri, lakini bao la mapema kipindi cha kwanza liliwafanya kutoka kwenye mfumo uliowafanya kupoteza nafasi.

Kocha huyo amesema kipindi cha pili alibadili mfumo wa kuwaingiza washambuliaji watatu wenye kasi ili kuwafungua Azam ambao mara nyingi walikuwa nyuma mpaka wakafanikiwa kusawazisha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news