Viongozi ni miongoni mwa waliokamatwa kwa tuhuma za kulima bangi

NA DIRAMAKINI

VIONGOZI wa kisiasa katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita ni miongoni mwa watu tisa ambao wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kulima bangi katika eneo la msitu wa Hifadhi ya Mienze iliyopo Kijiji cha Wavu Kata ya Shabaka ndani ya halmashauri hiyo.

Ukamataji huo umetokana na operesheni inayofanywa na ofisi ya Mkuu wa wilaya hiyo,Mheshimiwa Grace Kingalame, Jeshi la Polisi na Idara ya Misitu ambapo tayari mashamba yenye hekari zaidi ya sita yaliyolimwa bangi yameteketezwa.

Akizungumza wakati wa uteketezwaji wa dawa hizo, DC Kingalame amesema, hayupo tayari kuona baadhi ya watu wakifanya biashara ya kulima bangi wilayani humo na kuwataka wenye tabia hiyo kuacha mara moja.

Mheshimiwa Kingalame amesema, wanaofanya biashara ya kulima bangi watafute pa kwenda, kwani yeye kama mkuu wa wilaya hayupo tayari kuona jamii ya Nyang’hwale inakuwa kwenye hali hatarishi kwa sababu ya dawa za kulevya badala yake wafanye kazi halali za maendeleo.

Amesema, ametumwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia kuhakikisha maendeleo yanasonga mbele wilayani humo na si uhalifu.

Pia amewataka watendaji wa vijiji kuhakikisha maeneo yao yanakuwa salama na kuwataka kutoa taarifa mapema pindi wanaopoona viashiria vyovyote vya uhalifu.

Asafu Manya ambaye ni afisa misitu wilyani humo amesema, taarifa za uwepo wa mashamba katikati ya msitu huo zimetolewa na wasamaria wema na kuitaka jamii kuacha kuingia maeneo ya misitu na kufanya uharibifu wa mazingira.

Kwa upande wake Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Nyang’hwale, Daniel Nyange amewataka wananchi kuachana na kilimo cha bangi na badala yake wajikite kwenye shughuli nyingine za kuwapatia kipato ikiwemo uchimbaji wa madini, kilimo cha mpunga na biashara nyingine halali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news