WANANCHI WALIOMBA BUNGE KUPITISHA BIMA YA AFYA KWA WOTE

NA MWANDISHI WETU

WANANCHI wamepaza sauti na kuliomba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote kwa kuwa ndio suluhisho la upatikanaji wa huduma za matibabu.
Rai hiyo wameitoa kwa nyakati tofauti wakizungumzia juu ya Muswada huo ambapo wameweka wazi kuwa, wapo tayari kuunga mkono suala hilo na litakapoanza utekelezaji wake watajiunga ili kuwa na uhakika wa huduma za matibabu popote na wakati wowote.

Mzee Alphonce Mpayo ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Maya Maya mkoani Dodoma amesema kuwa Muswada huo una umuhimu mkubwa sana katika maisha ya Watanzania hasa katika kulinda afya zao tofauti na ilivyo sasa ambapo wananchi wanashindwa kumudu gharama za matibabu.

“Jambo hili tunalisubiri kwa hamu, Wabunge wetu walipitishe ili lianze kutumika, tunapokuwa na uhakika wa matibabu tunakuwa na amani na tunaweza hata kupanga mipango yetu ya maendeleo kwa ngazi ya Kaya,” alisema.

Alitumia mwanya huo pia kumpongeza Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwa kulipa kipaumbele suala hilo na kuwa mstari wa mbele katika uhamasishaji wananchi katika kujiunga na bima ya afya.

Kwa upande wa viongozi, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bi. Rosemary Senyamule amesema kuwa, jambo la huduma za matibabu ni jambo nyeti kwa maendeleo ya nchi hivyo amepongeza kazi inayoendelea kufanywa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa kuendelea kutoa elimu juu ya umuhimu wa Bima ya Afya kwa wote kwa wananchi hatua inayowezesha kuwa na maandalizi ya kutosha wakati utekelezaji wake utapoanza.

Mwananchi mwingine Mkazi wa Mtaa wa Majengo, Dodoma Bw. Lameck Nzigiwa ameipongeza Serikali kwa hatua iliyofikiwa kwa sasa ambayo ni hatua za mwisho.

“Tunawaomba sana Waheshimiwa Wabunge wapitishe huu muswada ambao ni mkombozi sana kwa wananchi kwani jambo la muhimu kwa kila mtu ni afya yake na sheria hii ikipita kila mmoja atalazimika kuwa na bima ya afya hivyo anapougua anakuwa na uhakika zaidi wa kupata huduma popote pale anapokuwa,” alisema Bw. Nzigiwa.

Naye Bi. Magdalena Mwango ambaye ni Mjasiliamali, amesema kuwa kupitishwa kwa sheria hiyo kutapunguza umasikini mkubwa ambao wananchi wanaupata kwa sasa kutokana na kugharamia huduma za matibabu ambazo zimekuwa zikiongezeka kila kukicha.

“Nimeshuhudia familia ninazozifahamu kabisa zikiingia kwenye umasikini mkubwa na zingine kutengana baada ya maradhi kuingia katika familia hizo, hivyo sheria hii ni mkombozi kwetu na wala hatupaswi kupinga bali tuunge mkono jitihada hizi zinazofanywa na Serikali yetu,” alisema Bi. Mwango.

Wananchi wengine wameiomba Serikali kupitia Wizara ya Afya na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuendelea kutoa elimu kwa wananchi wote ili kila mmoja awe na uelewa mkubwa wa umuhimu wa kuwa ndani ya mfumo wa bima ya afya.

Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya unatarajiwa kusomwa kwa mara ya pili na ya tatu mapema Februali 9, 2023 na endapo Bunge likiridhia utekelezaji wake utaanza mwezi Julai 2023.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news