Watumishi wa TRA wadakwa kwa hujuma

NA DIRAMAKINI

JESHI la Polisi Mkoa wa Iringa linawashikilia wafanyakazi wawili wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani humo akiwemo Upendo Msigwa (32) mkazi wa Mawelewele na Chali Chaliga (28) mkazi wa Donbosco mjini Iringa kwa tuhuma za kushirikiana na watuhumiwa wengine watatu kutoa leseni za udereva kinyume na sheria na taratibu za nchi.

Watuhumiwa hao watatu ambao ni wafanyabiashara wanaoishi katika maeneo tofauti mjini Iringa ni pamoja na Omary kibao (38) mkazi wa Kitwiru, Johnson Kihongosi (31) mkazi wa Zizi la Ng’ombe na Dikson Nelson (32) mkazi wa Feelimo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, ACP Allan Bukumbi amesema, watuhumiwa hao walikamatwa baada ya Jeshi la Polisi kupokea taarifa za uhalifu huo kutoka kwa wasamaria wema.

“Tarehe 16 mwezi huu wa pili majira ya saa 3.00 asubuhi tulipokea taarifa kwamba katika mtaa wa Mahiwa mkabala na ofisi ya TRA Mkoa kuna wafanyabiashara wa duka la vifaa vya maofisini wanashirikiana na maafisa wa TRA kutoa leseni za udereva kinyume cha sheria,”amesema.

Baada ya kupokea taarifa hiyo alisema waliunda timu ya upelelezi na kufanikiwa kumnasa Kihongosi, Kibao na Nelson ambao baada ya kufanyiwa upekuzi walikutwa na leseni za udereva 31, vitambulisho vya Nida na mpiga kura vinne, nakala za kadi za magari ya watu mbalimbali na Police loss reports.

Kamanda Bukumbi alisema, watuhumiwa hao walikuwatwa pia na namba za magari na Pikipiki 431,TIN namba nane, printer tano, laptop moja, kompyuta ya mezani moja, nakala za vyeti vya mafunzo ya udereva viwili, scanner moja na lamination mashine moja.

Alisema baada ya watuhumiwa hao kuhojiwa na kukiri kufanya uhalifu huo waliwataja maafisa hao wawili wa TRA kwamba ndio wamekuwa wakishirikiana nao kujipatia fedha kinyume cha sheria na kuipotezea serikali mapato yake halali.

Wakati wakiendelea na uchunguzi wa tukio hilo, wakati wakijipanga kuwafikisha watuhumiwa hao mahakamani alisema, watawatafuta watu wote ambao waliomba leseni hizo kinyume na mifumo halali ya nchi pamoja na wamiliki wa magari ambayo namba zake zilikutwa kwa watuhumiwa hao.

“Tutawatafuta watu hao ili watusaidie kujua utaratibu walioutumia kujipatia leseni na namba hizo za magari kupitia kwa watuhumiwa hao badala ya mamlaka rasmi zinazotambulika na serikali,”alisema Kamanda huyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news