Waziri Dkt.Mabula aweka wazi idadi ya nyumba nchini huku mahitaji yakiwa makubwa

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Dkt.Angeline Mabula amesema,pamoja na changamoto ya riba za mikopo ambayo inatolewa katika mikopo ya nyumba hapa nchini, bado Taifa linakabiliwa na uhaba mkubwa wa nyumba hususani nyumba bora na zenye gharama nafuu.

"Kwa mujibu ya Sensa ya Watu na Makazi ambayo tumekamilisha Agosti, mwaka jana (2022) wote tunatambua sasa Watanzania tuko milioni 61.7 ambao kwa kiasi kuna ongezeko la asilimia 3.2 na idadi ya majengo tuliyonayo ni milioni 14,348,572 ambapo majengo yasiyo ya ghorofa ni milioni 13,540,363 sawa na asilimia 94.3 ya majengo yote nchini.

"Na katika hayo maghorofa yako 68,742 sawa na asilimia 0.5, hivyo mahitaji ya nyumba bado ni makubwa na ukichukua kwa hesabu ya haraka haraka ambayo tukiangalia kwa namna takwimu zilizokuja Watanzania na idadi ya majengo tuliyonayo bado tunatakiwa pengine kuwa na nyumba zisizopungua kwa mwaka 390,981.

"Na kwa rekodi za nyuma zilizokuwepo tulikuwa tunasema tunahitaji walau nyumba 200,000 kila mwaka, lakini kwa sensa ambayo ilimalizika hivi karibuni tunatakiwa kuwa na nyumba walau 390,981;

Mheshimiwa Dkt.Mabula ameyasema hayo Februari 17, 2023 jijini Dar es Salaam katika hafla ya utiaji saini Hati ya Maelewano (MoU) baina ya Benki ya Absa Tanzania na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa lengo la benki hiyo kuwezesha wateja wake kupata mkopo ulioboreshwa kwa ajili ya manunuzi ya nyumba.

"Kwa hiyo unapoangalia unakuta kuna gape kubwa ambalo hatuwezi kuli-cover, kwa hiyo tunahitaji taasisi kama hizi zinazokuja na bidhaa mpya kwa ajili ya watu kupata nyumba na kuziba mapengo tunayokuwa nayo.

"Kwa takwimu hizi tunaweza kuona kwa namna gani kasi ya taasisi za uendelezaji miji zinatakiwa kuzalisha nyumba kwa kasi kubwa.

"Ukiangalia nyumba zilizojengwa tangu 2010 mpaka 2022 zimeweza kujengwa nyumba 14,000 tu sawa na nyumba 1,153 kwa mwaka, sasa tunaona jinsi tulivyo nyuma. Ni wazi kwamba bado tuko mbali na tunahitaji kwenda kwa kasi na kupata wabunifu wapya watakaowezesha watu kupata nyumba,"amefafanua Waziri Dkt.Mabula.

Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula amebainisha kuwa, jitihada hizo za benki kwa kushirikiana na Shirika la Nyumba la Taifa zitaipa faraja Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye naye pia imekuwa ni doto yake kutaka kuona Watanzania wanafanikiwa kuwa na makazi bora na kuwa na mahali panapotunza heshima ya Mtanzania.

Waziri Dkt.Mabula amebainisha kuwa, Sekta ya Nyumba uwekezaji wake unahitaji rasilimali fedha nyingi ambazo kwa hali ya kawaida ni vigumu kuzipata kwa wakati, lakini taasisi za fedha zinapoingia kati na kuwezesha upatikanaji wa mikopo yenye masharti nafuu kwa ajili ya nyumba wanafungua fursa za wengi kumiliki nyumba zao nchini.

"Sote tunafahamu uwekezaji katika Sekta ya Nyumba unahitaji kiasi kikubwa cha fedha, hivyo benki na taasisi za fedha zina michango mikubwa katika kukuza Sekta ya Nyumba nchini na kwa upande wa Serikali zipo jitihada zinafanywa ambazo zinakuza sekta ya fedha moja kwa moja ikiwemo suala la uanzishwaji wa mikopo ya nyumba.

"Hatua hizo ziliwezesha uanzishwaji wa Taasisi ya Tanzania Mortgage Refinance Company (TMRC) mwaka 2010 na kuanzisha pia mfuko wa mikopo midogo midogo ya Nyumba mwaka 2015, hizi zote zilikuwa ni jitihada za Serikali kutaka kumwezesha Mtanzania wa kawaida kuweza kumiliki nyumba."

"Uanzishwaji wa taasisi hizi umewezesha pia benki na taasisi kadha kuweza kuwa na mitaji kwa ajili ya mikopo ya nyumba kwa ajili ya Watanzania,"amefafanua.

Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula amebainisha kuwa, katika kutekeleza azima hiyo TMRC walianza na mabenki matatu katika zoezi lao la kukopesha, lakini kwa sasa wanazo benki 32 ambazo zinatoa mikopo.

"Na mikopo ambayo walikuwa wakiitoa ilikuwa inacharge kiasi cha asilimia 20 hadi 24. Sasa hivi kuna punguzo kidogo la asilimia 15 hadi 18, lakini ukiangalia kwa namna ambavyo tunakwenda mwendo huu kidogo bado tunasuasua, mahitaji ni makubwa uwezo ni mdogo, lakini pia na pesa zenyewe mtu anavyoaangalia anaona kama vile ni usumbufu kwa namna moja japokuwa anarahisishiwa kazi yake.

"Pia kumekuwa na wastani la ongezeko la muda wa marejesho kutoka kwa miaka mitano, sasa hivi wanakwenda kwenye miaka 15 mpaka 25 na tangu wameanza mpaka sasa ni jumla ya shilingi bilioni 552.95 zimetolewa kwa wateja 5,992 ni muda mrefu sasa toka imeanza.

"Lakini wadau wanaokwenda kupata huduma hiyo bado ni wachache, lazima tujiulize kwa nini ni wachache pengine product hii inagharama kubwa au masharti ni makubwa kadri tunavyozidi kupata taasisi zingine ambazo zinakuja na utaratibu mwingine katika kukopesha au kuwezesha Watanzania kupata nyumba basi pia inasaidia Serikali kufikiri mara mbilimbili nini cha kufanya katika kurahisha maisha kwa Mtanzania,"amebainisha Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

1 Comments

  1. Waziri pamoja najitihada kubwa zianazofanywa na serikali yapo maeneo hayajatiliwa mkazo kama vile kuwasaidia Wamiliki Ardhi na Nyumba nchini kuwapunguzia gharama za vifaa vya ujenzi kama vile, mabati,Nondo,na simenti,pamoja na kitoa mikopo yenye masharti nafuu ili waweze kujenga na kukarabati Nyumba.Tunaomba tushirikiane na sis Chama Cha Wamiliki Ardhi na Nyumba Tanzania.JU
    MA K. Mng'ombe Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki Ardhi na Nyumba Tanzania

    ReplyDelete
Previous Post Next Post

International news