Wizara ya Madini kuiketisha Dunia kwa siku mbili nchini

NA GODFREY NNKO

WIZARA ya Madini ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na dmg events na Ocean Business Partners Tanzania imesema Jukwaa la Madini na Uwekezaji Tanzania 2023 litafanyika Oktoba 25 hadi 26,mwaka huu nchini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Februari 10, 2023 na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Madini imefafanua kuwa,wadau wa madini kutoka maeneo mbalimbali duniani watakutana tarehe tajwa katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Jukwaa hilo linafanyika kwa heshima kubwa nchini chini ya mlezi, Dkt.Doto Mashaka Biteko (Mb) ambaye ni Waziri wa Madini kwa ushirikiano mkubwa wa Serikali.

Katika muongo uliopita, Afrika Mashariki imekuwa ikishuhudia Sekta ya Madini ikipanuka kwa kasi. Nchini Tanzania, mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa (GDP) umekuwa ukiongezeka kila mwaka.

Vile vile, katika mwaka 2020/2021 mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa ulipanda hadi asilimia 7.2 kutoka asilimia 6.7 mwaka 2019/2020. Kufuatia hatua hizo, sekta hiyo imekuwa ikiongoza kwa kuingiza fedha za kigeni katika uchumi.

Chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali imekuwa ikijikita katika kuhakikisha Sekta ya Madini inachangia angalau asilimia 10 ya Pato la Taifa ifikapo mwaka 2025.

Aidha,ushirikiano na jumuiya ya kimataifa ili kuhamasisha mitaji na uwekezaji katika Sekta ya Madini ni miongoni mwa mikakati ya kufikia azma hiyo.

Wizara kupitia taarifa hiyo imefafanua kuwa, Kaulimbiu ya Jukwaa la Madini na Uwekezaji Tanzania 2023 ni 'Unlocking Tanzania’s Future Mining Potential’ litaunganisha tena jumuiya ya uchimbaji madini ya Tanzania, Afrika na kimataifa na mawaziri,wakurugenzi wakuu, watunga sera na viongozi wa sekta hiyo jijini Dar es Salaam kukutana ana kwa ana na kujadili mikakati ya ushirikiano ili kufungua na kuendeleza fursa za maendeleo katika sekta hiyo muhimu.

Jukwaa hilo linatarajiwa kuvutia zaidi ya wahudhuriaji 2,000 wa kimataifa kutoka zaidi ya nchi 25, pia litajumuisha mkutano wa hadhi ya kimataifa na wazungumzaji zaidi ya 100, na vikao zaidi ya 20, hotuba kuu na mawasilisho ambayo yataendeshwa kwa pamoja na teknolojia kubwa yakiwemo maonesho ya uvumbuzi.

Jukwaa la mwaka huu litazingatia sana uwekezaji wa madini duniani, ikijumuisha miradi mipya na ubia, teknolojia, kanuni na ufadhili.

Pia litaangazia mada mpya kama vile sera za mazingira, kijamii na utawala, maendeleo ya kimkakati ya madini, uchimbaji endelevu wa madini, na maudhui ya ndani pia yatakuwa katikati ya majadiliano.

Akizungumzia kuhusu Jukwaa la Madini na Uwekezaji Tanzania 2023, Dkt.Doto Biteko (Mb), Waziri wa Madini, amesema, “Ninawaalika wadau wote wa madini nchini Tanzania, kutoka kote barani Afrika na duniani kote kushiriki katika Jukwaa la Madini na Uwekezaji Tanzania.

"Tunatarajia kutoa matangazo muhimu, kuandaa mikutano baina ya nchi na wawekezaji, kuonesha fursa za maendeleo ya miradi na kufanya kazi na washirika wetu wa kitaifa na kimataifa ili kufungua uwezo kamili wa sekta ya madini ya Tanzania.

"Tunatarajia kukutana nanyi jijini Dar es Salaam kwa vile Tanzania sasa iko katika viwango vya juu vya Afrika katika kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje.”

Katika majukwaa matatu yaliyopita, Jukwaa la Madini na Uwekezaji Tanzania limevutia zaidi ya wahudhuriaji 4,500 duniani kwa ushiriki kutoka zaidi ya nchi 15, likijumuisha mkutano wa hadhi ya kimataifa.

Sambamba na maonesho ya teknolojia, hafla ya utoaji tuzo kwa makampuni ya madini na watu binafsi waliofanya vizuri katika nyanja mbalimbali kupitia shughuli zao ndani ya Usiku wa Madini Gala. Jukwaa hili limekuwa moja ya hafla kubwa zaidi zinazofanyika nchini. Jifunze www.tanzaniamininginvestmentforum.com

Kuhusu dmg events

dmg events ni miongoni wa waandaaji wakuu wa hafla kubwa duniani, na hafla 84 katika tasnia kadhaa muhimu, na kuvutia zaidi ya wahudhuriaji 425,000.

Kazi zao katika nishati zinajumuisha baadhi ya matukio makubwa katika sekta hiyo, kama vile ADIPEC, Maonesho ya Petroli ya Misri,Maonesho ya Nishati ya Kimataifa. Zaidi www.dmgevents.com

Kuhusu Ocean Business Partners Tanzania

Ocean Business Partners Tanzania ni kampuni ya ushauri ya wazawa, na inayozingatia utaalamu katika fani mbalimbali za biashara katika Mafuta, Gesi, Nishati, Usafirishaji, Ushauri wa Uwekezaji, Ushauri wa Biashara, Ushauri wa Vihatari, Uhandisi wa Miradi na Fedha hayo yakiwa ni kwa uchache.

Washirika wa Biashara wa Ocean Tanzania wanajivunia kusaidia wateja wake mbalimbali kuanzia hatua ya msingi ya kubuni mawazo mapya ya mradi, hadi utekelezaji, na kutoa bidhaa au huduma zao katika soko la Mafuta, Gesi na Nishati.

Wanalenga kuunda mipango ya biashara ya kibinafsi kwa wateja wao ambayo inafikiriwa vyema na timu yao ya washauri ambao wanajivunia sana uzoefu wao wa vitendo katika Sekta ya Mafuta na Gesi na nyanja zingine zinazohusiana.

Wanaamini katika kutafuta suluhu kwa ushirikiano wa kazi yoyote ya mtu binafsi, na kufanya kazi pamoja kama timu na wateja wao. Jifunze zaidi www.obp-tanzania.co.tz

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news