7G: HII ZAWADI KWA MAMA

NA DIRAMAKINI

LEO Machi 18, 2023 Klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam imefanikiwa kutinga robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika baada ya kuifunga Horoya FC mabao 7-0.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, ushindi huu wa kishindo ni zawadi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye anatimiza miaka miwili madarakani.

Ikumbukwe kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia imetoa kipaumbele kikubwa katika Sekta ya Michezo ikitambua kuwa, licha ya michezo kudumisha afya pia ni fursa kubwa ya ajira kwa vijana.

Ndiyo maana Rais Dkt.Samia hivi karibuni alitangaza kutoa hamasa ya milioni tano kwa kila bao litakalofungwa na Simba na Yanga katika michezo yao ya Afrika ngazi za vilabu barani Afrika. Na leo, Simba SC imechukua milioni 35 kutoka kwa Rais Dkt.Samia. Endelea;

1.Hii zawadi ya Mama, Rais wetu Samia,
Magoli saba mazima, kwa miwili ya Samia,
Anatuongoza vema, Rais wetu Samia,
Hongera ushindi Simba, kazi nzuri kwa Samia.

2.Tunakupongeza Mama, kuongoza Tanzania,
Kwa vitendo tunasema, magoli twakupatia,
Huu ni ushindi mwema, watangaza Tanzania,
Hongera ushindi Simba, kazi nzuri kwa Samia.

3.Simba imefanya vema, vema kupeperushia,
Bendera yetu salama, inang’ara Tanzania,
Magoli saba mazima, hiyo heko kwa Samia,
Hongera ushindi Simba, kazi nzuri kwa Samia.

4.Rais mefanya vema, hamasa kutupatia,
Kiwanjani twajituma, pesa zipate ingia,
Nawe wazidi zitema, kapuni zinaingia,
Hongera ushindi Simba, kazi nzuri kwa Samia.

5.Saba Jii hii njema, kwake Rais Samia,
Na tema mama ni mwema, mapesa kutupatia,
Tunazidi kusimama, juu tunajipandia,
Hongera ushindi Simba, kazi nzuri kwa Samia.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news