SIMBA KWELI MNATISHA, ROBO FAINALI NDANI

NA DIRAMAKINI

LEO Machi 18, 2023 Klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam imefanikiwa kutinga robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika baada ya kuifunga Horoya FC mabao 7-0.

Ni kupitia mchezo uliopigwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam. Katika mchezo huo wa aina yake, kiungo mshambuliaji Clatous Chama amepiga hat trick.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa,ushindi huo si heshima kwa mashabiki na uongozi wa klabu hiyo tu, bali kwa Taifa lote. Endelea;

1.Hii ni dozi ya wiki, Jumamosi kunywa Chama,
Jumapili haifiki, hapo tena anywe Chama,
Ili iwe na mantiki, Jumatatu mpe Chama,
Simba kweli mnatisha, mlivyotuheshimisha.

2.Jumanne badilisha, Horoya anywe Baleke,
Na hiyo dozi zidisha, na Jumatano Baleke,
Alhamisi fikisha, ni Kanoute si Baleke,
Simba kweli mnatisha, mlivyotuheshimisha.

3.Haponi huyu Horoya, Ijumaa ni Kanoute,
Wiki hiyo bila haya, kapigwa magoli yote,
Sasa Simba on faya, ngazi apande apite,
Simba kweli mnatisha, mlivyotuheshimisha.

4.Mama Samia asante, kutupa mamilioni,
Thelathina tano zote, zaingia mfukoni,
Na wewe raha upate, robo fainali ndani,
Simba kweli mnatisha, mlivyotuheshimisha.

5.Hii ni jioni njema, sote tunafurahia,
Simba mmefanya vema, raha mmetupatia,
Baleke Kanoute Chama, maji tunamwagilia,
Simba kweli mnatisha, mlivyotuheshimisha.

6.Malengo yametimia, hatua tulofikia,
Huko tumeshaingia, timu twaisubiria,
Kwa kweli tumepania, juujuu kufikia,
Simba kweli mnatisha, mlivyotuheshimisha.

7.Walobakisha kiporo, heri tunawatakia,
Wasijekulala doro, kuchefua Tanzania,
Wafanye yasiyo kero, nchi kuing’arishia,
Simba kweli mnatisha, mlivyotuheshimisha.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news