Barabara ya Makongorosi-Rungwa-Itigi hadi Mkiwa kujengwa kwa kiwango cha lami

NA MWANDISHI WETU

SERIKALI imeanza kuunganisha mikoa ya nyanda za juu Kusini kwa kuijenga kwa kiwango cha lami barabara ya Makongorosi-Rungwa-Itigi hadi Mkiwa sehemu ya Noranga hadi Itigi katika kitongoji cha Mlongojii chenye urefu wa kilometa 25 kwa upande wa Mkoa wa Singida kwa lengo la kukuza uchumi wa mikoa hiyo.
Muonekano wa sehemu ya barabara ya Noranga – Itigi (km 25), inayojengwa kwa kiwango cha lami, mkoani Singida. Ujenzi wa barabara hiyo unatarajiwa kukamilika mwezi Machi, 2024 kwa gharama ya shilingi Bilioni 29.770.

Hayo yamesemwa wilayani Manyoni mkoani Singida na Naibu Waziri wa Ujenzi,Mhandisi Godfrey Kasekenya, wakati alipokagua hatua ya ujenzi wa mradi huo pamoja na ujenzi wa barabara za mji wa Itigi (km 10) kwa kiwango cha lami.

Mhandisi Kasekenya ameeleza kuwa, barabara hiyo ilikuwa ikitumika miaka ya 1970 kabla ya barabara ya TANZAM haijajengwa kwa kiwango cha lami na sasa Serikali imeona umuhimu wa kuijenga barabara hiyo na imetoa fedha kiasi cha shilingi Bilioni 29.770 kwa mkandarasi China Henan International Cooperation ya China ili kuikamilisha kwa muda wa miezi 18.

“Abiria waliokuwa wakisafiri kwenda Mbeya, Iringa na mikoa mingine ya nyanda za juu kusini kutoka kanda ya ziwa walikuwa wakija na treni mpaka itigi na kuchukuliwa na mabasi kwenda Mbeya na mikoa mingine ya nyanda za juu kusini hivyo barabara hii ni muhimu sana kiuchumi,”amefafanua Mhandisi Kasekenya.

Mhandisi Kasekenya ametoa maelekezo kwa Wahandisi Washauri kutoka Kitengo cha Usimamizi wa Miradi cha Wakala ya Barabara nchini (TANROADS) – TECU, kuhakikisha wanawasimamia wakandarasi hao kwa viwango vinachotakiwa na usanifu uliowekwa katika miradi hiyo.
Mhandisi Mkazi kutoka Kitengo cha Usimamizi wa Miradi TANROADS – TECU, Eng. Nada Shauri, akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi. Eng. Godfrey Kasekenya, wakati akikagua ujenzi wa barabara za mji wa Itigi (km 10) kwa kiwango cha lami, mkoani Singida.

“TECU dhamana mliyopewa ni kubwa katika usimimazi wa hii miradi na Rais wetu anatoa fedha nyingi katika ujenzi wa miundombinu anachokihitaji kutoka kwetu ni thamani ya fedha ionekane katika miradi ya barabara nchini,” amesisitiza Naibu Waziri Kasekenya.

Aidha, Kasekenya amewaagiza TANROADS kushirikisha taasisi nyingine kama wana mipango miji, Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) pindi wanapofanya usanifu wa barabara hasa za mijini ili kuweza kuimarishwa kwa mifumo ya mifereji kwaajili ya maji kwani mvua zinaponyesha maji yanashindwa kwenda kwenye maeneo husika na kuleta kero hasa wanaopitiwa na barabara za mijini.

Pia ametoa wito kwa wananchi kuzitunza barabara hizo kwa kutokuzitumia vibaya ambapo amewasihi kuacha kupitisha mifugo, kumwaga mafuta, kuiba alama za barabara na madaraja na kutupa taka ovyo katika mifereji ya barabara hasa za mijini.

Pamoja na hayo Naibu Waziri Kasekenya ameridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo ambapo ikikamilika italeta mabadiliko makubwa sana ya kiuchumi, kimaendeleo na kijamiii kwa wananchi wa Itigi na Singida kwa ujumla.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Kemilembe Rose Lwota amemuahidi Naibu Waziri huyo kusimamia utekelezaji wa maagizo yote yaliyotolewa ikiwemo uwepo wa mifereji ya maji ili kuzuia maji ya mvua kuathiri baadhi ya makazi ya watu. 
Muonekano wa Daraja la Msingi lenye urefu wa mita 100 na upana wa mita 10 pamoja na barabara za maingilio zenye urefu wa KM 1 ambao ujenzi wake umekamilika, wilayani Mkalama mkoani Singida.

Naye Meneja wa TANROADS mkoa wa Singida,Mhandisi Msama Msama, ameeleza kuwa sehemu ya ujenzi wa Noranga hadi Itigi (km 25) mkandarasi ameshaleta mitambo yote kwa asilimia 75 na ameshaanza kazi ya kuzalisha kokoto za ujenzi ambapo kwa ujumla mradi umefikia asilimia 18 na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Machi, 2024.

Ameeleza kuwa kwa upande wa mradi wa barabara za mji wa Itigi (km 10) unajengwa na mkandarasi mzawa kutoka kampuni ya Rocktronic kwa gharama ya shilingi Bilioni 8.598 kwa muda wa miezi 18 ambapo unatarajiwa kukamilika mwezi Julai, 2022 na mpaka sasa mradi umefikia asilimia 68.

Naibu Waziri Kasekenya yupo mkoani Singida katika ziara ya ukaguzi wa miradi inayoendelea kutekelezwa na Sekta ya Ujenzi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news