Jumuiya ya Wazazi yatoa kongole kwa Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT)

NA FRESHA KINASA

SHIRIKA la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) linalojishughulisha na kupambana na vitendo vya ukatili wa Kijinsia katika Mkoa wa Mara limepongezwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya chama hicho, Fadhili Maganya kwa juhudi za kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Mkurugenzi wa Hope for Girls and Women, Rhobi Samwelly akimkabidhi Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho (CC), Fadhili Maganya tuzo ya heshima alipotembelea Kituo cha Hope Mugumu Nyumba Salama.

Mwenyekiti huyo, ametoa pongezi hizo jana alipotembelea Kituo cha Hope Mugumu Nyumba Salama kinachomilikiwa na shirika hilo kilichopo Mugumu wilayani Serengeti mkoani Mara.
Amesema, Chama Cha Mapinduzi katika ilani yake kinakemea vitendo vya ukatili wa kijinsia na kitaendelea kutoa ushirikiano kwa shirika hilo na wadau wote wanaopambana na vitendo vya ukatili katika kuimarisha haki na usawa wa Kijinsia kwa maendeleo. 

Shirika la hilo, linamiliki vituo viwili ambavyo hutoa hifadhi kwa wasichana wanaokimbia vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ukeketaji na ndoa za utotoni ambapo ni pamoja na Kituo cha Hope Mugumu Nyumba Salama ambacho kipo Mugumu wilayani Serengeti na Kituo cha Nyumba Salama ambapo kipo Kiabakari Wilayani Butiama. 
Aidha, wasichana wanaopata hifadhi katika vituo hivyo huendelezwa kitaaluma na kifani sambamba na kufundishwa haki zao, kupewa ushauri wa kisaikolojia, mafundisho ya kiroho na huduma zote muhimu ili wafikie ndoto zao. 

Rhobi Samwelly ambaye ni Mkurugenzi wa shirika hilo (HGWT), amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwaruhusu watoto wa kike waliopata ujauzito wakiwa masomoni kuendelea na masomo yao jambo ambalo linawezesha kupata haki ya elimu na kufikia ndoto zao. 

Pia, Rhobi amekipongeza Chama Cha Mapinduzi kwa kuendelea kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia sambamba na kutoa msisitizo kwa umma kuachana na vitendo hivyo ambavyo vinakiuka haki za binadamu na Sheria za nchi. 
Aidha, Mkurugenzi wa Hope for Girls and Women in Tanzania Rhobi Samwelly alimkabidhi tuzo ya heshima Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi na Mjumbe wa Kamati kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi, Fadhili Maganya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news