BINTI HAYA YAPOKEE-1

NA LWAGA MWAMBANDE

MCHUNGAJI Imani Oscar Katana wa Kanisa la Baptist la Moto Ulao lililoko Dege katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni jijini Dar es Salaam ameendelea kuwa baraka kubwa, kwa mabinti kutokana na uendeshaji wa darasa la mabinti ambalo limekuwa likifanyika kwa msimu wa nne sasa.

Darasa la mabinti wenye hofu ya Mungu.Ambao wanaamini na kuenenda katika Neno kupitia kanisa hilo wamekuwa wakijitunza na kukataa kujichafua ili wawe wakfu kwa ajili ya Mungu na waume zao watarajiwa.

Pia, mabinti wamekuwa wakipata nafasi ya kujifunza pamoja na mabinti Sayuni na huwa wanapata nafasi ya kujifunza mambo yahusuyo msichana mcha Mungu,maombi na kufanya mitihani ya Biblia.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande kwa heshima na unyenyekevu mkubwa kwa mtumishi huyu wa Mungu, amemuomba Mungu ampe hekima ya juu kupitia mafundisho hayo yaliyojaa baraka nyingi na kuyaelewa, baada ya hatua kwa hatua anakushirikisha jambo kupitia mashairi mfululizo. Endelea;


1. Unataka usogee,
Watu wakuongelee,
Uwepo wachekelee,
Utafute upekee.

2. Wosia uupokee,
Na kwako usipotee,
Kuishi uendelee,
Utafute upekee.

3. Binti haya yapokee,
Pazuri usogelee.
Na pema uogelee,
Utafute upekee.

4. Yeyote asitokee,
Ya kwake yakukolee,
Njia yako ipokee,
Utafute upekee.

5. Uonao wa pekee,
Maisha yao si chee,
Kujifunza jitolee,
Utafute upekee.

6. Thamani jiongezee,
Hadi ufike uzee,
Kung’aa uendelee,
Utafute upekee.

7. Kwanza vaa kipekee,
Utoke upendezee,
Macho kwako yasogee,
Utafute upekee.

8. Watu wakuongelee,
Na wasikupotezee,
Ni kijana si mzee,
Utafute upekee.

9. Mwonekano wamezee,
Wasitake upotee,
Kucheki waendelee,
Utafute upekee.

10. Weee binti wa pekee,
Umeumbwa kipekee,
Nawe ishi kipekee,
Utafute upekee.

11. Wengine waendelee,
Kuiga wapendelee,
Acha huko wapotee,
Utafute upekee.

12. Nguo nzuri zizoee,
Za heshima utokee,
Aibu sikutokee,
Utafute upekee.

13. Hata wengi mtokee,
Na watu wawazoee,
Wewe uwe wa pekee,
Huo wako upekee.

14. Vema wakuongelee,
Jina lako lienee,
Kwa mbali wakupepee,
Huo wako upekee.

15. Na yako uendelee,
Karama uichochee,
Mungu simpotezee,
Uwe wako upekee.

16. Mwenendo uongezee,
Tabasamu likolee,
Na watu uwachekee,
Uwe mtu wa pekee.

17. Wakuone wamezee,
Kibidi wakumendee,
Wakija uwapokee,
Utafute upekee.

18. Mipango iendelee,
Posa na wakuletee,
Hadi ndoa ikolee,
Utafute upekee.

19. Mtaani utokee,
Kijiji ukolee,
Vema wakuelezee,
Wako huo upekee.

20. Na wewe uendelee,
Mtu asikuchezee,
Njia yako upotee,
Utafute upekee.

21. Heshima iendelee,
Wakubwa waipokee,
Na wadogo wasogee,
Utafute upekee.

22. Hata watu wachochee,
Maneno yakulemee,
Watetezi watokee,
Huo wako upekee.

23. Jua wewe wa pekee,
Mwingine asitokee,
Yake ndiyo yakolee,
Utafute upekee.

24. Mafunzo uyapokee,
Yale mema yakolee,
Busara yaongezee,
Utafute upekee.

25. Kuiga kusitokee,
Hata watu waachochee,
Dirayo iendelee,
Utafute upekee.

26. Jinsi uko wa pekee,
Thamani iendelee,
Na kamwe isipotee,
Utafute upekee.

27. Muonekano pekee,
Na mwenendo wa pekee,
Na mavazi ya pekee,
Utafute upekee.

28. Fanya wakuongelee,
Wema kwako ukolee,
Heri wakuongezee,
Huo wako upekee.

29. Watoto wakuzoee,
Ulivyo waelezee,
Waje kuwa wa pekee,
Una heri upekee.

30. Mungu akuongezee,
Baraka ziendelee,
Pakubwa utokezee,
Huo wako upekee.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602


Utenzi huu ni sehemu ya mafundisho ya Mchungaji Imani Oscar Katana (0752 352 116) wa Kanisa la Baptist la Moto Ulao lililoko Dege, Kigamboni jijini Dar es Salaam ambayo ameyatoa katika mitandao ya kijamii kwa ajili ya mabinti. mashairi haya yatakujia katika sehemu saba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news