BINTI:USIPOTEZE BAHATI-6

NA LWAGA MWAMBANDE

MSOMAJI karibu katika sehemu ya sita ya mfululizo wa mashairi haya ambayo yamelenga kuwapa mwanga mabinti wetu nchini ili waweze kutambua thamani yao kwa mustakabali mwema wa maisha yao, familia, jamii na Taifa.

Picha na freepik.

Ni imani yake mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande kuwa, kupitia mfululizo huu kuna jambo ambalo unajifunza, kumbuka tunatakiwa kuendelea kujifunza maishani mwetu. Endelea;


1. Ijali lafuzi yako,
Hata matamshi yako,
Yawe ni mvuto wako,
Yasifukuze bahati.

2. Kung’ata maneno yako,
Kama mwigizaji wako,
Wakati huko si kwako,
Utafukuza bahati.

3. Huo Unyakyusa wako,
Au na Uhaya wako,
Na hilo kabila lako,
Usipoteze bahati.

4. Hiyo arogansi yako,
Kwa huo usemi wako,
Wewe ni adui yako,
Utafukuza bahati.

5. Wewe na ubinti wako,
Hata hujafika kwako,
Kumpata mwenzi wako,
Usifukuze bahati.

6. Jipange maneno yako,
Levo ya sauti yako,
Huo utulivu wako,
Jua waita bahati.

7. Mfanano wako huko,
Apenda mapozi yako,
Na uongeaji wako,
Wapalilia bahati.

8. Kufoka kusiwe kwako,
Kusemasema si kwako,
Hizo ni vurugu kwako,
Usipoteze bahati.

9. Zitafute swaga zako,
Hayo maongezi yako,
Onyesha mvuto wako,
Unaiita bahati.

10. Kusema silaha yako,
Huku kuinuka kwako,
Hata kuanguka kwako,
Itengenezee bahati.

11. Kwa hayo mapozi yako,
Huo usikivu wako,
Nao usemaji wako,
Silaha ya mkakati.

12. Hayo matamshi yako,
Nalo tabasamu lako,
Kunjakunja uso mwiko,
Andaa yako bahati.

13. Ufanye kufika kwako,
Ndugu na jamaa zako,
Sura iwe ni mwaliko,
Usipoteze bahati.

14. Maneno upole wako,
Na hata adabu yako,
Hizo ndio nyenzo zako,
Tena za kimkakati.

15. Pengine maisha yako,
Ni hizo kauli zako,
Zitavuta watu kwako,
Uipate njema hati.

16. Na pia usemi wako,
Ule wa mkanganyiko,
Ndiyo kizuizi chako,
Kunyaka yako bahati.

17. Hii ni elimu kwako,
Kwa mdomodomo wako,
Faida na hasara kwako,
Meshikilia bahati.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Utenzi huu ni sehemu ya Mafundisho ya Mchungaji Imani Oscar Katana (0752 352 116) wa Kanisa la Baptist la Moto Ulao lililoko Dege Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni jijini Dar es Salaam ambayo ameyatoa katika mitandao ya kijamii kwa ajili ya Mabinti. Utenzi uko sehemu saba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news