Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) waja kivingine

NA DIRAMAKINI

CHAMA cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kimewaomba wadau na wanachama wa chama hicho kukichangia chama ili kufanikisha mikutano yake ya hadhara ambayo inatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu.
Wito huo umetolewa Machi 11, 2023 jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti Taifa wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Hashim Rungwe Spunda mara baada kikao cha Kamati kuu ya chama hicho.

Rungwe amesema, kwa sasa chama hakina pesa za kutosha za kuendesha mikutano yao nchi nzima hivyo wanatarajia kufanya mikutano yao ya awali kwa kuwafuata wananchi katika maeneo yao ya shughuli ikiwemo maeneo ya masoko na stedi za mabasi.

"Tunawaomba wadau,mashabiki na wanachama kukichangia chama kupitia akaunti zetu za CHAUMMA kwani kwa kufanya hivyo kutawezesha kufanikisha kufanya kampeni zetu na kutoa sera za chama na kuainisha mapungufu ya Serikali inayotutawala ambayo inaongozwa na CCM,"amesema Hashim Rungwe.

Mbali na hayo kupitia kikao hicho kimewapongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt.Hussein Alli Mwinyi kwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo huku wakitumia nafasi hiyo kumuomba Rais Samia kukubali mialiko kutoka vyama vingine vya upinzani.

"Tunampongeza Rais Samia kwa kuhudhuria mkutano wa Baraza la Wanawake wa Chama cha CHADEMA (BAWACHA), kwani ni kitendo cha kihistoria ambacho hakijawahi kufanywa hapa nchini na ni kitendo cha ujasiri na cha kidemokrasia na ingependeza kama Rais Samia angevitembelea na vyama vingine,"amesema Hashim Rungwe.

Naye Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Mohammed Masoud Rashid amewataka wanawake kujitokeza kwa wingi kujiunga na CHAUMMA na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi huku akisisitiza kuwa chama hicho kinatoa fursa za kutosha kwa wanawake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news