Hebu ongeza vituo, uza gesi asilia

NA LWAGA MWAMBANDE

KWA mujibu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Tanzania ina gesi asilia futi za ujazo trilioni 57, kiwango ambacho ni kikubwa kwa nishati inayohitajika nchini.

Tanzania imekuwa ikifanya utafiti wa gesi asilia kwa zaidi ya miaka 50. Ugunduzi wa kwanza wa gesi asilia nchini ulifanyika mwaka 1974 katika Kisiwa cha Songo Songo kilichopo Mkoa wa Lindi na kufuatiwa na ugunduzi wa pili katika eneo la Mnazi Bay mkoani Mtwara mwaka 1982.

Gesi asilia kutoka Songo Songo iliuzwa kwa mara ya kwanza mwaka 2004 na ya kutoka Mnazi Bay mwaka 2006. Ugunduzi huo umechochea kufanyika utafiti zaidi wa gesi asilia kwa maeneo ya nchi kavu na majini.

Wingi huo ndiyo uliovutia zaidi, mwaka 2022 Tanzania ikatiliana saini mkataba wa gesi na kampuni za Shell ya Uingereza na Equinor ya Norway ili kuutekeleza mradi wa dola bilioni 30 wa kuiwezesha kuuza gesi yake asilia.

Kulingana na mkataba huo, uwekezaji kwa ajili ya mradi huo utakamilishwa mwaka 2025 na kuanza shughuli kati ya mwaka 2029 na 2030 kwenye mtambo wa gesi ya kioevu utakaojengwa mkoani Lindi.

Aidha, hii inatajwa kuwa ni hatua muhimu ya kusonga mbele kwa Tanzania ya kuanzisha usafirishaji nje wa sehemu ya akiba kubwa ya rasilimali hiyo iliyopo kwenye sehemu za Pwani.

Katika hafla hiyo, Waziri wa Nishati, Mheshimiwa January Makamba alisema, Taifa halijawahi kufikia hatua kama hiyo ya maendeleo katika sekta ya gesi katika historia yake. Waziri Makamba alisema, mradi huo utaubadilisha uchumi wa Tanzania kwa kiasi kikubwa.

Watafiti wanaeleza kuwa, kijografia, ni rahisi kwa Tanzania kusafirisha nje gesi asilia na hasa kwa nchi za bara la Asia zinazotafuta masoko mapya ya nishati.

Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan aliyekuwepo kwenye hafla ya kutia saini mkataba huo aliubariki.

Alisema, hatua hiyo muhimu ilifikiwa katika mazungumzo juu ya mradi huo wa gesi asilia, lakini alieleza kuwa bado kuna kazi kubwa ambayo Tanzania inapaswa kuifanya katika utekelezaji na kuipa nchi uwezo wa kushindana katika sekta ya gesi duniani.

Kila mmoja wetu anatambua kuwa, gesi asilia ina faida nyingi ikiwemo kukuza teknolojia,nishati rafiki na salama, ni ya kuaminika, haiathiriwi na hali ya hewa.

Pia ni safi kuliko mafuta mengine, haina madhara, bei ya chini kuliko mafuta mengine, tulivu kwa matumizi ya majumbani, usafirishaji na matumizi mengineyo.

Kutokana na thamani iliyopo katika gesi hiyo asilia, mshairi wa kisasa,Lwaga Mwambande anasisitiza ni jambo la heri kuona juhudi mbalimbali zinafanywa na Serikali kuhakikisha inaendelea kuwa na tija zaidi huku akiomba nguvu kubwa ielekezwe pia katika kuongeza vituo vya kuuza gesi hiyo nchini. Endelea:


1. Jamani fanyeni kitu, adha wapunguzieni,
Hawa wa nishati kwatu, wa Dasalamu jijini,
Si hewa ukaa katu, gesi nzuri duniani,
Hebu ongeza vituo, uza gesi asilia.

2. Iweje ni viwili tu, vituo huko jijini,
Huku magari ya watu, yanazidi kusheheni?
Kila siku foleni tu, watu hawako kazini?
Hebu ongeza vituo, uza gesi asilia.

3. Gesi yetu ni madini, dhahabu ya duniani,
Si kwa fedha za kigeni, tunaipata nchini,
Vipi kwetu vituoni, zabaki ndefu foleni?
Hebu ongeza vituo, uza gesi asilia.

4. Ushawishi minadani, wa matumizi makini,
Mwingi sana chunguzeni, yaingia akilini,
Gesi asili amini, bei bora mkononi,
Hebu ongeza vituo, uza gesi asilia.

5. Magari barabarani, yaongezeka nchini,
Watoa mamilioni, mitungi iko garini,
Sasa kwa vipi foleni, inazidi vituoni?
Hebu ongeza vituo, uza gesi asilia.

6. EWURA mko kazini, hata hili lioneni,
Matumizi yasheheni, gesi kwa wengi nchini,
Lakini hizi foleni, karaha sana jijini,
Hebu ongeza vituo, uza gesi asilia.

7. Hata huko wizarani, Nishati angalieni,
Ni bora hamasisheni, wawekezaji nchini,
Tukate hizi foleni, watu waende kazini,
Hebu ongeza vituo, uza gesi asilia.

8. Kwa Ubungo kituoni, magari yanasheheni,
Na Tazara kituoni, foleni siyo utani,
Wateja angalieni, tena wasaidieni,
Hebu ongeza vituo, uza gesi asilia.

9. Vituo visambazeni, kotekote pelekeni,
Mitungi ilosheheni, ijazwe pasi foleni,
Wengine wavutieni, waweke gesi garini,
Hebu ongeza vituo, uza gesi asilia.

10. Hii gesi ileteni, huju kwetu mitaani,
Wengiwengi tumieni, magari barabarani,
Ipikiwe majumbani, bila fedha za kigeni,
Hebu ongeza vituo, uza gesi asilia.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news