HEKO KWAKO MWANAMKE

NA LWAGA MWAMBANDE

LEO Machi 8, 2023 wanawake nchini wanaungana na wenzao kutoka kila kona ya Dunia kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.
Wanawake mafundi wanaofanya kazi katika kituo cha kuhamisha teknolojia cha mRNA (The mRNA Vaccine Technology Transfer Hub in South Africa) nchini Afrika Kusini hivi karibuni. (Picha na MPP/WHO/Rodger Bosch).

Ni sherehe ambazo zinaadhimishwa kwa kuangazia nyanja za mafanikio, changamoto na hata mustakabali wao, sio tu kwa wanawake bali pia wasichana popote walipo.

Aidha, Umoja wa Mataifa umekiri kwamba makundi haya yanakabiliwa na vikwazo vingi, na kutoa wito kwa Dunia kuchukua hatua na kusimama pamoja na wanawake ili wapate haki zao za msingi na kuwalinda dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amekiri alipokuwa akitoa salamu za maadhimisho hayo kwamba, ingawa Dunia inasherehekea mafanikio ya wanawake, lakini ni lazima kila mmoja kutambua kwamba bado kuna changamoto zinazowakabili ambazo zinamuhitaji kila mmoja kushiriki ili kuzizuia ama kuziondoa kabisa popote pale.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema, maadhimisho haya ambayo yanaongozwa na kauli mbiu ya 'Ubunifu na Mabadiliko ya Teknolojia ni Chachu katika kuleta Usawa wa Kijinsia', dhamira hiyo itafikiwa iwapo kila mmoja atawajibika, kujituma kwa bidii na kufanya kazi bila kuchoka. Endelea;

1.Ni siku ya wanawake, hapa duniani kote,
Nasi tuna wanawake, heri nyingi wazipate,
Nafasi zao washike, na faida tuzipate,
Usawa kidijitali, haki tufaidi wote.

2.Nyumbani tunao wake, heshima yao wapate,
Majukumu wayashike, usaidizi tupate,
Kututii wasichoke, na mapenzi wayapate,
Usawa kidijitali, haki tufaidi wote.

3.Tuna watoto wa kike, malezi mema wapate,
Wakue wasiteseke, tuje wafaidi wote,
Na watakako wafike, maishani wasijute,
Usawa kidijitali, haki tufaidi wote.

4.Tuna rafiki wa kike, furaha yetu wapate,
Walipo wawajibike, shirikiano wapate,
Tukiwa nao tucheke, sisi tufurahi wote,
Usawa kidijitali, haki tufaidi wote.

5.Wafanyakazi wa kike, na tuwajibike wote,
Madaraka wayashike, tena usawa kwa wote,
Nao pia wainuke, kama wengineo wote,
Usawa kidijitali, haki tufaidi wote.

6.Heko kwako mwanamke, heshima yako upate,
Nafasi yako ishike, mafanikio tupate,
Kututunza usichoke, na Amani tuipate,
Usawa kidijitali, haki tufaidi wote.

7.Hii salamu wa wake, wa kwetu waume wote,
Pia watoto wa kike, walio nyumbani,
Bila ninyi wanawake, tungeadimika wote,
Usawa kidijitali, haki tufaidi wote.

8.Rafiki zetu wa kike, shangwe mzipate wote,
Pamoja tufurahike, siku yenu yetu sote,
Na zidi mneemeke, kwenye kazi zenu zote,
Usawa kidijitali, haki tufaidi wote.

9.Mama zetu wanawake, jua twawapenda nyote,
Dada zetu wanawake, salamu zetu mpate,
Watoto wetu wa kike, dunia ni yenu yote,
Usawa kidijitali, haki tufaidi wote.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news