Jean Baleke afunguka kuhusu mabao matatu, Simba SC yarejea Dar

NA DIRAMAKINI

MSHAMBULIAJI wa Simba SC, Jean Baleke ameweka wazi kuwa amefurahi kufunga mabao matatu ‘hat trick’ kwa mara ya kwanza akiwa na kikosi hicho.

Baleke amefunga hat trick hiyo katika ushindi wa mabao 3-0 walioupata Machi 11, 2023 dhidi ya Mtibwa Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliopigwa Uwanja wa Manungu Complex mkoani Morogoro.

Mshambuliaji huyo amesema, ni furaha kwa kila mshambuliaji kufunga na kuisaidia timu kupata ushindi umuhimu.

Baleke ameahidi kuendelea kuonesha umwamba wa kufumania nyavu kila atakapopata nafasi ya kufanya hivyo.

“Nina furaha kufunga hat trick ya kwanza nikiwa na Simba. Mimi ni mshambuliaji kazi yangu ni kufunga kwa hiyo nawaahidi nitaendelea kufunga,”amesema Baleke. Baleke amefunga mabao hayo katika kipindi cha kwanza kwenye dakika za tatu, saba na 33.

Katika hatua nyingine, baada ya ushindi wa mabao 3-0 waliopata dhidi ya Mtibwa Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliopigwa Uwanja wa Manungu Complex kikosi kilianza safari ya kurejea jijini Dar es Salaam.

Simba SC imeeleza kuwa, baada ya timu kufika wachezaji watapewa mapumziko ya siku moja ambapo watarejea mazoezini Jumatatu kuanza maandalizi ya mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Horoya FC kutoka Guinea.

Mchezo dhidi ya Horoya utapigwa Jumamosi Machi 18, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa saa moja usiku.

Ushindi katika mchezo huo ndio utawapa tiketi ya kufuzu hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo wanaupa umuhimu mkubwa zaidi.

Post a Comment

0 Comments