Simba SC yawaacha hoi Mtibwa Sugar

NA DIRAMAKINI

KLABU ya Simba ya jijini Dar es Salaam imefanikiwa kuzoa alama zote tatu kupitia mabao matatu ‘hat trick’ yaliyofungwa na mshambuliaji Jean Baleke yametosha dhidi ya Mtibwa Sugar.

Ni katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliopigwa Uwanja wa Manungu Complex mkoani Morogoro ambapo hadi dakika ya mwisho ubao ulisoma 3-0.

Baleke alitupatia bao la mapema dakika ya tatu akimalizia mpira wa kichwa uliopigwa na Moses Phiri kabla ya kumzidi mjanja mlinzi wa Mtibwa.

Aidha, Baleke aliongeza bao la pili kwa kichwa dakika ya saba baada ya kumalizia mpira uliopigwa na Saido Ntibanzonkiza kufuatia mpira wa kona aliyoanziwa na Clatous Chama.

Baleke alikamilisha hat trick kwa kufunga bao la tatu dakika ya 33 kwa kichwa akimalizia mpira wa kichwa uliopigwa na Shomari Kapombe.

Hii ni hat trick ya kwanza kwa Baleke tangu ajiunge na klabu hiyo katika dirisha dogo la usajili mwezi Desemba akiwa amefikisha mabao matano kwenye ligi.

Kipindi cha pili Mtibwa walirudi kwa kasi ambapo dakika 15 za mwanzo walifanya mashambulizi kadhaa ambayo hata hivyo yaliishia kwa walinzi wa Simba SC.

Wakati huo huo, kwa matokeo hayo, Simba SC inafikisha alama 57 wakiwa nafasi ya pili kwenye msimamo baada ya kucheza mechi 24.

Post a Comment

0 Comments