Kamati ya Bunge yaguswa na miradi ya NHC

NA MWANDISHI WETU

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imelipongeza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa kazi nzuri inayofanya katika kuendeleza miji na kujenga makazi bora kwa wananchi.
Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Bw. Hamad Abdallah akiwaeleza jambo wajumbe wa kamati hiyo kuhusiana na nyumba hizo. 

Hayo yamesemwa Machi 14, 2024 na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mheshimiwa Jerry Silaa wakati wa ziara ya kamati hiyo katika nyumba za makazi Iyumbu jijini Dodoma kwenye mradi unaotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Mheshimiwa Silaa amesema kuwa, baada ya kutembelea mradi huo,kamati yake imeridhishwa na hatua iliyofikiwa na kuitaka NHC kuendelea kujenga nyumba za namna hiyo katika maeneo mengine nchini ili kuweza kuisaidia Serikali katika azma yake ya kuongeza makazi bora kwa wananchi.

“Kamati inalipongeza sana shirika kwa hatua nzuri iliyofikiwa ya utekelezaji wa mradi huu ambao umechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza adha ya makazi kwa watumishi mbalimbali mara baada ya makao makuu ya Serikali kuhamia Dodoma, hii ni kuonesha kuwa NHC inatambua wajibu iliyo nao kwa nchi na watu wake katika kuhakikisha inawapatia makazi bora watu wake,”amesema Silaa.
Mkurugenzi wa Ujenzi NHC, Mhandisi Haikamen Mlekio (kulia) akimwongoza Bw. Jerry Silaa (katikati) na ujumbe wake kuelekea kwenye nyumba ya mfano.

Amebainisha kuwa, Shirika la Nyumba la Taifa pamoja na mipngo na mikakati iliyo nayo kwa nchi, lakini pia limekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha inabadilisha baadhi ya miji kwa kujenga majengo makubwa ya biashara na nyumba za makazi na kwamba kwa kufanya hivyo inaonesha dhahiri kuwa NHC inaunga mkono juhudi za Serikali.

Wakichangia taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Bw.Hamad Abdallah juu ya utekelezaji wa mradi wa nyumba 1000 jijini Dodoma, wajumbe wa kamati hiyo walilipongeza Shirika la Nyumba la Taifa kwa kazi nzuri inazofanya. 
Mkurugenzi wa Ujenzi, Mhandisi Haikamen Mlekio akitoa maelezo ya nyumba ya mfano kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya PIC, Uongozi wa NHC na wajumbe wa kamati hiyo.

Aidha,wabunge walitaka kujuwa namna shirika linavyosaidia ujenzi wa nyumba za gharama nafuu na kama uwekezaji unaofanyika Dodoma unaweza kuenezwa katika mikoa mingine. 

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurungenzi, Dkt. Sophia Kongela aliwashukuru wajumbe wa kamati kwa kuwa imekuwa ikiisimamia vyema NHC na kuahidi kuyafanyia kazi maagizo matano yaliyotolewa na kamati hiyo kwa ajili ya kuleta tija kwa shirika na Taifa. 

Pia alieleza kuwa, shirika linatekeleza miradi 12 ya uwekezaji ukiwemo mradi wa Samia Housing Scheme ambao utajengwa nyumba 5000 kwa gharama ya shilingi bilioni 466.
Meneja wa mradi wa Iyumbu Msanifu Majengo, Frank Mambo akimkaribisha Mwenyekiti wa Bodi Dkt. Sophia Kongela eneo la tukio.

Aidha, Dkt.Kongela kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi ya NHC ameialika kamati hiyo kutembelea miradi mingine mbalimbali inayotekelezwa na shirika jijini Dar es Salaam ukiwemo mradi wa Morocco Square.

Wakati huo huo, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Bw.Hamad Abdallah akiuelezea mradi huo alisema kuwa, shirika linatarajia kupata faida ya shilingi bilioni 3.8 kutokana na mradi wa Iyumbu na kwamba mradi huo umeweza kuzalisha ajira mbalimbali zikiwemo za wahandisi, mafundi wa kawaida, vibarua wa kawaida, baba na mama lishe wakiwemo watunza stoo.

Aidha, amezungumzia mauzo katika mradi huo ambapo mpaka sasa nyumba 163 zimeuzwa ambazo ni sawa na asilimia 54 ambapo kati ya hizo nyumba 108 zimeshalipiwa na nyumba 55 ziko kwenye hatua mbalimbali za malipo. 

Pamoja na faida iliyotarajiwa kupatikana, Bw. Abdallah amezungumzia pia changamoto mbalimbali walizokabiliana nazo katika kutekeleza mradi huo.

“Kupanda kwa gharama ya vifaa vya ujenzi hususani chuma wakati wa kipindi cha UVIKO-19 na vita ya Ukraine na Urusi kumesababisha mradi huu kutokamilika kwa wakati ambapo tulitarajia kuukamilisha katika kipindi cha miezi 18,”amesema Bw. Abdallah.

Mkurugenzi Mkuu amebainisha changamoto nyingine kuwa ni baadhi ya wauzaji wa vifaa kutokuwa na uwezo wa kuuza vitu vingi zaidi kwa wakati mmoja.

Hata hivyo, Bw. Abdallah amesema kuwa, shirika liko mbioni kukamilisha mradi huo kwani kazi zilizobaki ni chache. 
Muonekano wa baadhi ya nyumba za makazi zilizopo eneo la Iyumbu jijini Dodoma.

Kabla ya kuhitimisha kikao hicho, Mwenyekiti wa PIC alitoa maagizo ya kamati kwa shirika ambayo ni kuhakikisha NHC inakuwa na mpango madhubuti wa mauzo na masoko (pre sale), kuhakikishia NHC inapitia upya mpango wa mauzo kwenye mradi hasa kipengele cha kulipia asilimia 10 kama malipo ya awali kwa watumishi wa umma na kuhakikisha NHC inaweka mpango mkakati kuratibu upatikanaji wa miundombinu kama vile barabara, maji na umeme kabla ya kuanza kwa mradi husika. 

Maazimio mengine ni kuhakikisha NHC inafanya utafiti wa soko la nyumba katika mikoa mbalimbali ili kuongeza wigo wa huduma inazotoa hatua itakayosaidia kuhudumia wananchi wengi zaidi na kuongeza mapato kwa shirika. 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news