KAONDOKA NA MPIRA, NA MBUZI ALIYENONA

NA LWAGA MWAMBANDE

MIONGONI mwa mashabiki kindakindaki wa kiungo mshambuliaji Clatous Chama wa Klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam, amempa mshambuliaji huyo zawadi ya mbuzi aliyenona.

Zawadi hiyo imetolewa Machi 18, 2023 dakika chache baada ya Simba SC kuibamiza Horoya kutoka nchini Gunea mabao 7-0 huku Chama akipiga hat trick.

"Chama kwa heshima yangu, niliahidi lile goli dhidi ya Vipers, nitakuletea mbuzi na huyu hapa nimemuleta,yaani ninapoongea hapa mama yangu yupo frijini, alikufa Alhamisi, na msiba upo nyumbani, lakini kwa sababu wewe ni kipenzi cha familia,nimemuomba baba, ninaomba nimpelekee Chama zawadi,nimeota Chama utafanya mazuri zaidi, na kweli umefanya mazuri zaidi.

"Hata nikienda kumwambia baba ni kweli mazuri yamefanyika. Zawadi yangu juu yako ni hii. Nakuomba kwa heshima yako nikukabidhi zawadi hii na Jumatatu ninamsafirisha mama yangu kwenda kumzika Musoma (Mkoa wa Mara)," amesema shabiki huyo mkazi wa Kigamboni jijini Dar es Salaam.

... "Kwanza pole sana kwa msiba,na Mungu akupe nguvu, Mungu akusaidie, kingine naomba niongezee kusema ninashukuru sana kwa mapenzi na kwa zawadi uliyonipa, ninakuombea Mungu akubariki na wewe,"amebainisha Chama.

Kupitia matokeo hayo yaliyotokana na mtanage uliopigwa katika Dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam, Simba SC imefanikiwa kutinga robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika.
 
Chama aliwapatia Simba bao la kwanza dakika ya 10 kwa shuti kali la mpira wa adhabu nje ya 18 baada ya Jean Baleke kufanyiwa madhambi.

Naye Baleke aliwapatia Simba SC bao la pili dakika ya 32 baada ya shuti kali lililopigwa na Kibu Denis kupanguliwa na mlinda mlango wa Horoya kabla ya kumkuta mfungaji.

Chama aliwapatia Simba SC bao la tatu kwa mkwaju wa penati dakika ya 36 baada ya mlinzi wa Horoya Abdoulaye Camara kuunawa mpira ndani ya 18.

Kipindi cha pili,Simba SC walirudi kwa kasi ambapo dakika ya 53 Kiungo Sadio Kanoute aliwapatia bao la nne akipokea pasi ya upendo kutoka kwa Chama.

Baleke aliongeza bao la tano dakika ya 65 kufuatia Chama kumpoka mpira mchezaji wa Horoya kabla ya kumkuta mfungaji ambaye alimchambua mlinda mlango.

Pia, Chama aliwapatia bao la sita dakika 70 na kukamilisha hat trick yake baada ya kumlamba chenga mlinzi wa Horoya ndani ya 18 akimalizia pasi safi kutoka kwa Pape Sakho.

Wakati huo huo, Kanoute alipigilia msumari wa moto wa saba kwa shuti kali nje ya 18 dakika ya 86 akimalizia pasi ya upendo kutoka Shomari Kapombe. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, kila penye bidii na matokeo bora, licha ya wengi kupata furaha, pia mwenye kufanya mema huwa anatunukiwa zawada, hivyo Chama anastahili. Endelea;


1.Juzi limwandika Chama, leo namwandika Chama,
Kwa vile jamaa Chama, jinsi anafanya vyema,
Atufurahisha Chama, anatushindisha Chama,
Kaondoka na mpira, na mbuzi aliyenona.

2. Mchezaji bora Chama, ilopita wiki nzima,
Jinsi alicheza vema, Vipers kuwalima,
Mengi tulisemasema, na leo pia twasema,
Kaondoka na mpira, na mbuzi aliyenona.

3. Leo kazidisha Chama, magoli matatu Chama,
Lingine kapika chama, ushindi kwa timu nzima,
Nadhani takuwa vema, ubora apewe Chama,
Kaondoka na mpira, na mbuzi aliyenona.

4. Mchezaji bora Chama, hanao mfano Chama,
Simba tunaimba Chama, Zambia waimba Chama,
CAF nanyi imba Chama, jinsi anafanya vema,
Kaondoka na mpira, na mbuzi aliyenona.

5. Alompa mbuzi Chama, kwa kweli kafanya vema,
Mpenzi mtu mzima, ana msiba wa mama,
Kamwacha mochwari Mama, kwa kumtunuku Chama,
Kaondoka na mpira, na mbuzi aliyenona.

6. Kwa kumpoteza mama, pole familia nzima,
Zawadi yako kwa Chama, msiba kuweka nyuma,
Huo ni utu uzima, kwa kazi nzuri ya Chama,
Kaondoka na mpira, na mbuzi aliyenona.

7. Hongera za kwako Chama, pamoja na timu nzima,
Leo mmefanya vema, furaha kwa nchi nzima,
Mwaenda hatua njema, timu zije zitakoma,
Kaondoka na mpira, na mbuzi aliyenona.

8. Kanoute Baleke Chama, leo mmefanya vema,
Ntiba na pasi kwa Chama, kuna watu yawauma,
Pape Sacho mesimama, sambamba na huyo Chama,
Kaondoka na mpira, na mbuzi aliyenona.

9. Manula golini vema, bila kufungwa ni vema,
Jinsi unavyosimama, sifa zako tutasema,
Mo’d Zimbwe watakoma, kwa jinsi ulivyo noma,
Kaondoka na mpira, na mbuzi aliyenona.

10. Kapombe umesimama, goli unalinda vema,
Onyango mtu mzima, kazi yako twaisoma,
Inonga zidi kusema, fimbo chapa watakoma,
Kaondoka na mpira, na mbuzi aliyenona.

11. Mzamiru kwake Chama, na Phiri amesimama,
Kibu Denis twasema, wakome kusemasema,
Mmewakilisha vema, Afrika inatusema,
Kaondoka na mpira, na mbuzi aliyenona.

12. Benchi la ufundi zima, twawapongeza mazima,
Simba Yazidi kuvuma, pia Tanzania nzima,
CAF huko watusema, Horoya wameshazama,
Kaondoka na mpira, na mbuzi aliyenona.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news