Mabasi ya Classic Coach kutangaza filamu ya The Royal Tour nchini DRC bila malipo

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax ameipongeza na kuishukuru kampuni ya Mabasi ya Classic Coach kwa uamuzi wake wa kizalendo wa kukubali kuonesha filamu ya The Royal Tour iliyotafsiriwa kwa lugha ya Kifaransa katika mabasi yake yanayofanya shughuli za kusafirisha abiria nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) akitoa maelezo mafupi kwa wageni (hawapo pchani) walioshiriki hafla ya uzinduzi wa kuonesha filamu ya the Royal Tour katika mabasi ya kampuni ya Classic Coach. Wengine katika picha, watatu kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini DRC, Mhe. Said Mshana na watatu kulia ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga.

Pongezi hizo amezitoa wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa uoneshaji wa filamu hiyo kwenye mabasi hayo iliyofanyika jijini Kinshasa kwenye viwanja vya ubalozi wa Tanzania nchini humo tarehe 17 Machi 2023 na kuhudhuriwa na wageni mbalimbali wakiwemo maafisa wa Ubalozi wa Tanzania na wawakilishi wa kampuni hiyo.

Mhe. Dkt. Tax amempongeza Balozi wa Tanzania nchini DRC, Mhe. Said Mshana na timu yake kwa kufanikisha jambo hilo muhimu na la kupigiwa mfano.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) akibofya batani ili kucheza filamu ya The Royal Tour kwenye Basi la abiria la Kampuni ya Classic ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa kampuni hiyo kuonesha filamu hiyo kwa abiria wanaotumia mabasi yake.

Amesema Balozi Mshana ana mwaka mmoja tangu ateuliwe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kushika wadhifa huo, lakini katika kipindi hicho kifupi amefanikisha mambo mengi makubwa na muhimu, likiwemo hilo la kuishawishi kampuni ya Classic yenye mabasi 50 inayotoa huduma ya usafiri wa abiria katika miji mbalimbali ya DRC, ikiwemo ya Kinshasa na Lubumbashi, kutangaza filamu ya the Royal Tour bila malipo. 
Ameongeza kuwa, mabasi ya kampuni hiyo inayomilikiwa na Mtanzania, Bw. Amir Abdallah anayeishi Lubumbashi, DRC hayatumiwi na Wakongo pekee, bali yanatumiwa pia na raia wa nchi nyingine, hivyo ni fursa nzuri ya kutangaza Tanzania na fursa za uwekezaji, biashara pamoja na utalii ili kutimiza azma ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya kuvutia watalii milioni 5 na mapato ya Dola za Marekani bilioni 6 ifikapo mwaka 2025.

Waziri Tax ametoa wito kwa makampuni mengine na sekta binafsi kwa ujumla zijitokeze kushirikiana na Serikali katika jitihada za kukuza uchumi ikiwa ni pamoja na kuchangamkia fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini Tanzania.
Baadhi ya wageni walioshiriki hafla ya uzinduzi wakiwa kwenye moja ya basi litakalotumika kuoneha filamu ya the Royal Tour.

Waziri Tax alihitimisha hotuba yake kwa kueleza kuwa hafla hiyo ya uzinduzi ni sehemu ya kusherehekea miaka miwili ya Rais Samia Suluhu Hassan tokea aapishwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Machi 2021 ambapo mafanikio mengi yamepatikana katika kipindi hicho cha uongozi wake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news