Waziri Dkt.Mabula atoa maagizo muhimu kwa wakuu wote wa wilaya nchini

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angelina Mabula amewataka Wakuu wa Wilaya nchini kuhakikisha kila halmashauri inakuwa na rejista ya migogoro ya ardhi ili kujua chanzo chake pamoja na mikakati ya utatuzi wa migogoro hiyo kila inapojitokeza.
Sehemu ya Wakuu Wilaya wakifuatilia mada iliyotolewa kwao na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Dkt. Angeline Mabula jijini Dodoma.

‘’Natambua kuwa kila Mkuu wa Wilaya anapoteuliwa migogoro ambayo ilishapatiwa ufumbuzi huwa inaanza upya ndio maana nawataka kusimamia uanzishwaji wa rejista ya migogoro ya ardhi itakayosimamiwa na wakurugenzi ili kudhibiti na kumaliza migogoro ya ardhi,"amesema Dkt. Mabula.

Waziri Mabula amesema hayo leo wakati wa uwasiliajishaji wa mada yake kwa wakuu wa Wilaya wanaoshiriki mafunzo yanayoendelea jijini Dodoma chini ya Ofisi ya Rais TAMISEMI.

Katika mada yake hiyo,Dkt. Mabura alisema kumekuwepo na changamoto kwenye halmashauri ya kutodhibitiwa kwa migogoro ya ardhi na kutosimamia mipango ya matumizi ardhi iliyoandaliwa mijini na vijijini.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula akiongea na Wakuu wa Wilaya (hawako pichani) wanaoendelea na mafunzo jijini Dodoma.

Changamoto nyingine aliyoisema Waziri Mabula ni Halmashauri kutoshiriki kikamilifu kwenye mikakati ya makusanyo yanayotokana na sekta ya ardhi pamoja na bajeti ndogo ya kutekeleza majukumu ya sekta na kutokutengwa kwa ardhi ya uwekezaji.

Aidha, Waziri huyo aliwataka viongozi hao wa Wilaya kusaidia katika kuongeza hamasa kwenye suala la ukusanyaji wa mapato ya serikali yanayotokana na sekta ya ardhi ikiwemo kusimamia mikakati ya ukusanyaji maduhuli na kuwakumbusha wananchi kutumia fursa iliyotolewa na Rais ya msamaha wa malimbikizo ya kodi ya pango la ardhi inayoishia tarehe 30 Aprili, 2023.

Waziri Mabula amewataka viongozi hao wa Wilaya kusimamia Halmashauri ili zitenge fedha kwenye Bajeti ili kuhakikisha ardhi inapangwa, kupimwa na kumilikishwa huku akiwahimiza kutambua kuwa mamlaka za upangaji ardhi ziko chini ya Halmashauri.

‘’Halmashauri zitambue kuwa jukumu hilo bado ni lao na wanahitaji kuendelea kushiriki kikamilifu kwenye kutenga fedha ili kutekeleza majukumu yao na kuwawezesha watumishi waliopo katika Halmashauri kufanya kazi kwa mujibu wa taaluma zao,’’aliongea Waziri Mabula.
Baadhi ya Wakuu Wilaya wakifuatilia mada iliyotolewa kwao na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula jijini Dodoma.

Waziri Dkt.Mabula pia amedokeza kuwa kuna baadhi ya halmasahauri nchini ambazo zimetumia mikopo ya shilingi milioni 50 iliyotolewa na Rais kwa baadhi ya halmashauri ili zitumike Kupima, Kupanga na Kumilikisha ardhi, lakini baadhi ya Halmashauri zilielekeza fedha hizo katika matumizi mengine bila kuzingatia kusudio la mikopo hiyo.

Kwa mukutadha huo Waziri Mabula alielekeza Wakuu wa Wilaya kusimamia eneo hili ili wakurugenzi wa halmashauri watumie mikopo hiyo kwa ajili ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi na hatimaye kurejesha fedha hizo ili halmashauri nyingine ziweze kukopeshwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news