Malezi ya watoto yawe kipaumbele cha kwanza-Mama Mariam Mwinyi

NA DIRAMAKINI

MWENYEKITI wa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF) ambaye ni Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Bazaraza la Mapinduzi, Mama Mariam Mwinyi amewaasa wanawake nchini kulipa kipaumbele cha pekee suala la malezi ya watoto licha ya jitihada zao za kujitafutia riziki kwenye harakati zao za maisha.

Amesema, jamii ya wanawake wengi imekubwa na taharuki ya kukimbizana na harakati za uchumi na kujitafutia maisha huku jukumu la ulezi likipewa mgongo hali aliyoieleza inaathiri sana watoto kwenye ustawi wa makuzi yao bila ya uwepo wa mama karibu.
Mama Mariam Mwinyi ameyasema hayo kwenye ufunguzi wa kongamano la Siku ya Wanawake Duniani lililofanyika Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdul Wakil, Kikwajini Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Alisema, mwanamke ana wajibu mkubwa wa ulezi wa familia na jamii katika mipango yake yote anayojipangia lazima atenge muda kwa ajili ya watoto wake.

“Katika mipango yote tunayoipanga lazima tuhakikishe tunalizungumzia suala zima la nafasi ya malezi kwa mwanamke, tunapokimbizana sana na uchumi katika miaka hii ya karibuni pametokea mwanya wa malezi kwa watoto, lazima tutenge muda kwa ajili ya watoto wetu haijaalishi nafasi gani mwanamke yupo kwenye karakati zake, uwe Waziri au Mkurugenzi tuhakikishe watoto tunawapa nguvu na tunawaelekeza,"alisisitiza Mariam Mwinyi.
Alisema, wanawake wako kwenye sekta zote za uchumi, wanafanya kila linalowezekana kwaajili matunzo ya familia zao.

Alisema, katika harakati za kukabiliana na usawa wa kijinsi na kujikwamua kiuchumi kwa hali zote, wanawake wamekuwa wamebanwa na harakati hizo hivyo aliwaeleza kujua wajibu wao wa ulezi kwa watoto wao.

“Tusije tukakimbizana sana hili jambo la malezi tukalisahau sababu mwalimu wa kwanza duniani kwa mtoto ni mama, ni sisi ndio tunaobaki nao majumbani, mama ndie rafiki bora kwa mtoto, mama ni daktari wa kwanza nyumbani, duniani kwa mtoto ni mama, mama ndie anaetoa huruma kwa watoto wake, mtoto akiumia pale unapomwambia pole mwanangu, anapata hisia mama ndio kila kitu kwake, lazima tujichanganye kwenye muda wa kutafuta wakati huo huo ulezi wa familia,”alisisitiza Mama Mariam Mwinyi.
Alisema, kauli mbiu ya Siku ya Wanawake Duniani mwaka 2023 inachanganua na kuwasisitiza wanawake wawe wadadisi, wajasiri, wajasiriamali na wabunifu na wenye kuleta mabadiliko yatakayokabiliana na umaskini, haki, ukosefu wa kipato kwa jamii na taifa kwa ujumla kwa kutumia njia sahihi za teknolojia.

Aidha, Mama Mariam Mwinyi aliwashauri wanawake na kinamama kujitahidi kutumia fursa zinazopatikana kupitia teknolojia ya kisasa kwa kijitangaza kibiashara na kutumia soko la kimtandao kwa ajili ya kutangaza bidhaa na kazi za vikundi vyao ili kupata maendeleo ya haraka.

Pia, aliwashauri wazazi na walezi majumbani kuwashauri na kuwanasihi watoto wapende sana masomo ya sayansi ili kuwajenga mapema kuwa watoto wazuri wa teknolojia ya baadae, kwa kuwaunga mkono na kuwasaidia kwenye masomo ya sayansi na hesabati badala ya kuwaachia na kuwa watoto wakawaida.
Alisema, wazazi au walezi wanapaswa kutumia kigezo cha Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kuwa kigezo bora kuzifikia ndoto za watoto wao kwa kuwapa moyo na bidii kwenye masomo yao ili waje wafuate nyayo za Rais Samia.

Alisema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaunga mkono matumizi ya teknolojia kwa kuweka miundombinu bora ya teknolojia kwenye madarasa ya shule za msingi ili kuwajenga mapema watoto kiteknolojia.
Akizungumzia umuhimu wa bima, Mama Mariam Mwinyi aliitaka jamii kuona umuhimu wa kukata bima kwa ajili ya kujikinga na majanga. 

Aidha, aliwataka Mamala ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kuongeza bidii ya kutoa miongozo na elimu kwa umma juu ya umuhimu wa kuwa na BIMA nchini.

Akizungumza kwenye hafla hiyo kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Uchumi, Dkt.Sada Mkuya Salum, Naibu wa Wizara hiyo, Ali Suleiman Mrembo alisema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania zinadhamira njema kuhakikisha usawa wa kijinsia unakwenda sambamba kwenye kuleta maendeleo ya Watanania wote.
Alieleza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imeelekeza mipango na sheria, miongozo na taratibu zake kuona usawa wa jinsia kwenye teknolojia unakuwa chachu ya ukombozi wa wanawake.

Naye, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Watoto, Ana Anatasi Paul, aliwashauri wanawake kupitia vikundi vya wajasiriamali na kinama kuitumia teknolojia kwa kujitangaza na kujitoa kiuchumi. 

Alisema, wanawake walio wengi bado wako nyuma na matumizi ya tenkolojia, aliwashauri kuitumia fursa hiyo kujikwamua kiuchumi na kutangaza biashara zao na kulitumia vyema soko la teknolojia.
Kwa upande wake, Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Khadija Issa alisema mafanikio ya shirika hilo yalichangiwa na ubunifu wa elimu jumuishi pamoja na njia za kisasa za usambazaji wa bima aidha, alieleza malengo ya mamlaka hiyo kwa kushirikiana na wadau wake ikiwemo kutoa elimu kwa umma, kunzisha na kutekeleza mpango wa bima ya kilimo, uimarishaji na uunganishaji wa mifumo ya taasisi mbalimbali za serikali zikiwemo jeshi la polisi mamlaka za bandari, mamlaka zote za mapato nchini.

Pia, aliiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuipa ushirikiano mamlaka hiyo kwenye kutekeleza malengo yake hayo.Kongamano hilo la Siku ya Wanawake Duniani lilitayarishwa na Mamkala ya Usimamizi wa Bima Tanzania, (TIRA).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news