MIAKA MIWILI YA UONGOZI WA RAIS DKT.SAMIA WANANCHI WA KASULU WASEMA WAMEMUELEWA

NA RESPICE SWETU

IKIWA imetimia miaka miwili tangu Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. Samia Suluhu Hassan aingie madarakani, wakazi wa Hamashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma wamevutiwa na maendeleo makubwa yaliyofanyika katika kipindi cha uongozi wake.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kutoka katika maeneo mbalimbali ya halmashauri hiyo wamesema kuwa, katika kipindi hicho, halmashauri ya wilaya ya Kasulu imepiga hatua kubwa kwenye nyanja nyingi za maendeleo ikilinganishwa na ilikotoka.

Miongoni mwa maendeleo yaliyotajwa kupatikana kwenye kipindi cha uongozi Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ni katika sekta ya afya, elimu, kilimo, barabara, maji na utawala bora.

Akielezea mafanikio yaliyopatikana katika kata ya Kitanga, Diwani wa kata hiyo Eliyah Kagoma amesema katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, kata ya Kitanga imenufaika kwa kiasi kikubwa kutokana na miradi ya maendeleo iliyotekelezwa kwenye eneo hilo.

Kagoma ambaye pia ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu ameitaja baadhi ya miradi iliyotekelezwa kwenye kata hiyo kuwa ni ujenzi wa kituo kipya cha afya, ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari na mradi wa barabara.

Kagoma ameutaja pia mradi wa maji uliojengwa kwenye kata hiyo katika kipindi cha miaka miwili ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan kuwa miongoni mwa miradi mikubwa ya halmashauri hiyo.

"Mradi huo wa maji ni mradi mkubwa na umegharimu zaidi ya shilingi bilioni moja, unatoa maji kwenye chanzo cha mto Malagarasi kwa kutumia umeme wa Sola na kuyasambaza kwenye matanki hadi kwa wananchi, wakazi wa kata ya Kitanga wameshaanza kunufaika na maji ya mradi huo," amesema Kagoma.

Akizungumzia halmashauri ya wilaya ya Kasulu, mwenyekiti wa halmashauri hiyo amesema pia kuwa katika kipindi cha miaka miwili, halmashauri yake imepokea mabilioni ya fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi.

Ameitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na ujenzi wa makao makuu ya halmashauri, hospitali ya wilaya, zahanati, shule na upanuzi wa vituo vya afya. 

"Sio hivyo tu, miaka miwili ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa wananchi wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu imekuwa yenye neema kubwa kutokana na hatua mbalimbali za maendeleo zilizofikiwa kwa lengo la kuwasogezea huduma wananchi,"amesema.

Miongoni mwa huduma hizo ambazo ni "tunda" la miaka miwili ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ni pamoja na ujenzi wa maghala ya kuhifadhia nafaka sambamba na soko la wakulima linalojengwa kwenye "mji mpya" jirani na makao makuu ya halmashauri hiyo.

Kana kwamba haitoshi, kwa mara ya kwanza katika historia ya elimu kwenye halmashauri ya wilaya ya Kasulu, kumekuwepo na ziada ya vyumba vya madarasa ya Shule za sekondari.

Taarifa iliyowasilishwa na afisaelimu sekondari wa halmashauri hiyo Bahati Onesmo kwenye kikao cha wadau wa elimu kilichofanyika mapema mwaka huu, ilionesha kuwa, halmashauri ya wilaya ya Kasulu yenye shule 25 za sekondari, ina mahitaji ya vyumba 287 vya madarasa huku ikiwa na vyumba 331.

Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka miwili ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan, James Mlazi mkazi wa kijiji cha Mvugwe, amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyoifanya katika ujenzi wa vyumba vya madarasa kwenye halmashauri hiyo.
"Sasa ni tofauti na zamani tulipokuwa tunakimbizana na watendaji kujenga madarasa ya wanafunzi wa kidato cha kwanza, imekwisha hiyo, tukihitajika kuchangia tunaandaa benki ya matofali na vifaa vingine kusaidiana na serikali", amesema.

Kwa upande wake, kaimu afisa elimu awali na msingi wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu Joseph Maiga ameyataja mafanikio makubwa kwenye kipindi hicho kuwa ni pamoja na kuanzishwa kwa shule mpya za msingi.

Maiga amezitaja shule hizo kuwa ni Kazage, Kagege, Kwilibha, Rugufu Relini, Kacheli, Mkuyuni na Kumtundu.

Mafanikio mengine katika sekta hiyo kwa kipindi cha miaka miwili ni pamoja na ongezeko la wanafunzi lililochagizwa na maamuzi adhimu ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kufuta ada na michango mbalimbali iliyokuwa ikitozwa.
Aidha, kufuatia kufutwa kwa michango hiyo, serikali ya awamu ya sita ilitoa waraka unaotumika pindi shule inapohitaji msaada kutoka kwa wazazi na wadau wengine bila kuathiri ujifunzaji kama ilivyokuwa awali.

Naye mtumishi wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu ambaye hakutaka kutajwa jina lake, ameishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuonesha mfano wa utawala bora. 

"Amini usiamini mwandishi wa habari, kama sio utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan sijui ingejuwaje, namshukurua sana "mama" alipoingia madarakani nikapandishwa daraja na kuongezwa mshahara baada ya miaka kumi kupita, nani kama mama?,"alisema mtumishi huyo huku akiuliza swali hilo.
Mafanikio mengine ya kupigiwa mfano yaliyotokea katika kipindi hicho, ni katika sekta ya kilimo ambako katika hali isiyotarajiwa serikali imetoa mbolea kwa gharama nafuu. Mbolea hiyo ya ruzuku, imewafikia wakulima na kuwajaza matumaini katika msimu huu.

Kutokana na hali hiyo,wakulima katika halmashauri ya wilaya ya Kasulu wanatarajia kupata mavuno ya kutosha kutokana na kuwepo kwa matumizi ya mbolea hiyo.

Mengi yamefanyika katika kipindi cha miaka miwili ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye halmashauri ya wilaya ya Kasulu, itoshe tu kusema kuwa kwa hakika mama, ameupiga mwingi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news