WANANCHI WA TABORA WAISHUKURU SERIKALI KWA KUWASOGEZEA HUDUMA ZA KIBINGWA

NA CATHERINE SUNGURA-WAF

WAKAZI wa Tabora na viunga vyake wameishukuru Serikali kupitia Wizara ya afya kwa kuwasogezea huduma za Kibingwa na Ubingwa Bobezi kwenye hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Tabora-Kitete na hivyo kuwapunguzia gharama za matibabu endapo wangepata rufaa ya kuzifuata huduma hizo nje ya mkoa huo na ukizingatia wengine ni wazee na hali zao za maisha ni ngumu.
Daktari wa Masikio,Pua na Koo Dkt. Proscovia Mugyabuso kutoka Muhimbili-Mloganzila akimfanyia uchunguzi wa masikio mmoka wa watoto waliofika kupatiwa huduma za kibingwa katika kambi hiyo.

Wakiongea kwa wakati tofauti, Wakazi hao ambao wamefika kupatiwa matibabu ya kibingwa ambazo zimeanza kutolewa jana kwa muda wa siku tano(5) na Madaktari Bingwa wapatao 21 kutoka hospitali za rufaa za mikoa ya Dare es Salaam, Pwani na Dodoma kwa fani mbalimbali.

Bw. Daud Thelathini ambaye ni Mkazi wa Kata ya Kitete ambaye alifika jana na kuonana na madaktari hao na kufanya baadhi ya vipimo na hivyo anasubiri upasuaji amesema, anashukuru kwa ujio wa madaktari hao bingwa na ameridhika na huduma zao na ushauri wao. 
Mkazi wa Tabora Bw. Daud Thelathini akiwa ni mmoja wa wagonjwa waliopata matibabu siku ya kwanza ya kuanza kwa huduma za kibingwa na bobezi katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Tabora-Kitete na ameishukuru Serikali kwa huduma hiyo.

“Nashukuru sana madaktari wanakusikiliza vizuri na wanakupa ushauri kama tunavyojua ugonjwa hauna hodi na unaweza kuupata wakati wowote, kwa matatizo yetu wengine tungepata rufaa kwenda nje ya mkoa ingekua tabu kwani lazima ungegharamika hivyo kwa ujio huu nimeweza kupata huduma hizo hapahapa,"amesema Bw. Thelathini

Hata hivyo, amesema huduma ya kumuona daktari bingwa ni bure na vipimo unachangia kidogo tofauti na huduma zinazotolewa siku za kawaida kwahiyo hata kama mtu ana uwezo mdogo inamrahisishia kupata huduma za kibingwa bila shida. 

“Nampongeza Rais Dkt. Samia Suluhu kwa uongozi wake na usimamizi kwa huduma za afya kwani hivi sasa hospitali yetu ina majengo mazuri, tunaomba huduma hizi zingetolewa mara mbili kwa mwaka ili wnanchi wengi zaidi wasaidike."

Naye, Mwalimu Thea Temba Mkazi wa Urambo amesema anaishukuru Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu kwa juhudi zake za kusogeza huduma za afya karibu na wananchi pamoja na kuboresha huduma hizo katika hospitali ya rufaa ya Kitete.
Baadhi ya wananchi wa Tabora wakisubiri matibabu kutoka kwa madaktari bingwa ambao wameweka kambi ya siku tano katika hospitali ya rufaa ya Kitete.

“Tunashukuru Mungu kwani wengine tumeshatibiwa,nilikuwa nasumbuliwa na masikio nimeonana na madaktari bingwa hili ni jambo zuri nashukuru kwani kwa miaka minne sijaja kutibiwa hapa, unapopata huduma za madaktari bingwa unashukuru , sasa hivi magonjwa ni mengi sana, tunaomba waendelee kuja mara kwa mara ili kila mwananchi hasa wanaotoka vijijini wafike kupatiwa huduma hizi,"amesema Mwalimu Thea Temba.

Bw. John Witson, Mkazi wa Igunga ameipongeza Serikali kwa kuwasogezea huduma hizo na kuomba huduma kama hizo zisogezwe nchi nzima ili kila mwananchi aweze kutibiwa na madakatri bingwa.

“Serikali iendelee na mfumo huu wa kutusogelea ili kila mwananchi apate huduma hizo karibu na makazi yeke kwani kuzifuata huduma nje ya mkoa ilikua ikitugharimu sana, nampongeza kwakweli Rais wetu Dkt. Samia Suluhu kwa maboresho ya huduma za afya nchini.
Baadhi ya wakazi kutoka maeneo mbalimbali ya Tabora na viunga vyake wakisubiri huduma za kibingwa.

Wakati huo huo Mratibu wa Huduma za hospitali ya Rufaa ya Mkoa-Kitete Dkt. Nassib Msuya amesema kambi hiyo ya madaktari bingwa na bobezi inaendela vizuri na toka jana takribani wagonjwa 600 wameonwa na madaktari hao na wanatarajia kuanza huduma za upasuaji wa wagonjwa wanaotakiwa huduma hiyo.

Dkt. Msuya amesema kutopatikana kwa baadhi ya huduma za kibingwa na bobezi kwa baadhi ya fani hivyo wamekuwa inawaradhimu kuwapatia rufaa wagonjwa wao kwenda kutibiwa nje ya mkoa hivyo ujio wa madaktari hao itawasaidia wananchi wengi ambao wengine walikuwa wanashindwa kusafiri kutokana na changamoto za kifedha.

“Tunamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maboresho ya huduma za afya kwani kwa ujio huu wagonjwa wetu wanapata huduma zote za vipimo hapa hapa.”

Amesema kuwa hata madakatari hao wakiondoka huduma nyingine zitaendelea kutolewa kwani madakari wapo pia wanajengewa uwezo wa kuweza kutoa huduma hizo kwenye hospitali hiyo. 
Mkazi wa Igunga Bw. John Witson ameishukuru Serikali kwa kuwasogezea huduma za kibingwa na kuiomba huduma kama hizo zisogezwe nchi nzima.

Huduma za matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Tabora-Kitete inatarajia kuwaona wagonjwa zaidi ya elfu tatu na zimeanza kutolewa tarehe 13 hadi 17 mwezi huu kwa ufadhili wa kampuni ya Master Card na imewajumuisha madakarri bingwa na bobezi kutoka hospitali za rufaa za Mkoa wa Dar es Salaam, Pwani na Dodoma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news