MIWILI YAKE SAMIA-2:Kwa ustawi bora wa Taifa

NA LWAGA MWAMBANDE

APRILI 22, 2021 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu ikiwa ni siku chache baada ya kuapishwa aliudhirishia umma wa Watanzania na Dunia kuwa,Serikali ya Awamu ya Sita itadumisha umoja, mshikamano, upendo na kuendelea kustawisha demokrasia nchini.

Ni kupitia hotuba aliyoitoa bungeni akielezea mwelekeo wa Serikali yake ndani ya Bunge kuhusu nia yake ya kutaka kukutana na kuzungumza na vyama vya upinzani nchini.

Ikiwa leo Machi 19, 2023 Mheshimiwa Rais Dkt.Samia anaadhimisha miaka miwili ya uongozi wake madarakani,yale yote aliyoyasema wakati huo Watanzania na Dunia imeshuhudia akiyatekeleza kwa vitendo hatua kwa hatua.
Kwani, awali Mheshimiwa Rais Dkt.Samia alikutana na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe na walizungumza mambo kadhaa ya kujenga siasa zenye ushindani wa hoja na uwanja sawa wa siasa nchini.

“Kitu kikubwa tulichojadiliana ni kuwa, Tanzania ni yetu sote na tunapaswa kufanya kazi pamoja, kuijenga, lakini hili linawezekana tu iwapo tutajenga uaminifu na kudai haki, pamoja na kuheshimiana. Hii itatusaidia kupata nafasi ya kuijenga nchi yetu,” ilikuwa ni kauli ya Rais Samia baada ya mazungumzo yake na Mbowe.

...“Tumekubaliana kuwa, njia nzuri ya kuwa na maridhiano ni wakati kuna haki. Tumepitia madhila mengi, hakuna haja ya kuyarudisha mara kwa mara, badala yake tunapaswa kusonga mbele na kuwa na siasa safi na kuiunga mkono Serikali, na tunatumai kuwa itatuunga mkono kwenye shughuli zetu ili kila mtu afurahi,"alibainisha Mheshimiwa Mbowe wakati huo.

Aidha, mbali na kukutana na Mbowe, Rais Dkt.Samia akiwa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali walikutana na viongozi wa CHADEMA wakiwemo baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu na Sekretarieti ya chama hicho.

Katika kikao hicho, miongoni mwa mambo waliyojadiliana ni maridhiano katika uwanja wa siasa, ikiwemo hoja ya Katiba mpya na kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi.

Vile vile, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ndani ya miaka miwili alikutana na viongozi wa chama cha ACT-Wazalendo katika mwendelezo wake wa kukutana na viongozi wa vyama vya siasa kama alivyoahidi kwenye hotuba yake bungeni.

Ndani ya miaka miwili pia, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia alihutubia mkutano wa wadau wa kujadili hali ya demokrasia ya vyama vingi nchini na baada ya mkutano huo aliunda kikosi cha kujadili mapendekezo ya wadau wa siasa yatakayofanyiwa kazi na Serikali.

Kikosi kazi hicho kilifanya kazi yake na kukabidhi ripoti kwa Rais Dkt.Samia, aliyetoa kauli iliyoonyesha matamanio yake kuona Tanzania inaendelea kuwa moja na salama bila kuwa na kundi litakalohisi kuachwa nyuma katika safari ya kufurahia demokrasia ya kweli.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema, ndani ya miaka miwili ya uongozi wa Rais Dkt.Samia mafanikio ni mengi, na Mheshimiwa Rais Dkt.Samia kuna maeneo amefanya zaidi ya ahadi zake kwa manufaa, maslahi na ustawi bora wa Taifa. Endelea;


21.Pazuri ulianzia,
Kote ulikopitia,
Wapinzani kukujia,
Heko Rais Samia.

22. Wawili walifulia,
Nje ndani Tanzania,
Ulivyowafwatilia,
Heko Rais Samia.

23.Hali uliangalia,
Wala hukufurahia,
Kitu ulitufanyia,
Heko Rais Samia.

24.Mbowe walimfungia,
Kesi ikimtishia,
Wote tuliangalia,
Heko Rais Samia.

25.Wala hukuingilia,
Kesi ilivyoishia,
Lakini tunajulia,
Heko Rais Samia.

26.Vile ulimfanyia,
Ikulu akaingia,
Kuja kukusalimia!
Heko Rais Samia.

27. Wale tuliangalia,
Somo lilituingia,
Unachotaka Samia,
Heko Rais Samia.

28. Sasa nyoyo zatulia,
Vile twakuangalia,
Mtaji mejipatia,
Heko Rais Samia.

29.Na hapo hukuishia,
Hata nje Tanzania,
Watu uliwafikia,
Heko Rais Samia.

Tundu Lissu nakwambia,
Nchi aliikimbia,
Sababu twazijulia,
Heko Rais Samia.

30.Ona sasa Tanzania,
Wakimbizi waingia,
Nyumbani wakurudia,
Heko Rais Samia.

31. Yale yaliwatishia,
Mbali kuwafukuzia,
Sasa yameshaishia,
Asante Mama Samia.

32.Watu tunaangalia,
Ufanyayo yaingia,
Na kweli twafurahia,
Heko Rais Samia.

33.Livyokuwa Tanzania,
Ile kimbiakimbia,
Kusaka kujifichia,
Heko Rais Samia.

34.Nchi imeshatulia,
Yetu tunajifanyia,
Hata na siasa pia,
Heko Rais Samia.

35.Sasa tunaangalia,
Huru kujikutania,
Sera kututangazia,
Heko Rais Samia.

36.Jambo kubwa nakwambia,
Uhuru wa kuchangia,
Midomo kufungulia,
Heko Rais Samia.

37.Mbele yetu Tanzania,
Mengi tunatazamia,
Maisha kufurahia,
Heko Rais Samia.

38.Kuzingatia sheria,
Hilo umetuusia,
Tusije jitifulia,
Heko Rais Samia.

39.Sote ni Watanzania,
Nchi yetu Tanzania,
Tufanye Kitanzania,
Heko Rais Samia.

40.Haki wapenda Samia,
Tena wasisitizia,
Tuinuke Tanzania,
Heko Rais Samia.

41.Hata Neno latwambia,
Haki kama yatimia,
Tainua Tanzania,
Heko Rais Samia.

42.Kuonewa Tanzania,
Hutaki kukusikia,
Tena hutavumilia,
Heko Rais Samia.

43. Kesi za kusingizia,
Makosa bambikizia,
Hutaki kuyasikia,
Heko Rais Samia.

44.Tume umetuundia,
Haki kuishindilia,
Hili tunafurahia,
Heko Rais Samia.

45. Wende kutuchunguzia,
Mabaya kuyafagia,
Haki iweze rudia,
Heko Rais Samia.

46.Mahakama tapitia,
Polisi watapitia,
Hata Magereza pia,
Heko Rais Samia.

47.Tunapenda kufikia,
Pale tutafurahia,
Ni haki mtawalia,
Heko Rais Samia.

48.Mbele tukiangalia,
Miaka nayotujia,
Mema yatatuzidia,
Heko Rais Samia.

49.Haki ikishamiria,
Yote tunajifanyia,
Amani itazidia,
Heko Rais Samia.

50.Uonevu taishia,
Hapa kwetu Tanzania,
Utu tutazingatia,
Heko Rais Samia.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news