MIWILI YAKE SAMIA-1:Na mwanga ukaingia

NA LWAGA MWAMBANDE

MACHI 19, 2021 Samia Suluhu Hassan aliapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jaji Ibrahim Juma katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na marais wastaafu wa Tanzania na Zanzibar.

Mara baada ya kuapishwa alipigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride maalumu kwa mara ya kwanza akiwa kama Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Samia ambaye wakati huo alikuwa na miaka 61, ndiye mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wa pili Afrika Mashariki.

Slyvie Kiningi ndiye alikuwa rais wa pekee mwanamke aliyeshika wadhifa wa urais Afrika Mashariki nchini Burundi kati ya Novemba 1993 hadi Februari 5,1994.

Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye anafikisha miaka miwili ya uongozi wake Machi 19,mwaka huu aliapishwa kushika wadhifa huo kufuatia kifo cha Rais wa Awamu ya Tano, Dkt.John Pombe Joseph Magufuli kilichotokea Jumatano, Machi 17, 2021 wakati akiendelea na matibabu jijini Dar es Salaam.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema, ndani ya miaka miwili ya uongozi wa Rais Dkt.Samia, mambo mengi na makubwa yamefanyika. Endelea;


1.Miwili yake Samia,
Sasa imeshatimia,
Ndiyo tunafurahia,
Heko Rais Samia.

2.Hapa tulipofikia,
Mama twamshangilia,
Anatuthibitishia,
Heko Rais Samia.

3.Wale walifikiria,
Mwendo wake tafifia,
Vichwa wajiinamia,
Heko Rais Samia.

4.Pale ulipoanzia,
Hujabaki kusalia,
Mbele unakimbilia,
Heko Rais Samia.

5.Mengi umetufanyia,
Rais twajivunia,
Machache twakumbushia,
Heko Rais Samia.

6.ARA nne za Samia,
Hizo tumezisikia,
Kazi unazifanyia,
Heko Rais Samia.

7.Moja vema kuanzia,
Jinsi inavyovutia,
Hamu kweli yatutia,
Heko Rais Samia.

8.Kupatana nakwambia,
Yetu tukiyaridhia,
Yakolea yaingia,
Heko Rais Samia.

9.Kwetu sisi Tanzania,
Nasi ni Watanzania,
Nini cha kushindania?,
Heko Rais Samia.

10.Ni mwanga umeingia,
Na giza limekimbia,
Vema tunajisikia,
Heko Rais Samia.

11.Yule alituwangia,
Mema tukayafukia,
Mwingine kaibukia,
Heko Rais Samia.

12.Ulikwishatuambia,
Rais wa Tanzania,
Haki unafurahia,
Heko Rais Samia.

13. Siasa kujifanyia,
Sheria kuzingatia,
Ruksa ingeingia,
Heko Rais Samia.

14. Kweli tukikumbukia,
Miaka tulopitia,
Tunajisikitikia,
Heko Rais Samia.

15.Wapi ungevisikia,
Vyama vikituambia,
Yale wanapigania?
Heko Rais Samia.

16.Si watu walitulia,
Siasa kujifanyia,
Ni amri liingia,
Heko Rais Samia.

17. Ni ganzi iliingia,
Lazima kukumbatia,
Usijejiamulia,
Heko Rais Samia.

18. Wale walijaribia,
Kiberiti tingishia,
Rungu liliwapitia,
Heko Rais Samia.

19. Samia lipoingia,
Na mwanga ukaingia,
Tukaanza wasikia,
Heko Rais Samia.

20. Na hapo hukutulia,
Kimya kimya kusalia,
Mchakato lianzia,
Heko Rais Samia.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news