Naibu Waziri Gekul aguswa na ufanisi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OWMS)

NA MWANDISHI OWMS

OFISI ya Wakili Mkuu wa Serikali (OWMS) imepongezwa kwa kuendelea kuiwakilisha vyema Serikali katika kusimamia mashauri yaliyofunguliwa dhidi yake katika mahakama na mabaraza ya usuluhishi ndani na nje ya nchi.
Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Boniphace Luhende (wa tatu kulia) akimuonesha vitabu vya mashauri ya usuluhishi Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Pauline Gekul (wa pili kulia) alipotembelea Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujitambulisha. Wa kwanza kulia ni Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Bi. Sarah Mwaipopo na wa kwanza kushoto ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Utafiti na Huduma za Maktaba Kiuye Shemakame.

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul ametoa pongezi hizo leo alipotembelea Makao Makuu ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali jijini Dar es Salaam kwa lengo kujitambulisha na kufahamu namna Ofisi hiyo inavyotekeleza majukumu yake.
Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Boniphace Luhende (wa tatu kulia) akimuonesha vitabu vya mashauri ya usuluhishi Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Pauline Gekul (wa pili kulia) alipotembelea Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujitambulisha. Wa kwanza kulia ni Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Bi. Sarah Mwaipopo na wa kwanza kushoto ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Utafiti na Huduma za Maktaba Kiuye Shemakame.

Mhe. Gekul ameipongeza OWMS kwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kujitolea kwa kuiwakilisha Serikali kwenye mashauri mbalimbali pamoja na kuwa na rasilimali fedha chache na kuwataka kuendelea kuwa wazalendo.

Amesema kuwa Wizara ya Katiba na Sheria ni Wizara muhimu inayogusa wananchi wetu ambao wana haki zao nyingi ambazo wamekuwa wakizitafuta katika maeneo mbalimbali.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul akisisitiza jambo wakati akizungumza na wajumbe wa Menejimenti ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (hawapo pichani) alipotembelea Ofisi hiyo leo jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujitambulisha pamoja na kufahamu inavyotekeleza majukumu yake. Anayemsikiliza ni Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende.

“Nafanya ziara kwenye taasisi zote zilizo chini ya Wizara hii ili nione mwelekeo kwa lengo la kuhakikisha tunafanya kazi kwa kushirikiana na kuwa wawazi ili tumsaidie na kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye nafasi hizi tulizo nazo,“ amesema Gekul.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul (aliyesimama kushoto) akipokea taarifa ya utekelezaji ya nusu Mwaka wa Fedha 2022/23 ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kutoka kwa Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Boniphace Luhende. 

Ameongeza kuwa, Mhe. Rais Dkt. Samia amekuwa akifahamu mahitaji ya wananchi na amekuwa akigusa changamoto zao moja kwa moja kwa kuendeleza miradi mikubwa ya maendeleo, masuala ya afya na elimu ambayo kwa namna moja Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali imekuwa ikihusika nayo.

Akisoma taarifa ya Ofisi Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende, Wakili Mkuu wa Serikali amesema kuwa jukumu kubwa la OWMS ni kuratibu, kusimamia na kuendesha mashauri yanayofunguliwa na Serikali na taasisi zake au dhidi ya Serikali na taasisi zake kwenye mahakama na mabaraza ya utoaji haki ndani na nje ya nchi.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul (aliyesimama kushoto) akipokea taarifa ya utekelezaji ya nusu Mwaka wa Fedha 2022/23 ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kutoka kwa Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Boniphace Luhende. Aliyesimama katikati akishuhudia ni Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Bi. Sarah Mwaipopo baada ya ziara yake kwenye Ofisi hiyo jijini Dar es Salaam.

Dkt. Luhende amesema kuwa OWMS imeendelea kuuiwakilisha Serikali na taasisi zake kwa ufanisi katika mashauri yote ya madai na usuluhishi ambapo hadi kufikia mwezi Februari 2023, OWMS imesajili jumla ya mashauri 6,263 ambapo kati ya hayo mashauri ya madai ni 6,112 na mashauri ya usuluhishi 151 na hivyo kazi hii ya OWMS imeiwezesha Serikali kuepuka gharama kubwa za Mawakili wa kujitegemea.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul (aliyesimama katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende (wa kwanza kulia) na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Bi. Sarah Mwaipopo baada ya kikao chake na Menejimenti ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kilichofanyika jijini Dar es Salaam.

“Tumeendelea kusimamia mashauri hata kwenye taasisi binafsi ambazo Serikali ina hisa mfano Kampuni ya Simu ya Airtel Tanzania na baadhi ya benki,“ amesema Dkt. Luhende.
Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Boniphace Luhende (wa kwanza kulia) akimuonesha Mhe. Pauline Gekul, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria mazingira ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wakati wa ziara ya Naibu Waziri huyo alipotembelea Ofisi hiyo kwa mara ya kwanza tangu ateuliwe kushika nafasi hiyo. Anayefuata ni Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Sarah Mwaipopo.

Dkt. Luhende ameongeza kuwa OWMS imefanikiwa kuongoza na kushiriki katika Timu za Serikali za Majadiliano na kufanikisha kumaliza mashauri na migogoro mbalimbali kwa njia ya majadiliano, usuluhishi na maridhiano nje ya Mahakama.
Mhe. Pauline Gekul akiwasalimia watumishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali mara baada ya kuwasili kwenye Ofisi hiyo jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujitambulisha na kujionea namna inavyotekeleza majukumu yake. Wa kwanza kulia ni Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Boniphace Luhende.

Adha, Dkt. Luhende amesema maeneo ya vipaumbele vya OWMS ni kuendelea kuwajengea uwezo watumishi kwa kutoa mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi ikiwemo mafunzo ya ubobevu katika maeneo mtambuka kama vile ya nishati, gesi, uwekezaji.

Amesema OWMS inaendela kuimarisha mifumo ya kidijitali ikiwa ni sehemu ya kuboresha mfumo wa usimamizi wa mashauri na udhibiti ubora ili kuhakikisha mifumo ya OWMS inaongea na mifumo ya Taasisi nyingine tunazoshirikiana nazo.
Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Bi. Sarah Mwaipopo akizungumza wakati akiwatambulisha wajumbe wa Menejimenti ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa Naibu waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul (hayupo pichani) katika kikao kilichofanyika jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujitambulisha na kufahamu majukumu ya Ofisi hiyo.

Naye Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Sarah Mwaipopo akifafanua kuhusu fedha za miradi ya maendeleo alieleza kuwa katika Mwaka wa Fedha 2023/24, OWMS kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka zina mpango wa pamoja wa kujenga vituo jumuishi kwenye mikoa mbali mbali kwa lengo la kusogeza huduma kwa wananchi na kupunguza gharama za pango ya Ofisi. 
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul (aliyeketi katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe wa Menejimenti ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali baada ya kikao na wajumbe hao kilichofanyika jijini Dar es Salaam alipofanya ziara kwa lengo la kujitambulisha na kujionea namna Ofisi hiyo inavyotekeleza makujumu yake.

Kupitia mpango huo, OWMS inatarajia kujenga Ofisi hizo kwenye mji wa Dodoma na Tabora na tayari imeandaa andiko kwa ajili ya kujenga hoja ya kupata fedha za mradi wa maendeleo za ujenzi wa majengo ya vituo jumuishi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news