MPC yabaini kuimarika kwa sekta ya benki nchini

NA GODFRE NNKO

KAMATI ya Sera ya Fedha (MPC) imebainisha kuwa,sekta ya benki nchini imeendelea kuwa thabiti, yenye kiwango cha kutosha cha mitaji, ukwasi, na yenye kutengeneza faida.

Hayo yamebainishwa leo Machi 14, 2023 na Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tututba kupitia tamko la MPC ambayo ilikutana leo kwa lengo la kutathmini utekelezaji wa sera ya fedha katika miezi Januari na Februari 2023.

Sambamba na mwenendo wa uchumi, na kufanya maamuzi ya mwelekeo wa utekelezaji wa sera ya fedha kwa miezi miwili ijayo.

Gavana Tutuba kupitia taarifa hiyo ya kamati amefafanua kuwa, rasilimali za sekta ya benki na amana nchini katika kipindi hicho ziliendelea kuongezeka kutokana na kuimarika kwa shughuli za kiuchumi,pamoja na ongezeko la matumizi ya huduma za uwakala wa mabenki na huduma za fedha kidijitali.

Aidha, rasilimali za sekta ya benki zimeendelea kuboreshwa, zikiakisiwa na kupungua kwa kiwango cha mikopo chechefu hadi kufikia asilimia 5.85 mwezi Januari 2023, kutoka asilimia 8.42 mwezi Januari 2022;

"Kwa kuzingatia mwenendo na matarajio ya uchumi wa ndani na nje ya nchi, Kamati ya Sera ya Fedha imeridhia Benki Kuu ya Tanzania kuendelea na utekelezaji wa sera ya fedha inayolenga kupunguza kiwango cha ukwasi katika uchumi kwa mwezi Machi na Aprili 2023,"amefafanua Mwenyekiti wa kamati hiyo, Gavana Tutuba.

Kwa mujibu wa kamati hiyo, msimamo huu wa sera ya fedha unalenga kuhakiksha kuwa mfumuko wa bei unabakia ndani ya lengo la asilimia 5.4, na kuendelea kuchochea kuimarika kwa shughuli za uchumi nchini.

"Vilevile, sera hii ya fedha itasaidia kufikiwa kwa malengo yaliyoainishwa kwenye programu ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) chini ya Mpango wa Extended Credit Facility (ECF) kwa mwezi Machi na Juni 2023.

"Aidha, Benki Kuu itaendelea kuweka mazingira ya kisera yatakayowezesha kufikiwa kwa malengo mapana ya kiuchumi ya Serikali, na kufuatilia kwa karibu mwenendo mzima wa vihatarishi mbalimbali vinavyotokana na misukosuko ya kiuchumi duniani, na kuchukua hatua stahiki pale itakapohitajika,"imeongeza sehhemu ya taarifa hiyo ya MPC.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news