MPC yaridhishwa na utekelezaji wa sera ya fedha

NA GODFREY NNKO

KAMATI ya Sera ya Fedha (MPC) imeridhishwa na utekelezaji wa sera ya fedha iliyolenga kupunguza ongezeko la ukwasi kwenye uchumi ili kukabiliana na kasi ya mfumuko wa bei nchini.

Hayo yamebainishwa leo Machi 14, 2023 na Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tututba kupitia tamko la MPC ambayo ilikutana leo kwa lengo la kutathmini utekelezaji wa sera ya fedha katika miezi Januari na Februari 2023.

Sambamba na mwenendo wa uchumi, na kufanya maamuzi ya mwelekeo wa utekelezaji wa sera ya fedha kwa miezi miwili ijayo.

MPC imebainisha kuwa, kufuatia utekelezaji thabiti wa sera ya fedha, mfumuko wa bei umeendelea kubakia ndani ya malengo, na kiwango cha ukwasi kikiendana na mahitaji halisi ya shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Hali iliyochochea ongezeko la ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi, na kuweka mazingira ya kuendelea kuimarika kwa shughuli za kiuchumi nchini.

Vilevile, utekelezaji huu wa sera ya fedha umesaidia kufikiwa kwa vigezo vilivyowekwa katika makubaliano ya programu na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) chini ya Mpango wa Extended Credit Facility (ECF) kwa mwezi Desemba 2022, na kuendelea kupunguza athari za kiuchumi zitokanazo na mitikisiko ya kiuchumi duniani, hususani athari za ongezeko la bei za bidhaa katika soko la dunia.

Kuhusu mwenendo wa uchumi, kamati ilibaini kuwa mwaka 2022 uchumi wa Dunia uliathiriwa na mitikisiko ya kiuchumi na changamoto za mabadiliko ya tabia ya nchi.

Aidha, kutokana na haya, kasi ya ukuaji wa uchumi wa dunia inatarajiwa kupungua mwaka 2023, kabla ya kuongezeka tena mwaka 2024.

Bei za bidhaa katika soko la Dunia ziliendelea kuwa juu katika mwaka 2022, japo zilianza kupungua katika kipindi cha nusu ya pili ya mwaka.

Kutokana na hali hiyo, mfumuko wa bei umeendelea kupungua tangu robo ya mwisho ya mwaka 2022, japo umebaki juu ya malengo ya benki kuu za nchi nyingi, hususani mataifa yaliyoendelea.

Aidha, kamati ilibaini kuwa, mwenendo wa uchumi nchini umeendelea kuwa wa kuridhisha, huku viashiria mbalimbali vya shughuli za kiuchumi vikionesha matarajio chanya kwa kipindi kijacho.

Kwa kuzingatia kasi ya wastani wa ukuaji wa uchumi wa asilimia 5.2 katika robo tatu za kwanza za mwaka 2022 kwa Tanzania bara, kuna uwezekano mkubwa ukuaji wa uchumi ukafikia asilimia 5 kwa mwaka 2022, kiwango ambacho ni juu ya makadirio ya awali ya ukuaji wa asilimia 4.7.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news