Rais Dkt.Mwinyi atoa wito kwa wadau wote wa Kiswahili

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi ametoa rai kwa wataalamu wa lugha ya Kiswahili wakiwemo wahadhiri, walimu,  waandishi wa habari, watangazaji na wakalimani kuchangamkia fursa zilizopo kupitia Kiswahili zinazoendelea kuongezeka duniani. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akihutubia na kulifungua Kongamano la Idhaa za Kiswahili Duniani. Linalofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Sheikh Idrissa Abdulwaki Kikwajuni Wilaya ya Mjini Unguja jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu).

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo Machi 18, 2023 alipofungua Kongamano la Idhaa za Kiswahili kwa Mwaka 2023, lililofanyika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul-Wakil jijini Zanzibar.Kongamano hilo la Idhaa za Kiswahili Duniani linaongozwa na kauli mbiu ya Kiswahili ni Nyenzo ya Mawasiliano Tujiamini Kukitumia.

Amesema, lugha ya Kiswahili inaendelea kukua na kuwa ni bidhaa muhimu ya mawasiliano kimataifa. Hata hivyo bado inaonekana mwamko mdogo kwa watu katika kuzichangamkia fursa zilizopo.
Pia, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema,lugha ya Kiswahili ni lugha ya Taifa ambayo inatumika katika shughuli mbalimbali, hivyo ipo haja kwa vyombo vya habari kuitumia ipasavyo katika matamshi yake, kwani kufanya hivyo kunapelekea kuikukuza zaidi.
Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema,maarifa yatakayopatikana katika kongamano hilo yatawasaidia wanahabari nguli na chipukizi kuhamasisha kutumia lugha hiyo katika jamii na kuiendeleza.
Kwa upande wake, Waziri wa Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo, Mhe.Tabia Maulid Mwita amewataka waandishi wa habari kushirikiana na Baraza la Kiswahili kuweza kupata tafsiri za maneno ili kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.
Mheshimiwa Waziri amesema, wizara inaendelea kuiendeleza lugha hiyo ingawa kuna baadhi ya changamoto zinajitokeza kutokana na utandawazi ambao unapelekea kukichafua Kiswahii jambo, ambalo linarejesha nyuma jitihada hizo.

Mwenyekiti Baraza la Kiswahili, Saade Said Mbarouk amesema, jambo la kufurahisha ni kuona idhaa za Kiswahili zinatumia lugha hiyo, kwani zimesaidia kukuza na kukieneza kwa kasi duniani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news