Rais Dkt.Nabiijoshua apuliza kipenga kuelekea Siku ya Kitaifa ya Kongamano la Mashangilio kwa Umoja wa Mitume na Manabii Tanzania (UMMT)

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Umoja wa Mitume na Manabii Tanzania (UMMT), Dkt.Nabiijoshua Aram Mwantyala amesema, Aprili Mosi, mwaka huu itakuwa ndiyo Siku ya Kitaifa ya Kongamano la Mashangilio litakalofanyika katika Ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam.
Hayo ameyasema leo wakati akielezea kuhusiana na maandalizi ya kongamano hilo kubwa ambalo linatajwa kuwa la kihistoria na la kwanza kwa mitume na manabii kufanyika nchini.

Dhamira ya umoja huo ambao unalenga kuwaleta pamoja mitume na manabii kwa ajili ya kueneza habari njema ya neno la Mungu nchini, kuombea, kuwezeshana, kuwezesha wenye mahitaji mbalimbali pia umekusudia kushirikiana na Serikali kuhakikisha wanatekeleza miradi ya maendeleo kwa manufaa ya jamii na Taifa kwa ujumla.
Hivi karibuni,Dkt.Nabiijoshua Aram Mwantyala ambaye ni Kiongozi Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania alitwaa asilimia 80 ya kura katika uchaguzi wa nafasi ya urais katika Umoja wa Manabii na Mitume nchini Tanzania (Unity of Apostles and Prophets Tanzania).

Ushindi huo ulitokana na kura 179 alizopata huku akiwaacha mbali washindani wake akiwemo Mchungaji Ceasar Masisi aliyepata kura 42 na Mtume Joackim Kimanza aliyepata kura nne kupitia uchaguzi uliofanyika katika Ukumbi wa Anatoglo uliopo Ilala, Dar es Salaam.
Kwa matokeo hayo, Askofu Profesa Rejoice Ndalima alimtangaza rasmi Dkt.Nabiijoshua Aram Mwantyala kuwa Rais wa Umoja wa Mitume na Manabii nchini Tanzania.

Aidha, mitume na manabii mbalimbali nchini walionesha imani kubwa juu ya Dkt.Nabiijoshua huku wakimpongeza na kuahidi kumpa ushirikiano mkubwa aweze kutekeleza jukumu lake la kuwaunganisha viongozi hao wa kiroho ili waweze kulihubiri neno la Mungu kwa ufanisi nchini.
"Habari njema ni kwamba, Aprili Mosi, mwaka huu siku ya Jumamosi itakuwa ni Siku ya Kitaifa ya Kongamano la Mashangilio kwa Manabiii na Mitume Tanzania,kongamano hili litahudhuriwa na wazee wetu, waasisi wa injili ya kitume na kinabii katika Taifa la Tanzania, tutakuwepo na mzee wetu Apostle Dustan Maboya atakuwepo kwenye ukumbi siku hiyo, Baba yetu Mtume na Nabii Mwingira atakuwepo.

"Mheshimiwa Askofu Gwajima atakuwa pamoja na sisi, ninafurahi kwa sababu Mzee wetu Anthony Lusekelo atakuwepo na sisi. Kongamano hili litakuwa la kipekee, kwa sababu imeandikwa na nami nitaigeuza mioyo ya watoto waelekee baba zao, na mioyo ya mababa ielekee watoto wao.

"Wazee wako tayari kutushika mkono na kutuongoza, watuambie walitoka wapi, tuko wapi, watuambie tunakwenda wapi. Kwa hiyo mitume na manabii kote Tanzania ninawaomba msikose kufika, ninawaagiza wenyeviti wa wilaya, wenyeviti wa mikoa nchini kote anzeni sasa maandalizi, ya kuja pamoja jijini Dar es Salaam kwenye Ukumbi wa Ubungo Plaza kuanzia saa mbili asubuhi mpaka saa 12 jioni tutakuwa tunashangilia wema wa Mungu wa baba kukaa na watoto, Mungu awabariki sana,"amefafanua Rais UMMT, Dkt.Nabiijoshua Aram Mwantyala.
Ubungo Plaza panatajwa kuwa ni mahali pazuri sana kusherehekea hafla nyakati zote kwa sababu iko katikati ya jiji, na mawasiliano mazuri, maegesho, lifti na huduma zingine ambazo husaidia kuwezesha kila kitu unachohitaji kufurahia wakati wako.

Pia ni eneo rafiki kwa mtu yeyote anayefika kwa mara ya kwanza katika Jiji la Dar es Salaam, kwani hawezi kupata usumbufu wa kuuliza au kutoka kutafuta malazi nje ya eneo iwapo itamlazimu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news