Simba SC yatinga kibabe robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika

NA DIRAMAKINI

KLABU ya Simba ya jijini Dar es Salaam imefanikiwa kutinga robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika baada ya kuifunga Horoya FC mabao 7-0.

Ni kupitia mchezo uliopigwa leo Machi 18, 2023 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam. Katika mchezo huo wa aina yake, kiungo mshambuliaji Clatous Chama amepiga hat trick.

Chama aliwapatia Simba bao la kwanza dakika ya 10 kwa shuti kali la mpira wa adhabu nje ya 18 baada ya Jean Baleke kufanyiwa madhambi.

Naye Baleke aliwapatia Simba SC bao la pili dakika ya 32 baada ya shuti kali lililopigwa na Kibu Denis kupanguliwa na mlinda mlango wa Horoya kabla ya kumkuta mfungaji.

Aidha, Chama aliwapatia Simba SC bao la tatu kwa mkwaju wa penati dakika ya 36 baada ya mlinzi wa Horoya Abdoulaye Camara kuunawa mpira ndani ya 18.

Kipindi cha pili,Simba SC walirudi kwa kasi ambapo dakika ya 53 Kiungo Sadio Kanoute aliwapatia bao la nne akipokea pasi ya upendo kutoka kwa Chama.

Baleke aliongeza bao la tano dakika ya 65 kufuatia Chama kumpoka mpira mchezaji wa Horoya kabla ya kumkuta mfungaji ambaye alimchambua mlinda mlango.

Pia, Chama aliwapatia bao la sita dakika 70 na kukamilisha hat trick yake baada ya kumlamba chenga mlinzi wa Horoya ndani ya 18 akimalizia pasi safi kutoka kwa Pape Sakho.

Wakati huo huo, Kanoute alipigilia msumari wa moto wa saba kwa shuti kali nje ya 18 dakika ya 86 akimalizia pasi ya upendo kutoka Shomari Kapombe.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news