TAJIRI MTOTO ALIYEFAULISHWA KWA DHARURA-2

NA MARTIN SHABOKA

"Siku moja yule mama wa mtoto akiwa pale Car Wash akaja mwanamke wa makamu kidogo na kumsalimia, na baada ya salamu akajitambulisha kama nesi aliyemsaidia siku alipokuwa anajifungua, kisha akamuomba msamaha sana na kumwambia kuwa yule mtoto hakuwa wake, yeye mtoto wake alikufa ila mtoto huyo walimpa kwa sababu mama yake alikufa akiwa anajifungua hivyo wakaona ni vyema wampe yeye aliye hai ili mtoto asije akaishi kwa mateso.Mama akachanganyikiwa sana kwa taarifa hiyo." Endelea...
Mama akachanganyikiwa sana kwa taarifa aliyopewa na yule aliyejitambulisha kama nesi, akainuka na kwenda chooni kisha akalia sana, baada ya muda akarudi na kuendelea na maongezi na yule nesi, akamuomba chondechonde taarifa hii isije ikavuja na kumfikia mwanae, tajiri mtoto maana alihisi kuwa inaweza kumuharibu kisaikolojia.

Wakabadilishana namba na yule nesi mstaafu kisha mama mtoto akampatia shilingi laki mbili kama shukrani ya huduma aliyompatia miaka mingi iliyopita.

Tangu siku hiyo mama akawa hana amani sana moyoni, akaanza kunywa wine mara kwa mara huku taarifa aliyoipata akiifanya kama siri kati yake yeye na yule nesi.

Baada ya miezi miwili tajiri mtoto alipanga safari ya kuja Tanzania na mke wake wakitokea Msumbiji, na tayari mke wake alikuwa na mtoto mmoja wa kiume pamoja na uja uzito wa miezi saba, alikuwa ni mmakonde wa Msumbiji, lakini alikuwa na ndugu zake Tanzania ambao amekuwa akiwasiliana nao tu kwa simu ila hajawahi kuonana nao, isipokuwa shangazi yake ambaye amewahi kwenda Msumbiji zamani.

Tajiri akamwambia mke wake kuwa, kwa jinsi alivyoteseka na mama yake pamoja na dada yake anataka kwenda Tanzania kumpa zawadi mama na dada yake kama shukrani ya kusimama nae mpaka hapo alipofikia.

Mke wake aliafiki safari hiyo na akasema itakuwa advantage pia kwa mtoto wake kuwafahamu ndugu zake, lakini pia kwake yeye kuwajua baadhi ya ndugu zake walioko Tanzania, na makubaliano yao walipanga zawadi hiyo itolewe siku ya kumbukizi ya kuzaliwa mama wa mume wake.

Baada ya miezi miwili walipanda ndege kimya kimya kutoka Msumbiji kuja Tanzania, na wakafikia hoteli moja ya kifahari kwa ajili ya maandalizi ya birthday ya mama.

Tajiri akamuita dada yake pale hotelini bila kutaka mama yake ajue kama kuna kitu kinaendelea, na akampanga dada yake afanye maandalizi kwa ukubwa kwa ajili ya birthday ya mama yao.

Dada mtu alifurahi sana kumuona wifi yake na mtoto wao na pia akamuahidi kaka yake kuitunza hiyo siri.

Maandalizi yaliendelea kimya kimya pasipo mama mtu kujua, ukatafutwa ukumbi mzuri na wapishi wazuri kabisa, tajiri mtoto akanunua gari mbili mpya, moja ni Land Cruiser V8 toleo jipya, pamoja na Harrier nyeusi.

Siku moja kabla ya sikukuu, mke wa tajiri akawasiliana na shangazi yake ambaye alikuwa mkoani na akamsisitiza sana kwamba ajitahidi waonane na kama itawezekana afike kwenye sherehe hiyo, na akamuwezesha nauli.

Kesho yake maandalizi yakiwa yamepamba moto, mida ya saa kumi na mbili jioni Joyce dada pekee wa tajiri akamwambia mama yake, ''Mama kuna sehemu nataka twende unisindikize ni muhimu sana." lakini mama akaonyesha kuchoka na akamwambia, "Kwa leo sitaweza nahitaji kupumzika mapema."

Joyce akambembeleza sana mama yake hadi kufikia mida ya saa moja na nusu jioni ndiyo mama akakubali kwenda.

Huku ukumbini mambo yamepamba moto, watu wamejaa,shangwe nderemo na vifijo vinaendelea, ilibamba kweli kweli...Joyce na mama yake wakafika ukumbini na kukaa meza ya nyuma kabisa, hakuna aliyejua sherehe ile inahusu nini zaidi ya Joyce, Kaka yake, na wifi yake.

Mama akamuuliza Joyce, "Hapa kuna nini?" Ikabidi Joyce amdanganye kwamba ni sherehe ya rafiki yake anavalishwa pete ya uchumba.

Baada ya muda Joyce akatoka nje na kumpigia simu kaka yake kumtaarifu kwamba, mama tayari yuko ukumbini, ndipo tajiri na mke wake na mtoto wao, pamoja na shangazi ya mke wake ambaye alikuwa amewasili kutoka mkoani wakaanza safari ya kwenda ukumbini.

Walipofika ukumbini mama alipowaona tu akashtuka na kupoteza fahamu. Wakambeba na kumpeleka chumba cha ukumbini kwa ajili ya huduma ya kwanza, na alipozinduka akawaomba watoto wake na mka mwana watoke na kumuacha na shangazi wa mke wa mwanae.

Walipotii na kutoka ndipo mama akamuuliza shangazi mtu kuwa, "Mbona unanifanyia hivi? Si nilikuomba jambo hili liwe siri yetu?" Shangazi akamjibu, "Mimi mwenyewe nimealikwa na mtoto wa kaka yangu ambaye anaishi Msumbiji, nimeshangaa sana kukukuta hapa."

Kumbe shangazi wa mke wa tajiri ndiyo yule nesi aliyevujisha siri ya kwamba tajiri siyo mtoto wa kuzaliwa na yule mama.

Walikubaliana mule chumbani kwamba chondechonde taarifa hii iendelee kuwa siri kati yetu, na nesi akaafiki, ndipo mama akapata nguvu ya kusimama na kutoka mule chumbani na kwenda ukumbini.

Sherehe iliendelea japo kulikuwa na mshtuko kidogo, mama alipokaa kwenye meza yake, tajiri akashika kipaza sauti na kuweka wazi juu ya kinachoendelea, "Mabibi na mabwana karibuni sana kwenye sherehe hii ambayo ni maalumu kabisa kwa ajili ya mama yangu.

"Leo ni siku muhimu sana kwake ya kumbukizi ya kuzaliwa kwake. Nimeona nichukue fursa hii kumshukuru kwa upendo wake mkubwa sana kwangu, amenilea kwa shida kwa kutoa kila alicho nacho ili niweze kupata msingi mzuri wa maisha.

"Leo na mimi ni miongoni mwa vijana waliofanikiwa kiasi, ila ninaamini mafanikio yangu yamechangiwa sana na malezi ya mama yangu aliyenifundisha kujitegemea. Namshukuru Mungu nina uwezo wa kuishi vizuri na watu, maana katika makuzi yangu pia baada ya baba kunikataa nimesaidiwa sana na watu, hivyo niko hapa kuwashukuru wote, wafanya kazi katika kampuni yangu, wauzaji wenzangu wa madini, majirani zangu, wajomba zangu, lakini zaidi nawashukuru sana mama yangu na dada yangu Joyce ambao mmekuwa na mimi bega kwa bega.

"Mke wangu Mercy na mtoto wangu Johnson sijawasahau maana ninyi ni sehemu ya maisha yangu. Kwa kusema haya naomba nisiwe na shukrani ya maneno matupu kwa mama yangu na dada yangu, naomba wahusika mlete zawadi zao hapa".

Baada ya maneno hayo zikaletwa gari mbili ukumbini, mpya kabisa, ukumbi ukalipuka kwa shangwe, mama na dada mtu wakalia machozi ya furaha, lakini shangazi yake na mke wa tajiri akamwangalia usoni mke wa tajiri na kuonyesha kama mshangao wa kutofurahia tukio hilo..

Baada ya hapo mama mtu akapewa kipaza sauti, akaanza kusema, "Mwanangu nakushukuru sana, sikutegemea hata siku moja kuishi maisha haya, nakosa la kusema ila nakushukuru sana, Mungu akubariki sana.

Nimefurahi kumuona mjukuu wangu na mkamwana wangu karibuni sana nyumbani...Wakati mama anaendelea kuongea shangazi akamfuata mke wa tajiri na kumnong'oneza jambo.

ITAENDELEA.....

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news