Rais Dkt.Mwinyi:Kuhodhi vyakula vipande bei ni uhujumu uchumi, Serikali haitakubali

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema, Serikali itawachukulia hatua kali ikiwemo kuwafungulia kesi za uhujukumu uchumi wafanyabiashara watakaobainika kwa makusudi wanaficha vyakula na bidhaa kwa lengo la kuwapandishia bei wananchi.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vilivyopo Zanzibar ikiwa ni kawaida yake ya kuzungumza na Waandishi wa habari na Wahariri wa vyombo vya habari kila mwisho wa mwezi, mkutano huo uliofanyika Februari 28, 2023 katika Ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar. (Picha na Ikulu).
 
Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo kwenye mkutano wake wa kila mwisho wa mwezi na wahariri na waandishi wa habari uliofanyika Ikulu jijini Zanzibar.
Waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vya habari vilioko Zanzibar wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) akizungumza wakati wa mkutano wake wa kila mwisho wa mwezi na waandishi.
 
Amesema, kuelekea mwezi Mtukufu wa Ramadhani siku chache zijazo, Serikali imejihakikishia kuwepo kwa bidhaa nyingi ikiwemo vyakula kama unga wa ngano, mafuta ya kupikia, sukari na mchele kukidhi mahitaji ya mfungo wa Ramadhani.

Pia amesema, Serikali haitarajii kuibuka kwa mfumuko wa bei ama bidhaa kuadimika hali itakayosababisha taharuki kwa wananchi na waumini wa dini ya Kiislam ambao watakuwa wakitekeleza ibada ya Swaumu.

Rais Dkt.Mwinyi amesema kipindi kifupi kilichopita baada ya mkutano wake na wafanyabisahara mbalimbali wa vyakula kufuatia kupanda kwa bei za bidhaa za vyakula, ghafla vyakula vilienea nchi nzima na kuonya kwa mfanyabiashara atakayebainika anaficha vyakula kwa nia ya kujinufaisha, Serikali haitosita kumfungulia kesi ya uhujumu uchumi.

“Kuhodhi vyakula ili vipande bei ni uhujumu uchumi, atakaeficha vyakula kutamshitaki kwa kosa la uhujumu uchumi, tumetaarifiwa, mchele upo, sukari ipo, ngano ipo na mafuta ya kupikia yapo kwaajili ya Ramadhani, tukikubaini umehodhi kwa lengo binafsi tutakushitaki kwa kosa la uhujumu uchumi” Alitahadharisha Dk. Mwinyi

Kuhusu mfumuko wa bei, Dkt.Mwinyi alisema sio tatizo la serikali bali linachangiwa na sababu mbalimbali za kidunia, alisema Zanzibar inaingiza mchele kutoka Pakistan ambako kumekumbwa na mafuriko.

Aidha, ngano kutoka Ukraine ambako nako kumbekumbwa na vita baina yao na Urusi hali iliyosababisha bei za vyakula kupanda na kuongeza kuwa kwa asilimia kubwa Zanzibar pia inategemea vyakula kutoka Tanzania Bara ambako kwa baadhi ya mikoa inayozalisha vyakula ilikumbwa na janga la ukame.
Mwandishi wa habari wa kujitengemea, Bw.Ligwa Paulin akiuliza swali katika mkutano wa Waandishi wa Habari wa vyombo mbalimbali vya habari viliopo Zanzibar, na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani).

Kuhusu bandari Malindi Rais Dkt.Mwinyi, alieleza Serikali inatambua ufinyu wa bandari hiyo unaosababishwa kuwa na gati moja hali inayosababisha usumbufu kwa kukawia kushushwa mizigo mingi kwa wakati, nakueleza mpango wa serikali kuondosha changamoto hizo kwa kukamilisha ujenzi wa bandari ya Mangapwani inatarajiwa kutoa huduma zote muhimu zikiwemo bandari za kushushia, vyakula, nafaka, mafuata na bandari nyengine lengo ni kuongeza kasi ya uendeshaji bandarini.

Aidha, Dkt.Mwinyi alieleza Serikali imechukua jitihada za dharura kwa kuagiza mashine za kisasa zenye wepesi wa kushushia makontena, kuendelea kulitumia eneo la Bwawani kuhifadhia makontena na kutumia bandari ya Mpigaduri kushushia mizigo ili kupunguza msongamano kwa bandari ya Malindi.

Alieleza kukamilika bandari ya Mangapwani kutatoa fursa kwa bandari ya Malindi kutumika kuwa bandari ya utalii kwa kupakia na kushushia masuala yanayohusu utalii pekee.
Mwandishi wa Habari wa Azam TV, Bi. Mtumwa Said Nassir, akiuliza swali katika mkutano wa Waandishi wa Habari wa vyombo mbalimbali vya habari viliopo Zanzibar, na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) mkutano huo uliyofanyika katika Ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar.

Kuhusu masuala ya udhalilishaji, Rais Dkt.Mwinyi alivitaka vyombo vya sheria kuangalia kesi za watoto kati ya miaka 18 na 17, alieleza kumekuwa na malalamiko mengi kuhusiana na kesi hizo zinazodaiwa wasichana kuwatengenezea kesi za makusudi wavulana ambao wengi sheria huwatia hatiani, kwa kesi za udhalilishaji wa kinyama kwa watu wazima wanaume kuwadhalilisha watoto wachanga wa miaka 2 hadi 5 na zaidi, Rais Dkt.Mwinyi alivitaka vyombo hivyo kutofumbia macho kesi za aina hiyo wala kuzipa dhamana.

Akitoa ufafanuzi kwa watoa huduma wa kimataifa wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, kampuni ya kimataifa ya DNATA, kufuatia malalamiko yaliyotolewa na Chama cha upinzani cha ACT Wazalendo kwenye mkutano wao wa hadhara uliofanyika Nungwi mkoa wa Kaskazini Unguja,Rais Dkt.Mwinyi alieleza kipindi kifupi cha huduma zinazotolewa na kampuni ya DNATA, Serikali imengiza zaidi ya bilioni nane kwa robo mwaka ya kwanza ambapo inatarajiwa kuchangia zaidi ya bilioni 32 sawa na asilimia 12 kwa mwaka ikilinganishwa na kampuni wazawa walioongoza viwanja hivyo kwa zaidi ya miaka 25 ambao walikusanya bilioni mbili tu, sawa na asilimia 5 kwa mwaka.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akisisitiza jambo wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vilioko Zanzibar, ikiwa ni utaratibu wake wa kuzungumza na waandishi wa habari kila mwisho wa mwezi, mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar.
 
“Serikali ya Awamu ya Nane, imewapa kazi kampuni ya DNATA kuendesha Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume Terminal 3, hoja ACT kwa nini imepewa DNATA badala ya kampuni wazawa haina mantiki, kampuni za ndani zilitoa huduma kwa zaidi ya miaka 25 na serikali ilikuwa haipati kitu hata mishahara ya wafanyakazi Serikali ilitoa hazina, Serikali ilipata hasara tupu,”alifafanua Rais Dkt.Mwinyi.

Alisema kwa kipindi chote hicho hata mapato ya maegesho ya ndege ilichukua kampuni binafsi za ndani na hali ya uwanja wandege haikuwa kama sasa ilivyo ambapo Uwanja wa Ndege wa Zanzibar ni wa kwanza kwa ubora Tanzania nzima ikilinganishwa na viwanja vya ndege vya Dar es Salaam na Kilimanjaro.

Alieleza wanachokisema ACT Wazalendo hakina uhalisia na wala hawatetei kwa ajili ya maslahi mapana ya nchi wala kuitetea serikali bali ni kupotosha umma kwa maslahi yao binafsi hata hivyo, aliwafahamisha wananchi serikali inafanya yale ambayo nchi inataka kwa maslahi ya umma.

Kuhusu Serikali kuwaachia sekta binafsi kutoa huduma kwa wananchi, Dkt.Mwinyi alieleza ni mfumo mzuri wa kuendesha sekta za umma ili wananchi wanufaike na huduma za jamii, alieleza kwa sasa Serikali imeanza mfumo huo kwa Sekta ya Afya ambapo hospitali za serikali zitatoa huduma za vipimo na maabara kwa kusimamiwa na taasisi binafsi kisha Serikali itagharamia ili kuwaondoshea wananchi usumbufu wa kukosa huduma hizo.

Aidha,Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi alieza huduma hizo zitakua endelevu kwa tasisi nyingine za umma zinazotoa huduma za kijamii.

Katika hatua nyingine Rais Dkt.Mwinyi amevipongeza vyama vya siasa kwa kuanza mikutano ya adhara pia alivitaka vyama hiyo kuhubiri amani ya nchi badala ya kupotosha umma kwa mambo wanayofanyiwa na serikali yao na kuongeza kwamba hachukii kukosolewa, lakini watu wakosoe kwa kutengeneza hoja za msingi sio kuupotosha umma.

Alisema, demokrasia sio kuchochea, kueneza chuki kwa watu na kueleza masuala ya uvunjivu wa amani bali inataka kushirikiana, kueleza mambo yenye kutengeneza kwa mustakbali wa taifa na sio kupotosha umma.

Aliwatanabahisha wanasiasa wanaotumia majukwaa ya siasa kuwaaminisha umma masuala wasiyo na hakika nayo na kuwashauri kufanya uchunguzi wa kina ili kuwaelewesha wananchi mambo yenye ukweli na sio kuwapotosha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news